Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko 2021: Ni mwaka wa kipekee
Habari MchanganyikoTangulizi

2021: Ni mwaka wa kipekee

Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Magufuli
Spread the love

 

SAFARI ya siku 365 za mwaka 2021, zitahitimishwa siku kumi zijazo huku wananchi wakiwa na kumbukumbu ya tukio kubwa na la kwanza kutokea nchini. Anaandika Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ni tukio lilitokea saa 12 jioni ya tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, iliyopo Makumbusho jijini Dar es Salaam, kwa Rais aliyekuwa madarakani, Dk. John Pombe Magufuli kufariki dunia.

Vilio, majonzi na simanzi vilitawala kuanzia usiku wa saa tano siku hiyo, pale Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa makamu wa Rais alipoutangazia umma juu ya kifo hicho, kilichoambatana na siku 21 za maombolezo.

Mwili wa Dk. Magufuli baada ya kuagwa Dar es Salaam, Zanzibar, Dodoma, Mwanza na nyumbani kwao Chato mkoani Geita, ulipozikwa tarehe 26 Machi 2021.

Kifo hicho cha Dk. Magufuli, kilihitimisha safari yake ya urais ya miaka mitano na miezi minne, aliyokuwa ameianza tarehe 5 Novemba 2015, akipokea kijiti kutoka kwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Muonekano wa kaburi la Hayati John Magufuli

Samia, aliyekuwa makamu wa Rais, aliapishwa tarehe 19 Machi 2021, kuwa Rais kwa mujibu wa Katiba, Ikulu jijini Dar es Salaam na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma.

Samia alijiwekea rekodi nyingine ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke tangu Taifa hili lipate uhuru mwaka 1961. Awali, aliweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa Rais.

MwanaHALISI TV limezungumza na Mkurugenzi Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku na Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. George Kahangwa waliosema, kifo hicho kimeacha funzo kwa wananchi na viongozi wanaopata nafasi ya kuwatumikia wananchi.

Butiku anasema kifo hicho kimetufunza “hakuna anayejua atakufa lini, atakufa kwa nini na akifa nini kitatokea. Hiki hatukuzoea kwa Rais aliyeko madarakani, lakini yeye ni binadamu.”

Rais Samia Suluhu Hassan akiweka shada la maua katika kaburi la Hayari John Magufuli

Dk. George Kahangwa anasema, “kumpoteza Rais ni jambo kubwa sana ambalo lilitushitua sana watu wa kada mbalimbali.”

“Kila mmoja aliguswa kwani hatukuwahi kupata kitu kama hiki. Lakini lilitukumbusha juu ya asili yetu sisi wanadamu kwamba kifo hakijali nani ni nani,” anasema.

Dk. Kahangwa alisema, “maisha yetu binadamu ni kiumbe dhaifu na wakati wowote anaweza kupoteza maisha. Ni lazima kuishi kwa kupendana, kujaliana, kuheshimiana na kutobaguana.”

Mwaka huu pia, tumeshuhudia vifo vya watu maarufu kama wanasiasa, wafanyabiashara, wasanii na wanamichezo vikitokea.

Tarehe 17 Februari, saa 5 asubuhi, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, taifa lilimpoteza Jabari wa siasa hususan Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Maalim Seif, aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais Zanizbar na mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo alifikwa na mauti hospitalini hapo, baada ya kuugua corona. Mwili wake ulizikwa nyumbani kwao Pemba.

Maalim Seif Sharrif Hamad, Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Siku hiyohiyo, kigogo mwingine aliyefariki dunia alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, aliyefikwa na mauti katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma na mwili wake ulizikwa kwao Tanga.

Mwezi huohuo, tarehe 22, uliendelea kukumbwa na majonzi baada ya Profesa Benno Ndullu, aliyewahi kuhudumu nafasi ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alipofariki dunia katika Hospitali ya Kairuki, Dar es Salaam.

Februari utabaki kuwa mwezi wa kipekee mwaka huu kwani ikishuhudia ikipoteza wachumi mashuhuru kwa aliyewahi kuwa katibu mkuu wa wizara ya fedha na mipango, Dk. Servacius Likwalile kufariki dunia, tarehe 20 katika Hospitali ya Regency, Dar es Salaam.

Tarehe 12 Februari, Mbunge wa Muhambwe mkoani Kigoma (CCM), Atashasta Nditiye aliyekuwa naibu waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano alifariki dunia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya ajali aliyopita.

Mawaziri wengine waliofariki mwaka huu; ni Elias Kwandikwa wa Ushetu mkoani Shinyanga ambaye alikuwa waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa, aliyefariki tarehe 3 Agosti pamoja na Wilium Ole Nasha, mbunge wa Longido, Arusha ambaye alikuwa naibu waziri wa uwekezaji kufariki 27 Septemba, akiwa nyumbani kwake, Dodoma.

Mbunge wa Konde (ACT-Wazalendo), Said Khatibu Haji, alifikwa na mauti 19 Mei, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.

Marehemu Profesa Mwesiga Baregu

Wanasiasa wengine waliofariki; ni aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, aliyefariki tarehe 22 Julai, Hospitali ya Maunt Meru, Arusha. Enzi za uhai wake, aliwahi kuwa mwenyekiti wa ACT-Wazalendo na mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Mwanachama wa Chadema na mwanazuoni maarufu nchini, Profesa Mwesiga Baregu alifariki 13 Juni, katika Hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu. Mwili wake ulizikwa nyumbani kwao Bukoba mkoani Kagera.

Mwanazuoni mwingine aliyefariki mwaka huu ni Profesa wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (Ruco), mkoani Iringa, Gaudence Mpangala aliyefikwa na mauti ghafla akiwa jijini Dodoma, 4 Februari.

Marehemu Zacharia HansPope

Sekta ya ujenzi ilikuwa na majonzi ambapo tarehe 29 Juni, baada ya Mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale kufariki ghafla jijini Dodoma akiwa katika kikao.

Tarehe 20 Septemba, sekta ya michezo ilimpoteza miongoni mwa wadau wakubwa, Zacharia Hans Pope, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili wa Simba na mwili wake kuzikwa nyumbani kwao, Iringa.

Kwenye burudani, Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ilunga Khalifa maarufu C-Pwaa alifariki dunia 17 Januari.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!