August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

11 watumbuliwa Halmashauri Kondoa

Spread the love

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Vijijini limewatumbua watumishi 11 kwa madai ya kuisababisha hasara ya Sh. 320 milioni halmashauri hiyo, anaandika Dany Tibason.

Alhaji Omary Kariati, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kondoa amesema, Baraza la Madiwani limebaini kuwepo kwa upotevu wa fedha hizo.

Amesema, yapo makundi mawili ya watumishi na kila kundi limeisababishia halmashauri hiyo hasara hivyo kurudisha nyuma maendeleo.

Na kwamba, kundi la kwanza la waliotumbuliwa ni watumishi wanane wa idara ya fedha ambao kwa pamoja imebainika kwamba, walisaini matumizi ya fedha bila viambatanisho.

Amesema, watumishi hao wameisababishia hasara ya Sh. 180 milioni halmashauri hiyo na kwamba, Baraza la Madiwani haliwezi kufumbia macho.

Katika hatua nyingine amesema, kundi la pili ni la watumishi watatu ambao wapo katika idara ya ardhi na kuwa, kwa pamoja wamesababisha hasara ya Sh. 140 milioni.

Amesema, watumishi hao waligawa viwanja hewa kwa wananchi na kuwatoza fedha lakini fedha hizo hazikuingizwa katika halmashauri.

“Hawa watumishi wa idara ya ardhi walifanya zaoezi la upimaji na ugawaji wa viwanja hewa, lakini cha kushangaza ni kwamba watu ambao waliuziwa viwanja wana risiti za manunuzi wakati halmashauri haijapokea pesa hizo.

“Jambo lingine ambalo limefanywa na watumishi hao wa idara ya ardhi ni kuuza viwanja mara  mbili yaani kiwanja kimoja wanauziwa watu zaidi ya wawili,” ameeleza Alhaji Kariati.

Waliotumbuliwa ni Emmanuel Chindiol, Ally Mruma, Sekwao, Juliana  Jerengi, Dertha Augustine, Emmanuel Mvungi  na Isdory Mwalongo , aliyekua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa.

Wengine waliotajwa kwa nina moja ni Nambwanga, Kweyunga na Mvungi ambao ni watumishi wa idara ya ardhi.

 

error: Content is protected !!