Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Z’bar itarejea asili yake?
Makala & Uchambuzi

Z’bar itarejea asili yake?

Spread the love

HIVI ninavyojadili haja ya kuiona Zanzibar inarudia asili yake ya kuwa nchi yenye wastaarabu na iliyopiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi, kunatokea tukio baya kisiasa linaloakisi hasa kile ninachoshikilia kukiamini kuwa ni kasoro kubwa. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Kwamba nchi hii inayoundwa na visiwa vikuu viwili vya Unguja na Pemba na vingine kadhaa vidogo ambavyo pia vinaishi watu, inakosa uongozi mwema.

Kwa muda mrefu kumekosekana aina ya uongozi inayohitaji watu makini kifkra na wachamungu kwelikweli. Watu wanaoipenda nchi yao moyoni, wakaonesha hasa uzalendo juu yake, na tena wakajali haki na heshima za wale wanaowaongoza.

Kwamba kwa muda mrefu viongozi wanaoshika hatamu za utawala visiwani Zanzibar wamethibitika kwa kasoro za uongo, wasio na huruma, wabaguzi na wapenda ubinafsi.

Kwa kuwa hawapendi ukweli kusemwa na wanachukia kuona na kuipa haki nafasi yake, viongozi hawa wamezima ndoto za kisiasa -angalau kwa sasa – za mmoja wa wanasiasa vijana katika chama chao – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Abdalla Maulid Diwani si mwakilishi tena wa jimbo la uchaguzi la Jang’ombe, ndani ya Mji wa Zanzibar. Tayari kiti cha jimbo hilo kimetangazwa katika Baraza la Wawakilishi kuwa kipo wazi.

Sababu ya hali hiyo si kwamba mwakilishi huyo amepoteza maisha; wala si kwamba ameamua mwenyewe kujiuzulu kama alivyofanya Salim Msabaha Mbarouk mwaka 1997.

Msabaha aliyekuwa na elimu kubwa ya Dini ya Kiislam, alikuwa mwakilishi wa Jimbo la Mkunazini, pia mjini Zanzibar. Naye pia alikuwa mwanasiasa kijana bali akiwakilisha Chama cha Wananchi (CUF).

Alipotangaza kuwa amejiuzulu, alisababisha mshtuko mkubwa kwani ilikuwa ni baada ya muda mfupi kuzoa kura nyingi za wananchi katika uchaguzi wa kwanza ulioshirikisha vyama vingi baada ya mfumo huo kurudishwa.

Uamuzi wake ulishangaza pia kwa sababu haukutanguliwa na mgogoro wowote ndani ya chama chake na jimboni ilikuwa furaha tupu maana aliungwa mkono na vijana.

Lakini Msabaha alifisidiwa kisiasa kama alivyofanyiwa Diwani ambaye anawaambia watu wa karibu naye kwamba hakujutia “adhabu kali” aliyopewa.

Saa kadhaa kabla, alikuwa ameonesha ujasiri wa kisiasa na kiimani; na moyo mkubwa wa kujiamini na kujitoa kwa ajili ya kuiamini haki na kuishuhudisha.

Diwani ameonesha anapenda haki. Anaamini katika ukweli na isitoshe, anajitambua na kutambua wajibu wake kama kijana katika nchi huru bali iliyoganda kimaendeleo.

Anaijua vema nchi yake; anaijua historia yake, anajua masahibu mbalimbali ambayo yameikumba katika maisha yake na pia anajua mahitaji halisi inayoyadai kwa sasa.

Kwa kuwa anaitakia mustakbali mwema Zanzibar, Diwani alitaka wenzake katika CCM ile watulize akili zao na kutambua kuwa hiyo njia wanayopita katika kuendesha siasa, imejaa miba na haiwafalii tena.

Anawaelekeza kuamini katika kubadilika. Wafumbue macho yao, wazibue masikio yao na wajenge utamaduni mpya wa kuishi ndani ukweli na haki. Yapasa waache jeuri na kiburi mbele ya Mola muumba wao.

Wajue maisha ya kutamalaki kuchuma dhulma hayana maana na yatawaumiza tu. Wauone ukweli na kuukubali kwa sababu ingawa wamekawia, hawajachelewa kwa kuwa watahesabiwa tu kwa uamuzi wao wa kutubu uovu.

Watawala wa CCM warudi kwenye ukweli na uadilifu. Hawana chaguo isipokuwa kuchagua kweli na kuishi nayo. Hawatapoteza kitu bali zaidi waamini kuwa watalipwa fadhila stahiki maana huo ndio uchamungu wa kweli.

Diwani baada ya kubaini kuwa hapendezi kwa wakubwa zake kisiasa kwa sababu anaiamini na kuipenda hasa haki na kuichukia batili, aliamua kutafuna jongoo kwa meno.

Aliamua kujitoa na kujitolea. Akae mbele ili ahesabiwe kwa haki maana amechoka kuvumilia kutoeleza kitu anachokiamini. Hakutaka kuwa mnafiki kama baadhi ya vijana wenzake ndani ya CCM. Hakuchagua kuwa bendera, mfataji upepo.

Kwa sababu yu makini, muungwana na mwerevu, anajua Zanzibar inastahili kuwa ya Wazanzibari wote bila ya kumbagua yeyote yule awaye. Anajua ubaguzi si maendeleo, bali ni dhulma na dhambi.

Anajua ubaguzi wowote ule hauna kheri. Haujengi bali sanasana unachimba chuki katika jamii na ukiendelea kuachiwa kuwa ada ya kila siku, huichanachana jamii.

Diwani anaipenda Zanzibar kwa sababu ndio baba na mama yake. Anaipenda kweli hawezi kuishi akivumilia kuona inaumizwa. Ataishi wapi yeye iwapo hatoilinda?

Akavunja ukimya wa kinafiki – akasema “… hapana. siwezi na haiwezekani twende namna hii… ni muhimu na tutaonesha uzalendo tukikubali haki.”

Hayo ni maneno yangu. Lakini ndio maudhui ya maelezo ya Diwani mbele ya wakubwa zake ndani ya Baraza la Wawakilishi rasmi na akiwa baraza la nje ya Baraza la Wawakilishi.

Anasema Zanzibar inastahili kuendeshwa kiadilifu na kwa hivo kila Mzanzibari ana haki ya kupewa nafasi ya kutoa mchango katika kuiona nchi inakwenda vizuri na inawanufaisha watu wote si wachache.

Diwani anaamini Zanzibar si mali ya chama cha siasa chochote. Si kile kilichomtoa wala kinginecho chochote. Zanzibar ni ya watu wote wa Unguja na Pemba, waliomo ndani ya visiwa, katika jamhuri na wale walioko nje ya jamhuri.

Sasa haiwezekani watu wachache ndio wapate haki huku gharama ya uovu huo ikiachiwa kuwadhoofisha wananchi wengi wasio na hatia yoyote. Na wala huko si kudumisha fikra za mapinduzi.

Diwani anajua mapinduzi yalikuwa na maana ya kuiacha Zanzibar nchi huru kwa namna zote. Sio huru hivi bali vile yabanwabanwa.

Basi ni muhimu haki iwe ni haki kweli. Na penye haki ni vema iachwe kuishi.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!