February 27, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Z’bar na taswira ya kifo cha Mzee Bindu

Zanzibar

Spread the love

MZEE Ameir Ameir bin Soud, Mzanzibari kindakindaki, mjuzi mkubwa wa historia ya Zanzibar inayohusisha nyanja ya siasa, utamaduni, kilimo na ustawi wa jamii za Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi – kuanzia Afrika Mashariki mpaka Ghuba ya Uajemi – hatunaye tena. Ameaga dunia. Anaandika Jabir Idrissa….Zanzibar (endelea).

Msomi huyu wa dini ya Kiislam na mpiganiaji makini wa Zanzibar yenye mamlaka yake kamili, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 72, kwa mujibu wa kauli aliyoitoa kwangu siku sita hivi kabla ya kifo chake.

Akijuulikana kwa umaarufu kwa jina la Mzee Bindu, alikutwa na mauti akiwa kitandani Hospitali ya Al Rahma iliyopo mtaa wa Kilimani, mjini Zanzibar. Hapo alikuwa amelazwa ili kupatiwa matibabu baada ya afya yake kuzorota ghafla.

Kadhia hii iliyomfikisha hospitalini na hatimaye kwenye mauti yake, ilimkuta mara tu alipotoka mikononi mwa watesi wake ambao walimchukua nyumbani kwake kijiji cha Bwejuu, mashariki mwa Pwani ya Kisiwa cha Unguja.

Alichukuliwa tarehe 26 Oktoba, siku mbili kabla ya siku ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar na Tanzania uliofanyika 28 Oktoba 2020.

Watu waliokuwa wameficha nyuso zao kwa soksi pana, huku wakiwa na silaha ikiwemo vile nondo na marungu yaliyovishwa misumari, walifika nyumbani kwake saa 6 usiku na kumuita kwa sauti.

Akiwa ameanza kupatwa na usingizi wakati huo, ananisimulia tukiwa ndani ya vipenu vya hospitali alikolazwa, alishtuka. Akaamka na kusikiliza sauti ya kuitwa. Aliporidhika kuwa akiitwa yeye kwa jina lake, aliinuka na kukaa kitako. “Niliuliza wewe unayeniita ni nani mwenzangu,.” Jibu likawa “tunakutaka utoke nje, huku ndo utajua sisi ni nani.”

Akauliza tena, “Ni sawa lakini nambieni basi mnataka nini kwangu usiku huu… na kwanini msije asubuhi kama mnanifuata kwa jambo la kheri.” Jibu likawa “usituulize hayo, tunataka utoke sasa hivi ndo utaona na kutujua sie ni nani.”

Mzee Bindu anasema alichungulia na kuridhika kuwa amefuatwa na “wanaume wa kazi.”

Mzee Bindu anasema alijua amekutwa. Kwamba ni zamu yake sasa, baada ya kuwa akisikia tu watu wa aina hiyo wanafuata wananchi majumbani mwao na kuwaamrisha kutoka nje. “Nilijisemea ‘siku zangu zinahisabika. Hawa watanihujumu tu mnyonge wa Muungu mie; sina shaka yoyote kwa hili,” anasema.

Alivuta seruni na kujifunga kiunoni. Akachukua fulana ya ndani na kuiweka begani. Akaamua kutoka kwa mlango wa nyuma, akijua ni dhaifu usohitaji nguvu kuufungua. Aliusukuma kidogo tu ukaachia. Alipochomoza kichwa ili kuangalia nafasi ya kujinusuru, alishtuka kukuta wale mazombi kumbe wameizunguka nyumba.

“Mmoja nilimkuta hatua mbili tu kutoka mlangoni. Aliponiona nataka kutoka, akanisogelea. Huku nikiwa nimeushika mlango akanifuata karibu. Ghafla nikaona anainua mkono wake ulioshika silaha na kuisukuma akinielekezea usoni kwangu.

“Ni bahati tu nilijikuta nausukuma ule mlango na ndio hasa ulioniwezesha kukwepa kupigwa tako cheke. Ni hapo nikajua wala si mchezo, maisha yangu yapo hatarini,” ananisimulia.

Mzee Bindu ambaye amekuwa na ujasiri wa kurikodi maelezo anayoyaita ni ya nasaha kwa jamii wakiwemo viongozi wake, ya kuyarusha mitandaoni, anasema baada ya hapo alijisalimisha na kukamatwa na watu hao.

“Nilipata uhakika kuwa wale vijana si pima yangu. Wao ni vijana tena wamebeba silaha, sifanani nao hata kidogo; nikawa tai (mtulivu) kwao,” anasema.

Haikuchukua muda akajikuta amedhibitiwa vilivyo. Akatupwa ndani ya gari. Hapo tayari seruni yake imemvuka na fulana imemuanguka. Wale watu walimfunga kitambaa cheusi usoni huku gari ikiwa imeanza mwendo. Alijua inaelekea kusini mwa kijiji muelekeo wa Paje, kijiji jirani na Bwejuu. Baadaye alibaini gari imenyoosha njia ya mjini.

