Rais John Magufuli

Wenye Ulemavu Tanzania wampa heko JPM

Spread the love

Jumuiya ya Wanawake ya Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata) wamempongeza Rais John Pombe Magufuli jinsi alivyotambua mchango wa watu wenye ulemavu katika Serikali aliyoiunda. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Pia, wamempongeza jinsi alivyotambua kundi hilo kwa kuwasaidia mathalani vifaa mbalimbali vya kujifunza na kufundishia kwa shule za msingi na sekondari pamoja na asilimia mbili za wenye ulemavu.

Pongezi hizo zimezitoa leo Jumatano tarehe 17 Juni 2020 na viongozi wa Jumuiya hiyo wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuelezea miaka mitano ya utawala wa Rais Magufuli.

Shivyawata inaundwa na vyama mbalimbali kumi vinatotetea na kusimamia maslahi ya wenye ulemavu.

“Nia yetu na dhamira yetu ya dhati ni kutoa pongezi kwa Rais John Magufuli kwa mambo mbalimbali aliyoyafanya kwa kundi la wanawake wenye ulemavu na watoto na Watanzania kwa ujumla,” amesema Nuru Awadhi, mwenyekiti wa wanawake na watoto wenye ulemavu Tanzania.

“Bila ya kujali rangi, dini wala kabila. Bila kujali itikadi ya vyama na kama anavyosemaga yeye mwenyewe ‘maendeleo hayana itikadi’ na sisi tumeona tutoe shukrani kwa Rais jinsi alivyotutendea kwa jamii ya watu wenye ulemavu na wasio wenye ulemavu,” amesema.

Baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya Wanawake ya Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata)

Nuru amesema, utawala wa awamu ya tano tangu ulipoingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015 chini ya Rais Magufuli, ulisikiliza kilio cha muda mrefu cha wenye ulemavu cha kitengo cha wenye ulemavu kukiondoa wizara ya afya na kipelekwe ofisi ya waziri mkuu.

“Hili limetekelezeka kwa asilimia 100 na Rais Magufuli alifanya hivyo baada tu ya kuingia madarakani. Hakuishia hapo tu, alikwenda mbali zaidi kwa kuteua watu wenye ulemavu mbalimbali kuongoza na cha kushangaza, akateua mwanamke mwenye ulemavu kutuwakilisha kama naibu waziri (Stella Ikupa),” amesema.

Amesema, katika kipindi chake cha uongozi, amenunua vifaa mbalimbali na kuvisambaza katika shule za msingi 213 na za sekondari 22 nchini ili kuwezesha wanafunzi kujifunza kwa ufasaha.

“Katika bajeti ya mwaka 2019/20 imenunua na kusambaza vifaa vya wanafunzi wenye ulemavu vyenye thamani ya zaidi ya Sh1.13 bilioni. Baadhi ya vifaa hivyo ni CCTV karema ambacho kinatumika kukuza maandishi.”

“Amejenga shule maalum mkoani Arusha itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wenye ulemavu  640. Sisi kama wanawake wenye ulemavu, tunaona Rais amefanya vitu vingi,” amesema.

Rais John Magufuli akimwapisha Stella ikupa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia wenye ulemavu(picha na Maktaba).

“Kama wenye ulemavu, watoto wenye ulemavu, tunaona dhamira hii ya kutuondoa na tunaposema elimu jumuishi, wanafunzi watapata elimu na hawatokuja kuwa tegemezi.,” amesema Nuru.

Jambo jingine, Nuru amesema ni la asilimia mbili za wenye ulemavu zinazotengwa na Halashauri zote nchini kwamba, “hizi fedha za mikopo ni mizuri, tutoe wito kwa wanawake na vijana wenye ulemavu kuzichangamkia ili kujikwamua kiuchumi.”

Kuhusu uchaguzi mkuu 2020, Nuru amesema, “tunaomba wadau mbalimbali kumuunga mkono kwa jinsi alivyojitoa na kuwapigania wenye ulemavu. Tunaingia kwenye uchaguzi, tunamwombea amani kwani Rais amefanya mema. Tumuunge mkono Rais.”

“Sisi kura zetu wenye ulemavu, hatupangi foleni na kupitia jumuiya zetu na wenye ulemavu nchi nzima, watajitokeza kwenda kupiga kura. Kura zaidi ya milioni tatu, zipo,” amesema.

Naye Katibu wa Jumuiya ya wenye ulemavu wanaotumia viti mwendo (KASI), Furaha Mbilinyi amemwomba Rais Magufuli, “kama itakupendeza, tunaomba tupate wateule wa ngazi mbalimbali watokane na jumuiya ya wanawake wenye ulemavu.”

Katika hilo, wameomba Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT), “ishirikiane na Jumuiya za wenye ulemavu kupendekeza majina ya viongozi halisi watakaotoka ndani ya jumuiya ya wanawake.”

“Kwa sababu jumuiya yetu ina vyama kumi wenye ulemavu na mgombea atakayetoka ndani ya chama chetu atakuwa na uzoefu wa changamoto walizonazo za walemavu wa aina zote,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Idara ya Wanawake na Watoto Wenye Ulemavu kutoka Chama cha Viziwi Tanzania (Chavita), Lupi Mwaisaka amesema, kitendo cha kumpata mgombea anayetoka ndani ya vyama hivyo, anakuwa anazijua, “haki zote chungu na tamu za wenye ulemavu.”

Pia, amewaomba wenye ulemavu kujitokeza katika uchaguzi mkuu kugombea katika nafasi mbalimbali.

Naye, Blandina Sembu, Katibu Mkuu wa Shivyawata amesema, “tunaunga juhudi za Rais Magufuli. Tunasema Asante Rais, asante sana Rais. Ndani ya miaka mitano ametutoa wapi na kutupeleka wapi.”

“Kuteua wanawake wenye ulemavu hadi wengine kuwa mabalozi, naibu waziri na nafasi zingine ni jambo kubwa sana kwetu,” amesema

Katibu Mkuu huyo ameomba Rais Magufuli akutane nao ili kuweza kuzungumza ana kwa ana ikiwemo kumpa pongezi hizo.”

“Hapa tulipo tunatamani tuwe nawe. Hatuzidi hata 20, ila tunaomba kukutana nawe. Tutashukuru sana,” amesema.

Jumuiya ya Wanawake ya Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata) wamempongeza Rais John Pombe Magufuli jinsi alivyotambua mchango wa watu wenye ulemavu katika Serikali aliyoiunda. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea). Pia, wamempongeza jinsi alivyotambua kundi hilo kwa kuwasaidia mathalani vifaa mbalimbali vya kujifunza na kufundishia kwa shule za msingi na sekondari pamoja na asilimia mbili za wenye ulemavu. Pongezi hizo zimezitoa leo Jumatano tarehe 17 Juni 2020 na viongozi wa Jumuiya hiyo wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuelezea miaka mitano ya utawala wa Rais Magufuli. Shivyawata inaundwa na vyama mbalimbali kumi…

Review Overview

User Rating: Be the first one !

About Mwandishi Wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!