Saturday , 13 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya uchochezi MAWIO danadana
Habari za Siasa

Kesi ya uchochezi MAWIO danadana

Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki (kulia) akiteta jambo na Wahariri gazeti Mawio, Jabir Idrissa (kushoto) na Simon Mkina walipokuwa mahakamani Kisutu
Spread the love

KWA mara ya pili sasa, kesi inayohusu tuhuma za uchochezi ambayo inawakabili waandishi wa habari waandamizi nchini akiwemo Mhariri Mtendaji wa gazeti la MAWIO, Simon Mkina, imeahirishwa kwa sababu Tundu Lissu, mtuhumiwa wa nne, hayupo nchini, anaandika Faki Sosi.

Lissu, mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amekosekana mahakamani kwa kuwa anatibiwa majeraha nje ya nchi yanayotokana na kushambuliwa kwa risasi alipokuwa anawasili nyumbani kwake Area D, mjini Dodoma, akitokea kuhudhuria kikao cha Bunge.

Tukio hilo lililofanyika kiasi cha saa 7 mchana siku ya tarehe 7 Septemba mwaka huu, lilishtua umma na mpaka sasa hakuna taarifa za kukamatwa mtu yeyote kuhusiana na shambulio hilo. Lissu pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Ikiwa ni zaidi ya mara 12 kesi hiyo kufikishwa mahakamani, ililazimu kupangwa siku nyingine baada ya upande wa mashitaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde, kueleza kuwa Lissu hayupo kwa vile anapatiwa matibabu nje ya nchi.

Mbali na Mkina na Lissu, kesi hiyo Na. 208 ya mwaka 2016, inawakabili pia Jabir Idrissa, mwandishi wa habari iliyohusu uchaguzi wa Zanzibar ambayo ndiyo imetumika kufungulia mashitaka, na Ismail Mehboob, meneja wa kiwanda cha uchapishaji magazeti cha Flint.

Wakati ikipangiwa siku nyingine ya kutajwa, kwa mara ya kwanza Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba anayesikiliza kesi hiyo, amesema kesi hiyo inapaswa kuwa miongoni mwa kesi zinazofanyiwa utaratibu wa kuondolewa kwa vile imeshapita muda wa kubaki mahakamani.

Hakimu Simba amesema kesi hiyo iliyoanza Juni mwaka uliopita, imeshapita muda unaotakiwa kubaki mahakamani lakini inaahirishwa kwa sababu inajulikana mtuhumiwa mmoja hayupo.

Akimuelekea wakili wa serikali, Elizabeth Mkunde, Hakimu Simba alisema tangu usikilizaji kuanza, imeshapita miezi sita inayoelekezwa na taratibu za usikilizaji kesi za jinai, hivyo upande wa mashitaka unashauriwa kuiondoa.

Mashtaka yanayowakabili

Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashitaka manne:

Kupanga njama za kutoa chapisho la uchochezi, kosa linalodaiwa kutendwa kati ya tarehe 12 na 14 Januari 2016 linalowahusu Jabir, Mkina na Lissu wanaodaiwa kupanga njama za kuchapisha taarifa za uchochezi katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam.

Shitaka pili linawakabili Jabir, Mkina na Lissu, wakidaiwa kuchapisha chapisho la uchochezi katika gazeti la MAWIO, toleo Na. 182 la tarehe 14-20 Januari 2016.

Shitaka la tatu linamkabili Ismail peke yake anayedaiwa kuchapisha gazeti la MAWIO lenye kichwa cha habari “Machafuko yaja Z’bar” bila ya kupeleka kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Shitaka la nne linawakabili Jabir, Mkina na Lissu wakidaiwa kuchochea hofu miongoni mwa wananchi kwa kuchapisha habari hiyo ambayo “ingeweza kuzua vita au umwagaji damu.”

Habari iliyobeba kichwa cha maneno “Machafuko yaja Z’bar” ilihusu maelezo kwa njia ya maoni binafsi ya watu akiwemo Lissu.

Maoni ya Lissu yalilenga kumsihi Rais Dk. John Magufuli kutokana na nafasi yake ya amiri jeshi mkuu, kuchukua hatua ya kuepusha machafuko.

Kwamba aingilie kati kutatua mgogoro wa kisiasa uliozuka Zanzibar baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutoa tangazo tarehe 28 Oktoba 2015, la kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba 2015.

Wengine waliokuwa na maoni katika habari hiyo ni Hassan Nassor Moyo aliyepata kuwa waziri katika Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad.

Uchaguzi ulifutwa na Jecha ambaye hana mamlaka ya kisheria ya kufanya hivyo; na alichukua hatua hiyo siku ambayo kulingana na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, Na 5 ya mwaka 1985, Tume ilitakiwa kutangaza mshindi wa urais.

Badala yake, Jecha alitangaza kufanyika kwa alichokiita “uchaguzi wa marudio” ambao ulifanywa tarehe 20 Machi 2016 huku CUF na vyama kadhaa vya upinzani vikiususia. Jecha alimtangaza Dk. Ali Mohamed Shein kuwa mshindi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Nchimbi aanika ugonjwa wa CCM

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emanuel Nchimbi,...

Habari za Siasa

Chadema yapuliza kipyenga uchaguzi viongozi kanda

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza maandalizi ya uchaguzi...

Habari za Siasa

CCM :Hatutaki ushindi wa makandokando uchaguzi Serikali za mitaa

Spread the loveCHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakihitaji ushindi wa makandokando katika...

Habari za Siasa

Makala: Puuzeni wanasiasa wanaojigamba wanaweza kubadili maamuzi ya mahakama

Spread the loveKATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),...

error: Content is protected !!