January 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wizara Afya kuzindua mpango mpya wa usafi

Wafanyakazi wakifanya usafi maeneo yao ya kazi

Spread the love

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatarajia kuzindua Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Afya na Usafi wa Mazingira (2021-25). Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).

Mpango huo unaolenga kuimarisha huduma za afya ya usafi wa mazingira ili kukabiliana na milipuko ya magonjwa yatokanayo na usafi duni, ikiwemo kipindupindu, kuhara na kichocho.

Pamoja na mambo mengine, mkakati huo unalenga kutengeneza mfumo wa kuziwezesha wizara na taasisi husika kufanya kazi kwa pamoja katika kuboresha usafi wa afya ya mazingira.

Wizara hizo ni pamoja na Wizara ya Elimu, Maji, Ofisi ya Raisi (Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa), Mamlaka ya Dawa na Vifaa vya Tiba Tanzania (TMDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA).

Mkakati huo unatarajiwa kuzinduliwa na Waziri wa Afya, Dk. Doroth Gwajima Ijumaa tarehe 18 Desemba 2020, Jijini Dodoma  katika kilele cha mkutano wa mwaka wa Afya na Usafi wa Mazingira unaofanyika jijini humo kwa siku nne.

Aidha, katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Prof. Mabula Nchembe ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya amesisitiza kuwa, afya na usafi wa mazingira ni eneo nyeti kwani inahusika na afya ya kisaikolojia, akili na afya ya binadamu.

“Mnakabiliwa na jukumu kubwa na changamoto kwani katika ofisi nyingi, maeneo ya umma, na mashule ndani ya nchi hali ya afya na usafi wa mazingira bado sio nzuri, lazima ninyi wenyewe muoneshe maana ya usafi wa mazingira,” amewaambia maofisa wa afya wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi, Afya ya Mazingira na Usafi wa mazingira katika wizara ya afya, Dk Khalid Massa alisema mkutano huo ni jukwaa la wataalamu kupitia na kujadili juu ya utendaji wa sekta hiyo kwa mwaka uliopita, lakini pia, kutoa mapendekezo yatakayosaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo muhimu

error: Content is protected !!