“Nilitambua tumepita Kitogani na kuelekea mjini. Mote humu wale watu wananipiga kama mtoto mdogo wa chuoni. Kipigo si kidogo huku wakinisemeza maneno ya ovyo sana,” anasimulia.

Mzee Bindu alipatwa na machungu makubwa ya kupigwa, kipigo kilichomrudisha kukumbuka yaliyopita wakati wa miaka ya baada ya mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964. Anayakumbuka mateso ya nyumbani kwa Mandera ingawa hakueleza kama yeye binafsi aliwahi kushikwa na kuteswa wakati huo.

Nyumba ya Mandera ilikuwa eneo la Maisara mjini Zanzibar ambako wananchi mbalimbali hasa vijana na wasomi, walipelekwa na kuteswa baada ya kukamatwa kwa sababu za kisiasa kwa kuonekana walipinga mapinduzi au walikuwa wafuasi wa kilichokuwa chama cha Hizbu – kikiitwa Zanzibar Nationalist Party (ZNP).

Mzee Bindu anasema, kipigo kiliendelea mpaka alipotakiwa kushuka kwenye gari. Hakuwa na nguvu. Kwa hakika alikuwa ameshachoka na akijisikia maumivu makali.

“Niliposhuka tu nikadakwa na vijana wale na hapo nikaendelea kupigwa tena. Nilibaini baadaye kuwa nilizimia na kuanguka.Wale walionichukua nyumbani walinikabidhi kwa wenzao kule nilikoshushwa.

“Nikajikuta nimefunguliwa kitambaa sasa. Napumua kama mtu niliyetoka mazoezi lakini nina maumivu makali. Mwili unauma kila mahali na mivilio ya damu kutokana na kipigo imenijaa mikononi mpaka miguuni,” anasema.

Akiwa ndani na kubaini asubuhi changa imeingia, aliulizwa na watu waliosimama mbele yake “unajua upo wapi hapa?” na akajibu haraka “hapana. Sijui.”

Sawa hujui ni wapi hapa; lakini unaweza kubaini jiografia ya hapa ulipo, aliulizwa tena, “ninaona jua linaanza kuchomoza. Ninaona upande ambako jua linatokea ndiko kwenye mgongo wangu kwa vile nilivokaa,” anajisemea huku akitafuta jibu.

“Hawa watoto ni vema niwaoneshe mie nina akili zangu nzuri ili wajue si mtoto mwenzao,” anawaza. Nikawaambia, “huku mgongoni kwangu ni urejua ambako ndiko jua linachomozea, huku kulia kwangu itakuwa ni alkaaba huku. Na mbele yangu basi itakuwa ni uchewejua ambako jua linazamia huku. Na kushotoni kwangu itakuwa kusini,” anasema akiwajibu wale “wanaume wa kazi” wanaompima akili. Aliulizwa alkaaba ndio wapi? Ni kaskazini kuliko na kibla ambako ni upande wa mahsusi wa kusimamia ibada ya sala kwa Waislam kote duniani.

“Ahaa, sawasawa Mzee Bindu kumbe una akili sana,” alisikia mmoja akisema. Hapa tupo Hanyegwa Mchana. Umeletwa hapa ili tukutie adabu… tunatekeleza tulichoambiwa na waliotuleta hapa.

Nilimuuliza Mzee Bindu, “sasa unanisimulia yaliyokukuta kule ndani. Huogopi kurudishwa tena wakati umenambia walikuonya kuwa ukirudi kule hutorudi tena nyumbani.” Alijibu “sina cha kuogopa katika umri nilionao na nadhani hawatonichukua tena. Hawatonipata tena.”

Mzee Bindu aliachiwa tarehe 13 Novemba, siku ya Ijumaa ambayo baadhi ya watu waliokuwa wamekamatwa miongoni. Kifo chake kilikuja siku 12 tangu alipoachiwa.

Alinieleza “walinieleza wazi kuwa kule kwangu wanatafuta vitu viwili. Kwanza wanataka kuona simu yangu. Wanataka kujua kama nina mawasiliano ya karibu na viongozi wa kisiasa na kunitajia baadhi yao.

“Na wanatafuta taarifa kuwa mimi ni mwanajeshi na nina utaalamu wa kutengeneza na kufyatua mabomu. Niliumia sana kwamba wataiona simu yangu maana sikuificha. Ilikuwa kwenye chaji wakati nilipokuwa nalala. Niliogopa sana kwa sababu walisema wakithibitisha wanachokitafuta watani***,” anasimulia.

Anasema kwa sababu “nampenda sana” Mwenyeezi Mungu, nilimuelekea na kumuomba anivue kwa hili kama alivyowanusuru mitume wake akina Yusuf na Nuhu, walipokumbwa na matatizo.” Ikatokea hawakukuta chochote walichokitafuta nyumbani kwa Mzee Bindu.

