January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

115 waliofariki kwa mlipuko wa tenki la mafuta wazikwa

Spread the love

 

Watu 115 waliofariki katika mlipuko wa tenki la mafuta wiki iliyopita tarehe 5 Novemba, 2021 nchini Sierra Leone, wanazikwa kwa pamoja katika mji mkuu wa nchi hiyo – Freetown.

Mlipuko huo ulitokea baada ya lori la mafuta lenye urefu wa futi 40 kugongana na gari jingine kwenye makutano yenye shughuli nyingi jijini humo.

Picha za video zilizorushwa na vyombo vya habari vya ndani zilionesha miili iliyoungua vibaya.

Akizungumza na Shirika la Habari la Reuters, Waziri wa Afya nchini humo, Amara Jambai ametoa wito kwa watu kujitolea damu haraka ili kuwatibu wahanga walioungua na moto ambao ni zaidi ya 100 wamelazwa hospitalini.

Maofisa wanasema wasambazaji wa damu wanaweza kuishiwa ndani ya saa 72.

Aidha, waziri huyo amesema mazishi hayo yamefanyika leo tarehe 9 Novemba, 2021 katika eneo ambalo watu wapatao 1000 walizikwa mwaka 2017 baada ya kupoteza maisha kutokana na mmomonyoko wa udongo.

Rais wa nchi hiyo, Julius Maada Bio ametangaza siku tatu za maombolezo kitaifa na bendera kupeperushwa nusu mlingoti kufuatia janga lililotokea Ijumaa.

Mlipuko huo unaaminika ulitokea kwenye makutano nje ya Duka Kuu la Choitram lililo na shughuli nyingi katika eneo la Wellington mjini.

Ripoti moja ilisema basi lililojaa watu liliteketea kabisa, huku maduka ya karibu na maduka ya soko yalishika moto huo wakati mafuta yalipomwagika barabarani.

Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga la Sierre Leone, Brima Bureh Sesay aliviambia vyombo vya habari kuwa wengi waliofariki dunia walikuwa wamejitokeza kwenda kuchota mafuta, ikiwamo madereva bodaboda na teksi.

Aliongeza wengine walifariki wakiwa ndani ya magari yao kwani baada ya ajali hiyo kutokea, kulitokea foleni kubwa ya magari hali ilioyosababisha msongamano mkubwa wa watu na magari.

Mji huo wa bandari, ambao ni makazi ya watu zaidi ya milioni moja, umekabiliwa na majanga kadhaa makubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Mwezi Machi mwaka huu, zaidi ya watu 80 walijeruhiwa baada ya moto mkubwa katika mojawapo ya vitongoji duni vya jiji hilo na kusababisha zaidi ya watu 5,000 kuyahama makazi yao.

Na mwaka 2017 zaidi ya watu 1,000 walipoteza maisha baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha maporomoko ya matope yaliyokumba jiji hilo, na kuwaacha karibu watu 3,000 bila makazi.

error: Content is protected !!