WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema jumla ya watu 12 wamekamatwa na kuwekwa mahabusu kwa kuvujisha mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022 kwenye Shule ya Sekondari Twibhoke iliyopo mkoani Mara. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Hatua hiyo imekuja baada ya wanafunzi 66 wa shule hiyo kati ya 67 waliofanya mtihani huo kuandika majibu yaliyofanana kwenye mtihani huo jambo lililolazimu Baraza la Mtihani nchini (NECTA) kufuta matokeo hayo isipokuwa kwa mwanafunzi huyo mmoja ambaye majibu yake hayakufanana na wenzie 66.
Prof Mkenda ametoa kauli hiyo leo tarehe 9 Februari 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu muongozo wa Mbunge wa Bunda, Bonipace Getere aliyetaka kujua sababu za kufuta mitihani hiyo ilihali wasimamizi wa mitihani walijaza ripoti kuwa imefanyika vizuri.
Prof. Mkenda amesema katika suala la mtihani kwa ujumla ni vizuri kwani udanganyifu wake una madhara makubwa kwa mfumo wa elimu, uchumi na maisha ya watu kwa ujumla.
“Hili suala la shule ya Mara, kilichotokea kuna sababu za kutosha kwamba kulikuwa na udanganyifu katika mitihani. Kulikuwa na majibu ya mfanano ambao kitakwimu haiwezekani kutokea bila kuwa na uwezo binafsi, tumeangalia na sisi wizara na kujiridhisha kilichotokea,” amesema.
Amesema watu hao 12 wapo mahabusu na chunguzi unaendelea kujua nini kilitokea hadi wanafunzi wakawa na majibu yaliyofanana kiasi hicho.
https://www.youtube.com/watch?v=y4MNWEw6bAk
Pia amesema tayari barua zimeandikwa kwa mamlaka ya waajiri ya wale waliosimamia mitihani kwenye shule hiyo ili wachukuliwe hatua.
“Pia kuna shule moja ambayo ilifungua mtihani kabla ya muda wakawaweka wanafunzi kwenye bwalo la chakula na kuwafundisha namna ya kujibu mtihani, wanafunzi wakaingia kwenda kuufanya… matokeo yao yamefutwa na tunafikiria kwenda kuifutilia mbali hii shule,” amesema.
Aidha, ameomba wabunge wote kusimame kidete kwenye suala hili la udanganyifu wa mitihani kwani ni muhimu kusimamia Baraza la Mitihani kwa uweledi.
Ameongeza kuwa wazazi iwapo wanahisi kuna uonevu, wizara ipo tayari kukutana na wazazi hao kuwaonesha kilichotokea kwa watoto waliokuwa wanasoma shuleni hapo.
Naye Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson amesema udanganyifu hauna namna ya kuutetea na wao kama viongozi lazima waupinge kwa nguvu zote ili nchi yetu ikue kielimu.
“Tunachosisitiza kwa serikali ni kufanya uchunguzi na kuchukua hatua katika mnyororo mzima kwa wanaohusika katika udanganyifu. Kwa sababu mwisho wa siku ndio wanakuja kuchukua nafasi zote tulizonazo hivyo lazima watu wawe wenye uadilifu wasiojifunzi udanganyifu kwenye ngazi ile,” amesema.
Leave a comment