Wednesday , 24 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Zanzibar ‘mkao wa kula’
Makala & UchambuziTangulizi

Zanzibar ‘mkao wa kula’

Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar (kushoto) walipokuwa katika mazungumzo ya muafaka na Maalim Seif Shariff Hamad
Spread the love

Kalamu ya Jabir Idrissa

SIASA visiwani Zanzibar ni ada kimaisha. Siasa ni kila kitu kwa wananchi. Na kila kitu ni siasa Zanzibar. Kila kile kinachoongelewa au kujadiliwa, kwa Zanzibar ni siasa. Kinahusianishwa na kuwa na mantiki yake kisiasa.

Basi ni sahihi mtu kusema siasa ni maisha ya kila siku kwa wananchi wa Zanzibar, nchi ya visiwa vikuu vya Unguja na Pemba, na vingine kadhaa vidogo – vinavyoishi watu kama Kisiwapanza, Kojani na Fundo (Pemba) na Uzi, Michamvi na Tumbatu kwa Unguja na visivyoishi watu bali ni vivutio na hazina kwa utalii.

Hata hivi unaposhuhudia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikijinasibu kwa kufikisha miaka miwili na nusu (miezi 18) ya kushika hatamu za uongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein, tangu wafanikiwe kuhujumu haki ya wananchi kupitia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015, usije ukaamini kuwa hakuna siasa Zanzibar.

Utakuwa unajidanganya pakubwa. Hutakuwa unajitendea haki hata kidogo. Hutakuwa unayajua na kuyafatilia maisha ya siasa ya Wazanzibari. Hujuma ilitendwa na hatimaye CCM kujirudisha madarakani, lakini bado wananchi walioithibitisha haki kwa kutia kura zao kwa Chama cha Wananchi (CUF), na mgombea wake wa urais, Maalim Seif Shariff Hamad, wanaamini haki yao itarudi mikononi mwao.

Matumaini ya Wazanzibari kwamba haki yao ya kuongozwa na kiongozi huyo waliyemchagua kihaki lillahi katika uchaguzi uliokuwa na utulivu mkubwa kabla ya kuvurugwa kwa tangazo la Jecha Salim Jecha, kwa nafasi yake ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), yanachagizwa na kauli za viongozi wao mbalimbali.

Tena usije ukadhani ni kauli za zamani. Hapana. Kauli za hivi karibuni. Ni kauli zilizotoka juzi tu baada ya kuwa Rais Dk. John Magufuli ameshafanya dhihaka ya kisiasa jukwaani Uwanja wa Amaan, mjini Zanzibar, mbele ya hadhara ya wananchi wakiwemo vijana na watoto waliokuwa wakisikiliza hutuba ya maadhimisho ya kilele cha mbio za mwenge wa uhuru.

Ilikuwa ni tarehe 14 Oktoba 2017, Rais Magufuli alichepusha hutuba iliyokuwa ikizungumzia mwenge wa uhuru na kusema, “nasikia wapo wengine wanajiandaa kuapishwa… sijui wameishia wapi.” Hakuongeza neno baada ya hayo. Na kila anayejua na kuyafatilia maisha ya kisiasa ya Zanzibar, alijua kule ambako Rais Magufuli alilenga. Yanajulikana kwa upana masuala haya.

Wazanzibari wanajua Maalim Seif anashughulikia kurudishwa kwa haki ya wananchi kuongozwa na kiongozi wampendaye. Aliwaahidi kuwa atashughulika kuirudisha haki hiyo na atarudi kwao kuwajulisha pale itakapokuwa ameridhika ameshindwa kuipata haki hiyo. Hajarudi kuwajulisha. Wanatumainia ataipata tu.

Basi kupitia kwa wasaidizi wake katika chama, Maalim Seif anaendelea kushikilia kuwa ahadi yake hiyo ingali maridadi. Kwamba hajakata tamaa na jitihada zinazofanyika zinaendelea kumpa matumaini kuwa zitafikia hatua ya haki ya wananchi kurudishwa mikononi mwao.

Wasaidizi wake wawili hivi karibuni walijitokeza mbele ya hadhara ya wanachama wa CUF walio wajumbe wa mikutano mikuu ya wilaya mbili ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alianza Hamad Masoud Hamad, Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa (BKUT), na Mwakilishi wa wananchi wa jimbo la Ole, kisiwani Pemba, ambaye alichaguliwa katika uchaguzi halali wa 25 Oktoba 2015. Alikabidhiwa cheti cha ushindi ambacho angali nacho mpaka leo.

Hamad aliyewahi kuwa mmoja wa mawaziri waliotumika katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya mfumo wa umoja wa kitaifa – Novemba 2010-Oktoba 2015 – kabla ya kujiuzulu katika ile dhana ya kuwajibika baada ya kutokea ajali ya meli mkondo wa Nungwi, alialikwa kuwa mgeni rasmi kwenye Mkutano Mkuu wa CUF Wilaya ya Magharibi B.

