March 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Aweso awasimamisha watatu DDCA, atoa maagizo Dawasa

Juma Aweso, Waziri wa Maji

Spread the love

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewasimamisha kazi watumishi watatu wa Wakala wa Uchimbani Visima (DDCA) kutokana na tuhuma za ubadhilifu na kuagiza uchunguzi dhidi yao ufanyike. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea)

Pia, ameiagiza Mamlaka ya Majisadi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) kuongeza mikoa ya kihuduma ili kuhakikisha inasogeza huduma kwa wananchi.

Waliosimamishwa ni; Abdallah Abdulhaman (Kitengo cha Ufundi), Fadhir Sauko (Kitengo cha Utafiti wa maji ardhini) na Hamad Msuwa wa Kitengo cha Manunuzi.

Aweso amechukua uamuzi huo leo Jumatatu tarehe 14 Desemba 2020 alipofanya ziara ya kutembelea miradi ya maji mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Amemuagiza Katibu Mkuu, Wizara ya Maji,Mhandisi Antony Sanga kufanya uchunguzi wa tuhuma za Chuo cha Maji kuhusu uuzwaji wa nyumba za chuo kinyume na utaratibu ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Awataka watendaji waliopo chini ya Wizara ya Maji, kufanya kazi kwa kufuata misingi na kanuni za utumishi wa umma.

Aweso ameahisi kutowafumbia macho watumishi wasio waaminifu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja

Kuhusu Dawasa, amesema ili kuwafikia wananchi karibu zaidi ni lazima kuongeza mikoa ya kihuduma.

Kwa sasa, Dawasa ina mikoa 15 ya kihuduma ikiwa ni mamlaka ya maji kubwa kuliko zote nchini Tanzania ikiwa inaongoza pia katika ukusanyaji wa mapato.

“Mnafanya kazi nzuri Dawasa kwa kusimamia vyema miradi ya maji kwa ufanisi na kuleta matokeo makubwa kwa haraka zaidi, lakini ongezeni mikoa ya kihuduma ili kuwasogezea wananchi huduma,” amesema Aweso

Aweso ameitaka Dawasa kuhakikisha Mradi wa Maji Mkuranga -Vikindu unakamilika kabla ya muda wa mkataba ambao ni Februari 2021 ili wananchi waanze kupata huduma ya majisafi.

Waziri huyo ameahidi kuwalipa wakandarasi kwa wakati ili mradi uweze kumalizika mapema huku akiipongeza
kampuni ya Shanxi Construction Engineering kwa kukamilisha ndani ya wakati.

Agizo jingine ambalo Aweso amelitoa ni kuitaka Dawasa kukaa pamoja na ofisi ya bonde la maji Wami ili kupata eneo kubwa zaidi kwa ajili ya kulinda chanzo cha Maji kwa Mji wa Mkuranga.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja amemuahisi Waziri Aweso kutekeleza maagizo yake ili kusogeza huduma kwa wananchi kwa kasi zaidi.

Mhandisi Luhemeja amesema, wanaendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwa fedha za mapato ya ndani ili kuhakikisha wananchi wanapata majisafi kwa wingi.

error: Content is protected !!