August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Machinga ‘wakoga’ mabomu

ACP Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza

Spread the love

WAFANYABIASHARA ndogo (machinga) wametawanywa kwa mabomu baada ya kugoma kuondoka katikati ya jiji hilo kwa madai maeneo wanakopelekwa si rafiki kwa shughuli zao, anaandika Moses Mseti.

Mvutano huo ulianza jana saa mbili na nusu asubuhi katika nyumba ya ibada ya Wahindi iliyopo eneo la Makoroboi, Wilaya ya Nyamagana baada machinga kutakiwa kuondoka eneo hilo.

Mwanahalisi Online ilishuhudia mgambo wa Jiji la Mwanza na askari polisi waliokuwa na mabomu ya machozi na silaha za moto katika eneo hilo wakiwaamrisha machinga kuondoka.

Polisi baada ya kufika eneo hilo, walianza mazingumzo na machinga hao yaliyodumu kwa saa tatu bila muafaka na hivyo kuanza kwa vurugu.

Katika mazungumzo hayo, baadhi ya machinga walikubali kuondoka eneo hilo lakini wenzao waligoma na kuwashawishi wenzao kuanza vurugu upya kupinga kuondolewa eneo hilo.

Katika hatua hiyo, Jeshi la Polisi lililazimika kutumia nguvu za ziada kwa kupiga mabomu ya machozi matano kuwatawanya machinga hao waliosikika wakisema, “nyie ndo mtutafutie maeneo rafiki ya kufanyia biashara zetu.”

Wakizungumza baadhi ya machinga hao, Daud Chacha na Rehema Abdul wamesema kuwa, serikali inawaondoa katika eneo hilo kutokana na kuwathamini raia wa kigeni kuliko wazawa.

Wamesema kuwa, maeneo ambayo serikali inataka kuwapeleka sio rafiki kwa shughuli zao na kwamba, kama serikali ya awamu ya tano ina nia njema na wananchi wanyonge iwatafutie maeneo mazuri.

“Sisi machinga hatugomi kuondoka katika eneo hili, tatizo ambalo tunapelekwa sio rafiki, kama ni hawa wahindi huwa tunawapisha wanafanya ibada zao na tukapewa masharti ya kutopiga kelele na tukatekeleza,” amesema Abdul.

Hata hivyo wamesema kuwa, kama hawatatafutiwa maeneo rafiki, hawatakubali kuondoka katika eneo hilo lililopo katikati ya jiji na kwamba wapo tayari kufia eneo hilo.

Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza amesema kuwa, eneo hilo wanapofanyia shughuli machinga hao sio rasmi na kwamba, walipewa kwa muda ili watafutiwe maeneo yaliorasmi kwa biashara zao.

Amesema kuwa, hata machinga hao wakikataa kuondoka eneo hilo, watatumia njia nyingine ya kuwaondoa huku akisisitiza kwamba, wamevamia maeneo yasioruhusiwa kwa shughuli zao.

Kibamba aliyataja maeneo yaliotengwa na ofisi yake kuwa ni pamoja na Sinai (Mabatini) Community Centre (Mirongo) na maduka tisa (Nyasaka) ambayo tayari yametengwa kwa ajili yao machinga.

Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza alipotafutwa kuzungumzia kama kuna athari za kibinadamu zimetokea, amesema kuwa polisi imeingilia baada ya machinga hao kuanza vurugu.

Kamanda Msangi amesema kuwa, katika vurugu hizo watu wanane wamekamatwa na wapo katika Kituo cha Polisi kati huku akiwataka machinga kutumia kauli ya Rais John Magufuli ya kufanya biashara katikati ya jiji vizuri.

“Polisi wamelazimika kutumia mabomu ya machozi baada yao (machinga) kuanza kurusha mawe kuwaponda mgambo wa jiji na Polisi waliokuwepo eneo hilo na sisi kurejesha amani lazima tuwatawanye,” amesema Msangi.

error: Content is protected !!