Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Waziri Mkuu Majaliwa akagua SGR, yazalisha ajira 18,700
Habari Mchanganyiko

Waziri Mkuu Majaliwa akagua SGR, yazalisha ajira 18,700

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Masanja Kadogosa, ndani ya treni inayotumia umeme alipokagua mradi wa reli ya kisasa ya SGR
Spread the love

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na kusema mradi huo umesaidia kupungua tatizo la ajira kwa kuajiri wafanyakazi 18,700. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea).

“Kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huu, kumesaidia kupunguza ukosefu wa ajira kwa kutoa ajira 7,400 kwa kipande cha Dar hadi Morogoro.”

“Kipande cha Morogoro hadi Singida kimetoa ajira 6,300 wakati mradi wa umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere nao pia umetoa ajira 5,000,” alisema Waziri Mkuu

Waziri Mkuu alisema hayo jana Alhamisi, tarehe 14 Mei 2020 baada ya kutembelea mradi huo na kuzungumza na wananchi aliowakuta kwenye stesheni ya Soga, iliyoko wilayani Kibaha, mkoani Pwani.

Alisema faida nyingine ya mradi huo katika awamu yake ya kwanza, ni kupunguzwa kwa muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Morogoro.

Aliwataka wananchi hao wawe walinzi wa mradi huo kwa sababu utakapokamilika utawanufaisha na wao pia.

Reli hiyo itakuwa na vituo sita vya Dar es Salaam, Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere na Morogoro, huku vituo vya Dar es Salaam na Morogoro vikiwa ndiyo vituo vikuu.

“Kwenye vituo vya kushusha abiria vya reli hii, kutakuwa na huduma za kibenki na maduka, kwa hiyo wananchi hata kama hamsafiri, mtaweza kupata huduma na mahitaji yenu kutokea hapo,” alisema.

Akielezea maendeleo ya mradi huo unaojengwa kwa awamu mbili, Waziri Mkuu amesema Serikali iliweka malengo ya kukamilisha mradi huo kwa wakati na ndiyo maana aliamua kwenda kuukagua.

“Katika awamu ya kwanza, ambayo inatoka Dar es Salaam hadi Morogoro (km. 300), mradi huu umekamilika kwa asilimia 77.91. Hii maana yake ni kwamba wamemaliza kazi hii kwa zaidi ya robotatu. Wametengeneza njia na kulaza mataruma na mimi nimekuja na hii treni maalum kwa karibu kilometa 20,” alisema huku akishangiliwa na wananchi hao.

“Rais wetu, Dk. John Pombe Magufuli alianzisha mradi huu na kuwaahidi Watanzania kwamba tunaweza kuujenga kwa fedha zetu. Vilevile, mradi huu ni utekelezaji wa agizo la Ilani ya CCM ambalo linaitaka Serikali ya awamu ya tano, iimarishe usafiri wa reli nchini.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akishuka, ndani ya treni inayotumia umeme, wakati alipokagua mradi wa reli ya kisasa ya SGR

Alisema katika kutekeleza agizo hilo, Serikali ya awamu ya tano, mbali ya kujenga reli hiyo ya kisasa, imefanikiwa pia kufufua reli ya kutoka Dar – Tanga – Moshi ambayo ilikuwa haitumiki kwa zaidi ya miaka 20. Huduma ya mizigo katika reli hiyo ilikuwa haifanyi kazi kwa miaka 12 na huduma ya kusafirisha abiria ilisitishwa tangu mwaka 1994.

Akielezea kuhusu awamu ya pili ya ujenzi wa mradi huo, Waziri Mkuu amesema ujenzi wa reli kutoka Morogoro hadi Makutupora, Dodoma (km. 422) ulianza mwaka jana mwishoni na sasa hivi umefikia asilimia 30 ya kazi, ambapo wanatarajia kuukamilisha ifikapo Juni, 2021.

Waziri Mkuu alisema sambamba na ujenzi wa reli hiyo, umeme pia umeanza kuwekwa ambapo nguzo 154 kati ya 160 zinazotakiwa kuwepo zimeshasimikwa.

“Tumeweka miundombinu ya umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere, kutoka Kidatu na Kinyerezi. Nia yetu ya kupata umeme kutoka vyanzo vyote vitatu, ni kuhakikisha kuwa umeme upo saa zote.”

“Tuna uhakika wa kutumia umeme wa Kinyerezi na Kidatu au Kidatu na Mwalimu Nyerere au Mwalimu Nyerere na Kinyerezi na hata umeme ukikatika kabisa, mabehewa yetu yana uwezo wa kutunza umeme kwa dakika 45, na katika muda huo, ni lazima tutakuwa tumerejesha umeme kutoka chanzo kimojawapo,” alisema.

Waziri Mkuu amesema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa reli hiyo na akawapongeza mafundi wa kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki ambayo inajenga reli hiyo.

“Kampuni ya Yapi Merkezi imefanya kazi kama walivyosaini kwenye mkataba na Serikali, na ninaamini watakamilisha kazi kabla ya muda,” alisema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

error: Content is protected !!