Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zitto rasmi UKAWA bungeni
Habari za SiasaTangulizi

Zitto rasmi UKAWA bungeni

Spread the love

MBUNGE wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) na kiongozi mkuu wa chama hicho, Zitto Zuberi Kabwe, sasa ameruhusiwa kujiunga rasmi na kambi ya upinzani bungeni. Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Dodoma … (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya kambi hiyo na zilizothibitishwa na Mwenyekiti Mwenza wa Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), James Mbatia zinasema, Zitto ameruhusiwa kujiunga na kambi hiyo baada ya kuomba kufanya hivyo.

Amesema, wabunge wa kambi rasmi ya upinzani bungeni waliokutana mjini Dodoma walipitisha kwa kauli moja, azimio la kumkaribisha na kufanya kazi na Zitto katika umoja wao.

Mwenyekiti huyo wa taifa wa NCCR-Mageuzi na mbunge wa Vunjo mkonia Kilimanjaro alisema, kukubaliwa kwa Zitto kujiunga na kambi hiyo, kunalenga kuongeza umoja wa upinzani bungeni na nguvu ya kukabiliana na serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Zitto ni mbunge mwenzetu. Ni kiongozi wa chama cha upinzani na mmoja wa wabunge mahiri katika Bunge la Tanzania. Tumeona ni vema tukafanya naye kazi pamoja,” ameeleza.

Mbatia amesema, kufuatia uamuzi huo, sasa Zitto atalazimika kufanya kazi zake kwa kufuata kanuni za upinzani, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma ambapo alikuwa anajifanyia anavyotaka.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Zitto aliwasilisha ombi la kujiunga na kambi hiyo kwa barua rasmi ya tarehe 7 Februruari mwaka huu.

Katika barua yake ambayo MwanaHALISI ONLINE imeiona, Zitto alisema, “katka siku za hivi karibuni, kumekuwa na maendeleo makubwa kadhaa katika jitihadaza za kujiimarisha kama upinzani. Ili kujiweka katika hali endelevu zaidi, naomba na mimi kama mbunge wa Kigoma Mjini, niingizwe rasmi katika kambi.”

Naye David Silinde, Katibu Mwenza wa wabunge wa upinzani amesema, wabunge walipokea barua ya Zitto na wakapitisha kwa kauli moja azimio la kumuingiza kwenye kambi yao na kwamba kujiunga kwa Zitto kwenye kambi kutawaimairisha zaidi.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa wabunge wa CUF, Suleman Bungala (maarufu kama Bwege), amesema “kukubaliwa kwa Zitto kujiunga na kufanya kazi pamoja na wabunge wenzake wa upinzani bungeni,” ni uthibitisho tosha kuwa wao kama UKAWA wako kwa ajili ya “maslahi ya taifa.”

Kabla ya Zitto kujiunga rasmi na kambi ya upinzani bungeni, kambi hiyo ilikuwa inaundwa na wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokarasia na Maendeleo (Chadema) na NCCR- Mageuzi.

Vuguguvugu la kumuingiza Zitto kwenye kambi hiyo, lilianzia kwenye mkutano wa vyama 10 vilivyokutana mjini Dodoma wakati wa mchakato wa kupitia Sheria ya Vyama vya Siasa.

Alikuwa ni katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad aliyeomba wabunge kushirikiana na Zitto katika kazi zao bungeni kwa maelezo kuwa katika hali tuliyonayo sasa, “kila mtu anamhitaji mwenzake.”

Maalim Seif aliwaasa wabunge kushirikiana, kupendana na kuaminiana kwa maelezo kuwa mgawanyiko wowote utakaotokea, utarudisha nyuma jitihada zao za kukabiliana na utawala wa Rais John Magufuli ambao wamekuwa wakiutuhumu kuvuruga demokrasia nchini.

Aidha, kujiunga kwa Zitto kwenye kambi, ni utekelezaji wa Azimio la Zanzibar, lililotaka vyama vilivyoshiriki “tafakuri ya pamoja” kushikiriana. Mkutano wa Zanzibar uliofanya tafakuri ya hali ya kisiasa nchini na jinsi ya kupambana na vikwazo vilivyopo, uliitishwa na kusimamiwa na Maalim Seif.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwakyembe : Zanzibar waliongoza kutaka Serikali 2 za muungano

Spread the love  MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema mjadala wa...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

error: Content is protected !!