Mzee Bindu hakuwahi kupata mafunzo ya kijeshi popote pale maishani mwake. Wala hakuwahi kuingia kwenye kambi ya jeshi la aina yoyote na popote pale Tanzania. “Lakini wale vijana waliniambia kuwa, taarifa walizopewa si lazima waziamini ila lazima wazifanyie kazi.”

Anahadithia “walinipiga sana (mara nyingi) kwa kutumia pande la nondo. Wameniumiza sana hapa.” Alionesha sehemu mbalimbali za mwili ambamo mna makovu ya kupigwa mapanga na pale alipoumizwa.

Jumapili, siku mbili baada ya kuachiwa, Mzee Bindu alipelekwa Hospitali ya Al Rahma kuangaliwa afya yake. Alifanyiwa uangalizi wa kifaa cha mionzi (X-Ray) na kukutwa hakuvunjika isipokuwa mguu umetisika sana.

Lakini huku akiwa anaendelea kutumia dawa za kumpunguzia maumivu, alilazimika kurudishwa siku tatu baadaye, hali yake ikiwa imebadilika. Alionesha kukosa nguvu ya mwili kiasi cha kusimama kwa shida.

Daktari aliyemkagua, alibaini Mzee Bindu amepatwa na maambukizi kutokana na kipigo alichokipata. Alipatiwa matibabu yakiwemo ya sindano tano, akianzia na mbili palepale; moja kwenye kalio na nyengine ya mkononi.

Daktari alielekeza sindano nne achomwe mkononi kwa siku nne zilizofuatia. Tiba hii iliendelea lakini ilipofika Ijumaa jioni, hali yake ilibadilika tena huku mwili wake ukiongezeka joto. Sasa alishindwa kutembea.

Daktari aliyekuwa akimchoma sindano nyumbani, aliahidi atafika kumpima kiwango cha sukari asubuhi Jumamosi. Uchunguzi huu ulithibitisha sukari imepanda kuliko kiwango cha kawaida.

Siku ya Jumapili ililazimika kumrudisha hospitali.  Akafanyiwa uchunguzi wa vipimo mbalimbali ikiwemo mapigo ya damu (BP), kiwango cha damu mwilini na sukari.

Daktari aliyemshughulikia, aliamua kumlaza ili apate matibabu chini  ya uangalizi hospitalini. Kiwango cha sukari kilikuwa kikishuka kidogo asubuhi lakini kikipanda sana mchana.

Jumatatu madaktari waliamua kumpeleka Mzee Bindu chumba cha upasuaji – Theatre. Wakati huu mguu wake ulioumizwa kwa kipigo ukiwa umefanya jeraha kubwa baada ya ngozi yake kuganduka lakini ngozi mpya ikiwa imeathirika.

Kwa kuwa tayari amegundulika tatizo la sukari kupanda, ambalo hakuwa nalo hapo kabla, jeraha lilikua haraka ndipo madaktari walipoona anahitaji kuchunguzwa zaidi. Tiba yake ilichukua kiasi cha saa mbili lakini Mzee Bindu alikuwa hajazinduka hata ikiwa imeingia usiku siku ile ya Jumatatu.

Siku kabla yake, alikuwa akitoa simulizi za kuwa karibu sana na kisomo cha Quran. Alikuwa akiomba dua na kutoa maneno ya kukemea dhulma. Alikuwa akiasa wananchi waendelee na jitihada za kuipigania Zanzibar yao.

Hakuweza kutambua watu waliofika kumjulia hali. Hatimaye aliaga dunia adhuhuri ya Jumanne tarehe 24 Novemba na kuzikwa kijijini kwake Jumatano 25 Novemba.

Umma mkubwa ulifika Bwejuu kushiriki maziko ya Mzee Bindu ambaye Wazanzibari watachukua miaka mingi kumsahau kutokana na ukakamavu wake katika kutoa elimu ya dini na dunia.

Katika uhai wake, alikuwa mtoa elimu kwenye nyanja za utamaduni, dini na historia ya Zanzibar kuanzia na tawala za kale mpaka yalipofanyika mapinduzi ya 1964. Mzee Bindu akijulikana kwa ujuzi wa ufugaji wa nyuki na kurinda asali kulikompeleka safari nyingi ndani na nje ya Tanzania.

Alikuwa akitoa mihadhara ya masuala hayo kwenye vyombovya habari na mikusanyiko ya watalii mahotelini hasahasa ukanda wa mashariki mwa kisiwa cha Unguja.

Ndio maana alijijengea jina miongoni mwa watembezi wa mataifa ya Ulaya na Marekani waliokuwa wakimlipa usafiri kutoka nyumbani kwake kwenda kuwaelimisha hotelini.

“Wakimrudisha usiku mkubwa nyumbani kwake. Watalii wamepata hasara kubwa kumkosa gwiji huyu wa historia ya Zanzibar,” anasema Ali Dawa, mmoja wa watu wa karibu kiharakati waliokuwa na marehemu. Anastahili kuombewa msamaha kwa Mola muumba, na katika haya aliyotendewa, wa kushtakiwa ni Muumba pekee.

error: Content is protected !!