July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

2015; mwaka wa kulia waliojisahau

Katibu Mkuu wa CCM, Abrahaman Kinana (katikati) akiwa na wanachama wa CCM katika moja ya ziara zake

Spread the love

KUJISAHAU kubaya. Mtu aliyejisahau katika jamii; iwe mahali pa kazi au uraiani huwa hafikiri zaidi ya leo.

Kwa bahati mbaya sana mtu aliyejisahau awe ofisa au mkurugenzi au raia tu, huwa hajijui, hivyo haoni alama za nyakati wala onyo.

Mtu aliyejisahau huwa hafikirii kwamba kesho anaweza kustaafishwa au kuachishwa kazi naye akabaki hohehahe. Mlevi wa madaraka ni kati ya waliojisahau. Wababe hujisahau kiasi cha kutoona uwezekano wa kupigwa.

Mwaka 1995 wahariri wangu walijisahau walipoandika kichwa cha habari kumkejeli Benjamin Mkapa alipojitosa kuwania urais.

Wana CCM kadhaa waliokwenda Dodoma kuchukua fomu wakiwemo jamaa waliojiita Boyz II Men waliandikwa vizuri. Lakini alipokwenda Mkapa, akisindikizwa na marafiki zake, kushoto Jenerali Ulimwengu na kulia Balozi Ferdinand Ruhinda, wahariri wangu waliandika “Mkapa naye ataka urais”.

Asubuhi, wakati wa kupitia magazeti (postmortem) ndani ya chumba cha habari, Mkapa alikuwa gumzo. Waliocheka, walicheka; walioguna, waliguna.

[pullquote]Wewee! Wenye CCM walikaa Dodoma wakaibuka na jina la Mkapa – na aliposhika hatamu, waliokuwa wakitamba makao makuu Lumumba walipukutishwa na wahariri wangu wakachukua ‘mdogomdogo.’[/pullquote]

Kujisahau kubaya. Juzi tu waliwekwa pale Lumumba – kina Tambwe Hiza – waliojiona miungu watu. Wako wapi leo? Wanaotesa ni Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

Nawaomba Kinana na Nape wafikirie mwaka 2015 ni nani ndani ya CCM atateuliwa kuwa rais? Wajiulize itakuwaje ‘mteule’ akiwa ni yule ambaye Nape alimshambulia kuwa ni fisadi? Ikitokea mteule ni aliyemshambulia wakati wa upanuzi wa jengo la Umoja wa Vijana, ataficha wapi uso wake?

Kinana na Nape watajificha katika shimo lipi ikiwa walioitwa mawaziri wachovu, mmoja wao akaibuka kidedea?

Pia, CCM wajiulize, itakuwaje waking’olewa? Leo, hawafikirii hilo kwa vile wamejimilikisha nguvu za kuumba wanalotaka. Lakini itakuwaje wakikosa mabavu haya mwakani? Hawafikirii hayo kwa vile wamejisahau.

Wamejisahau kwa vile wamenajisi akili za Watanzania. Mwaka 2009,  tulihamasishwa tupige kelele sana ilipoibuliwa kashfa ya Richmond na baadaye ilipopewa jina la Dowans. Lakini ilipobatizwa jina la Symbion Power, mbatizaji akiwa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, tumelazimishwa kuimba kampuni hiyo imeleta wokovu wa umeme.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2010 CCM walipinga wapinzani walipokuja na sera yao ya kuhakikisha nyumba za tembe zinaisha na kutoa elimu bure. CCM walidai haiwezekani, lakini leo, wamegeuka wanasema watatoa elimu bure na upo mkakati wa kumaliza nyumba za tembe nchini.

Tazama, serikali imezuia mikutano yote ya siasa katika mikoa ya Lindi na Mtwara kufuatia sintofahamu iliyojitokeza mwaka jana kuhusiana na masuala ya gesi. Lakini kila mmoja ni shahidi, mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM kutoka Lindi, Salma Kikwete anafanya mikutano na kupokewa kwa maandamano; amri haimhusu isipokuwa wapinzani.

Ujumbe wa Kinana ulipita katika mikoa hiyo na kufanya mikutano ya ndani na nje. Kwa CCM sawa, wapinzani hapana.

Bungeni wamejipa haki ya kutengeneza kanuni inayoruhusu wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba walioko Hijja kupiga kura, kwa madai ni haki yao ya msingi. Lakini mbona wajumbe hao hao wanapinga haki ya msingi ya kupata habari iliyofafanuliwa vizuri katika Katiba?

Wakati umefika Watanzania kusema imetosha kuchezewa akili zetu na CCM. Tuseme kujisahau basi. Huu ni ushauri wa bure.

Makala hii imeandikwa na Joster Mwangulumbi

error: Content is protected !!