JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam nchini Tanzania, limemkamata Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akiwa Kituo cha Polisi Osterbay jijini humo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Zitto amekamatwa leo mchana Jumanne tarehe 3 Novemba 2020 akiwa kituoni hapo alipokwenda kuwajulia hali, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wenzake wanaoshikiliwa kituoni hapo.
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, Janeth Rithe amesema, “ni kweli Zitto amekamatwa na polisi akiwa kituo cha polisi cha Oysterbay alikokwenda kuwaona viongozi wa Chadema.”
Soma zaidi:-
Zitto aliyekuwa mgombea ubunge wa Kigoma Mjini amekamatwa saa chache kupita tangu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kutangaza kumtafuta Zitto na Halima Mdee, aliyekuwa mgombea ubunge Kawe, Dar es Salaam kupitia Chadema.
Kamanda Mambosasa aliwataka wawili hao kujisalimisha polisi kwa mahojiano dhidi ya tuhuma zinazowakabili.
Kukamatwa kwa Zitto kumebakisha Mdee, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha).
Leave a comment