Alipopewa nafasi ya kutoa nasaha zake za ufunguzi rasmi wa mkutano huo kwenye ukumbi wa Majid, Kiembesamaki, mjini Zanzibar, Hamad alisema Maalim Seif atafikia kuongoza Zanzibar muda si mrefu ujao. Alisema hatua za kufikia hapo ziko nchani kukamilika na hata siku hiyo alikuwa kwenye sehemu ya harakati hizo ndio maana akakosa kuhudhuria.

Awali ilitarajiwa kwamba Maalim Seif ndiye angekuwa mgeni rasmi wa mkutano huo. Hata hivyo, ikatolewa dharura ghafla kwamba ameipata na kuwa badala yake atawakilishwa na Hamad Masoud Hamad.

Alianza hutuba yake kwa kusema kwamba jambo likishakuwa ni jukumu la Imam kulisema, kiutaratibu wa kidini katika Uislam, hakuna mwengine wa kulisema. Hamad akasema yeye ametumwa kuja kueleza chochote kwa mlahaka huo lakini, “maneno hasa ya suala hili anayo mwenyewe Maalim Seif (imam wetu kwa suala hili).”

Msaidizi mwengine wa Maalim Seif ni Ahmed Nassor Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa Zanzibar. Akihutubia Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Mazrui alisema anajua kwamba haki ya Wazanzibari ingalipo na ipo karibu kurudishwa mikononi mwao.

Mazrui ambaye pia ni mmoja wa mawaziri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), akishughulikia sekta ya biashara, viwanda na uwekezaji, alisema Maalim Seif anaendelea kusema kwamba hana wasiwasi ataiongoza Zanzibar wakati wowote kuanzia sasa.

Akasema Maalim Seif anazidi kuwaambia wale wasioamini wakiwemo wa ndani ya CUF, kuwa wasubiri wasije kushangaa siku ya kufikia hatua hiyo. Mazrui anasema wakati huu chama kinapoendesha mikutano yake ngazi ya wilaya, ni vema viongozi wakautumia kujipanga kuwa na utendaji wa namna mpya wakijua watakuwa wana rais.

Viongozi wa CUF wamekuwa wakisema katika siku za karibuni kuwa wanajiandaa kuwa ni chama kilichoshika dola kwa hivyo ni muhimu viongozi wakabadilika na kutenda kwa ufanisi. Ni kama vile kuwaelekeza viongozi wote na wananchi kuwa “kaeni mkao wa kula.”

Kumeenea habari Zanzibar na katika mitandao ya kijamii inayojumuisha Wazanzibari mpaka walioko ughaibuni (Zanzibari Diaspora) zinazosema kuwa suala la kurudishwa haki ya Wazanzibari kuhusu kiongozi waliyemchagua, linashughulikiwa kwa kasi.

Taarifa za karibuni zimesema tayari jopo la wanasheria wakiwemo wa Zanzibar wakiongozwa na mmoja wa majaji maarufu, limeyahakiki upya matokeo ya urais yaliyompa Maalim Seif ushindi mkubwa wa asilimia 54 dhidi ya Dk. Shein, na kwamba wiki iliyopita walikamilisha kazi hiyo kisiwani Pemba.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo hakuna kiongozi yeyote katika CUF wala upande wa CCM, aliye tayari kuzithibitisha, ripoti maalum ya matokeo ya kura za urais wa Zanzibar kwa uchaguzi wa 25 Oktoba 2015, ilitarajiwa kuandaliwa ili ikabidhiwe kwa kiongozi wa juu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huyo, habari zinasema, ndiye atapaswa kusimamia hatua ya mwisho ya makabidhiano ya serikali kutoka kwa Dk. Shein kwenda kwa Maalim Seif.

Mara baada ya mwenyekiti Jecha kumtangaza Dk. Shein kuwa mshindi wa urais kutumia kilichoitwa “Uchaguzi wa marudio” uliofanywa tarehe 20 Machi 2016, Maalim Seif aliongoza ujumbe wa wasaidizi wake kuzunguka dunia kwa lengo la kuwasilisha malalamiko ya namna CCM inavyohujumu uchaguzi wa kidemokrasia na kujiweka madarakani, kwa kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama.

Katika ziara hiyo ndefu, Maalim Seif alifika Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, na Mahakama ya Uhalifu wa Kivita jijini The Hague, Uholanzi.

Pia alikwenda Uingereza waliko Wazanzibari wengi miongoni mwa nchi za Ulaya, Ubelgiji kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya (EU), Canada na nchi mbalimbali za Ghuba ya Uajemi ambako Zanzibar ina mafungamano makubwa.

Mara kadhaa uvumi wa kuwepo mabadiliko ya uongozi Zanzibar umekanushwa na viongozi wa CCM akiwemo Dk. Shein mwenyewe. Mwaka mmoja uliopita wakati akiwa amefikia mwaka mmoja wa kushika serikali, alisema hakuna mabadiliko kama hayo na kwamba yeye ndiye rais na hataingia mwengine mpaka utakapofanyika uchaguzi mwengine Oktoba 2020.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

error: Content is protected !!