Tuesday , 16 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Waziri Mkuu Majaliwa aunda tuwe kuchunguza ajali ya moto Morogoro
Habari MchanganyikoTangulizi

Waziri Mkuu Majaliwa aunda tuwe kuchunguza ajali ya moto Morogoro

Spread the love

WAZIRI mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imeunda tume ya wataalam mbalimbali kuchunguza kama mamlaka za serikali ziliwajibika ipasavyo katika kudhibiti ajali ya moto iliyotokana na lori la mafuta iliyosababisha vifo na majeruhi Mkoani Morogoro. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Waziri Majaliwa aliyasema hayo katika viwanja vya chumba cha kuhifadhia maiti kwenye hospitali ya Rufaa mkoani Morogoro, wakati utambuzi wa miili ya watu waliokufa kwa kuungua na ajali ya hiyo uliotokana na mlipuko wa gari la mafuta uliotokea Agosti 10 majira ya saa 2:30 asubuhi kwenye eneo la Itigi Msamvu.

Majaliwa alisema kuwa tume hiyo itakayodumu kuanzia Agosti 11 hadi Agosti 16, imeundwa ili serikali iweze kujiridhisha kama vyombo vya ulinzi ikiwemo Polisi, kikosi cha usalama barabarani na Jeshi la Zimamoto viliwajibika ipasavyo toka gari hilo la mafuta la kampuni ya Chesco ya Mafinga kuanguka  huku watu wakichota mafuta na hatimae kulipuka na kuua watu na kusababbisha majeruhi.

“Na sisi serikali lazima tujiridhishe, ndani ya serikali kama tuliwajibika vizuri, ajali hii imetokea katikati ya manispaa, tena saa mbili asubuhi  watu wanafanya kazi, je wakati ajali inatokea kila mmoja aliwajibika, ilivyoanguka tu nani alijitokeza kwanza,” alihoji Waziri Majaliwa.

“Ajali imetokea mahali penye shughuli nyingi za kijamii ikiwemo kituo cha basi, kuna trafiki, polisi wa ulinzi, je muda wa kukutana watu wote waliotangulia mbele ya haki, ni nani aliyewajibika kuwazuia?  Na toka lori lilipoanza kuungua fire walikuja kwa muda gani? Kuna vitu vingi hapa lazima tuviangalie ili tujue nani hakuhusika kwa namna yake, na kwa maana hiyo mimi nitaunda tume, na hiyo tume itaanza kazi leoleo,“ alisisitiza Majaliwa.

Aidha Waziri Majaliwa alisema serikali inasimamia mazishi kwa miili iliyotambulika ambayo itazikwa katika makaburi ya Kola, na kwamba ndugu watakaokuwa tayari kuchukua miili ya ndugu zao kwenda kuzika wenyewe kwenye makaburi ambayo yameshaandaliwa, na kuongeza kuwa utambuzi huo utafanyika mpaka Agosti 12.

Aliongeza kuwa kwa wale ambao watashindwa kuwatambua ndugu zao kutokana na kuungua vibaya, serikali itasimamia upimaji wa vinasaba (DNA) baina ya ndugu na miili ili kuhakikisha wanawatambua ndugu zao.

Hata hivyo majeruhi 65 wa ajali hiyo kati yao 46 wamehamishiwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili na 17 kubaki hospitali ya Rufaa Morogoro, huku mgonjwa aliyekuwa akisafirishwa kwa helkopta kufariki dunia akiwa hewani na kufanya idadi ya vifo kufikia 69.

Kwa upande wake Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge kazi ajira vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama, alisema lita 166 za damu wananchi wamejitolea kusaidia kuokoa majeruhi waliopo hospitalini, na kwamba watu 48 wamejitokeza kubaini ndugu zao ambapo maiti 33 zimeshatambulika.

Aliongeza kuwa misaada mbalimbali imeendelea kutolewa Ikiwemo mablanketi , madawa, vifaa tiba na elimu ya saikolojia kwa waathirika wa tukio hilo.

Alisema tayari Madaktari bingwa 10 kutoka hospitali za Mloganzila, Muhimbili na Benjamin Mkapa wameshawasili katika hospitali ya rufaa mkoani Morogoro kuendelea kutoa matibabu.

Nao baadhi ya ndugu waliojitokeza kuwatambua ndugu zao,  Emmanuel Benard na Benadikto Emanus walisema hali ya miili hiyo ni mbaya na ni ngumu kuitambua.

Aidha wameziomba mamlaka husika kutoa elimu kwa jamii  namna ya kuepukana na majanga kama hayo kutokana na tukio kama hilo kujitokeza kwa mara ya tatu nchini, ikiwemo la mdaula na Mbalizi jijini Mbeya.

Ajali hiyo ilitokea Agosti 10, majira ya alfajiri ambapo lori lenye namba za usajili T. 717 DFF aina ya Scania likivuta tera lenye namba T, 645 CAN lililokuwa na shehena ya mafuta aina ya Petroli na Dizeli lililolipuka moto na kusababisha vifo na majeruhi hao.

Hata hivyo viongozi mbalimbali walihudhuria katika tukio hilo wakiwemo Mawaziri, manaibu waziri, Wabunge, Madiwani na wenyeviti na makatibu wa vyama vya siasa.

Mwisho.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Samia arejesha mikopo ya 10%, bilioni 227.96 zatengwa

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amerejesha utaratibu wa utoaji mikopo...

Habari Mchanganyiko

Sekta binafsi yasifu utekelezaji wa Mkumbi

Spread the loveSERIKAL imepongezwa kwa utekelezaji wa mapendekezo ya sekta binafsi kupitia...

Habari Mchanganyiko

Kamati ya bunge yapigia chapuo kilimo ikolojia

Spread the loveSERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imeshauriwa kushirikiana na wadau wa...

Habari Mchanganyiko

Serikali yapata hasara 113 milioni hospitali kuwapa misamaha wagonjwa wasiostahili

Spread the loveSERIKALI imepata hasara ya kiasi cha Sh. 111.76 milioni, baada...

error: Content is protected !!