JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, limewakamata watuhumiwa 147 mkoani humo kwa kujihusisha na makosa mbalimbali ikiwemo ya dawa za kulevya aina ya heroin, bangi, mirungi na pombe haramu ya gongo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili tarehe 23 Agosti 2020, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Emmanuel Lukula amesema, watuhumiwa hao wanashikiliwa baada ya jeshi hilo kuanza msako mkali kuanzia 30 June hadi 22 Agosti 22 2020.
Amesema, watuhumiwa 51 wamekamtwa kwa kosa la kupatikana na bangi zenye uzito wa kilo 483 na gramu 270, watuhumiwa 42 kwa kukutwa na mirungi yenye uzito wa kilo 774 na gramu 80, watuhumiwa wanne kwa kosa la kustawisha mirungi kiasi cha miti 1,101.
Kamanda Lukula amesema, jeshi hilo limekamata watuhumiwa wawili kwa kukutwa na heroin yenye uzito wa gramu 4.15, watuhumiwa 49 kwa kukutwa na gongo lita za ujazo 830 pamoja na kukamata watuhumiwa watatu kwa kukutwa na mitambo sita ya kutengenezea gongo.
Amesema, uchunguzi utakapokamilika, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.
Leave a comment