Saturday , 20 April 2024
Home Kitengo Habari Kimataifa Wauwaji wa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi waumbuka
KimataifaTangulizi

Wauwaji wa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi waumbuka

Mwandishi Jamal Khashoggi enzi za uhai wake
Spread the love

SIRI juu ya mauaji ya mwandishi wa habari wa kimataifa raia wa Saudia, Jamal Khashoggi, zimeanza kufichuka. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa kutoka jijini Istanbul nchini Uturuki zinasema, ushahidi huo mpya umekuja kufuatia kupatikana kwa kanda mpya za Kamera za CCTV zilizokuwa zimefungwa kwenye nyumba moja iliyopo karibu na jengo la ubalozi wa Saudia. 

Kamera hizo za CCTV zilikuwa zimefungwa na majasusi wa Uturuki. Jama Khashoggi, anaonekana katika kamera hizo zilizokuwa zimefichwa, akiuawa na genge moja la wauaji ndani ya ubalozi huo.

Kanda hizo zilizorekodiwa zimesikika na watu wachache sana, wawili kati ya watu hao tayari wamezungumza na kipindi cha BBC cha Panorama.

Jasusi wa Uingereza, Baroness Hellena Kennedy, alisikia wakati Jamal Khashoggi alipokuwa akifariki.

”Tisho la kusikiliza sauti ya mtu, hofu katika sauti ya mtu na kwamba unamsikiza mtu aliye hai; inakufanya uingine na hofu mwilini,” anaeleza Kennedy akiandika maelezo ya mazungumzo aliosikia kati ya wanachama wa kundi hilo la wauaji wa Saudia.

Anasema, “unaweza kuwasikia wakicheka. Ni biashara ya kuogofya. Wanasubiri hapo wakijua kwamba huyu mtu ataingia na kwamba atauwawa na kukatwa katwa.”

Kennedy alialikwa kujiunga na kikosi kinachoongozwa na Agnes Callamard, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa (UN), kuhusu mauaji ya kiholela.

Akimnukuu Callamard, mwanaharakati maalum wa haki za kibinadamu, Kennedy anasema, “niliambiwa kuhusu jukumu la kutumia uwezo wangu kuchunguza mauaji hayo, wakati Umoja wa Mataifa ilipochelewa kuanzisisha uchunguzi wa kimataifa.”

Mjumbe huyo maalum wa UN kuhusu mauaji ya kiholela, anasma limchukua takriban wiki kadhaa kuwabembeleza majasusi wa Uturuki kumruhusu yeye na Kennedy, pamoja na mkalimani wao wa Kiarabu kusikiliza kanda hizo.

”Lengo la Uturuki kuniruhusu kuzisikiliza lilikuwa ni kuthibitisha mipango iliyofanywa kabla ya mauaji hayo,” anasema Keneddy na kuongeza: ”Sina wasiwasi akilini mwangu, kwamba ulikuwa mpango mkubwa na ulioandiliwa kutoka juu. Haikuwa operesheni ndogo.”

Waliweza kusikiliza dakika 45 zilizotolewa katika kanda hiyo iliorekodiwa kwa siku mbili.

Jamal Khashoggi alikuwa mjini Istanbul – mji ambao wapinzani wa serikali kadhaa Mashariki ya Kati wamekuwa wakijificha – wiki chache kabla ya kuuawa.

Baba huyo mwenye umri wa miaka 59 aliyetalakiana na mkewe, alikuwa amechumbiana na mpenzi wake mpya, Hatice Cengiz, mtafiti msomi wa Uturuki.

Walikuwa na matumani ya kuanzisha maisha ya pamoja katika mji huo ulio na mchanganyiko wa raia; Khashoggi ilimhitaji hati za talaka ili kufunga ndoa tena.

Mnamo tarehe 28 Septemba, yeye na mchumba wake, Hatice Cengiz, walielekea katika ofisi ya mji wa Uturuki lakini waliambiwa kwamba walihitaji kupata makaratasi hayo kutoka kwa ubalozi wa Saudi.

Hiyo ndio ilikuwa njia ya mwisho. Alilazimika kwenda ili kujipatia makaratasi yake kutoka kwa ubalozi ili kufunga ndoa rasmi kwa sababu hakuweza kurudi kwao Saudia, Cengiz alianiambia tulipokutana katika mkahawa mmoja.

Khashoggi aliambiwa arudi siku nyengine. Lakini mara tu baada ya kuingia kwenye ubalozi huo, simu zilianza kupigwa mjini Riyadh nchini Saudia; zote zikirekodiwa na majasusi wa Uturuki.

Kile kilichovutia kuhusu simu hizo ni kwamba zilikuwa zikimtaja Khashoggi kama mtu aliyekuwa akitafutwa, kulingana na Callamard.

Hatice Cengiz, mke wa Jamal Khashoggi akiwa na mume wake enzi za uhai wake

Simu ya kwanza inaaminika kumwendea msaidizi wa Saudia mwenye uwezo mkuu katika afisi ya mawasiliano kwa jina Saud al-Qatani.

Inaelezwa na kuthibitika kwamba simu zote katika ofisi hiyo ya mawasiliano, zilikwenda kwa Saud al-Qatani, anaendelea.

Saud al-Qatani ametajwa moja kwa moja katika kampeni tofauti dhidi ya watu binafsi. Wakati Khashoggi ana kwenda katika ubalozi, Cengiz alilazimika kusalia nje.

Cengiz anasema, mchumba wake huyo, aliambiwa arejee tena siku nyingine na kwamba maombi yake yatafanyiwa kazi.

Al-Qahtani tayari alikuwa ametuhumiwa katika utekaji na utesaji wa watu kadhaa waliokuwa wametajwa kuwa wapinzani wa serikali ya Saudia, akiwamo mwanaharakati wa kike aliyejaribu kuendesha gari kabla ya marufuku hiyo kuondolewa pamoja na maafisa wengine wakuu waliokataa kuitii serikali ya nchi hiyo.

Katika maandishi yake, Khashoggi alimshutumu al-Qahtani kwa kuongoza kundi la wauaji wa mwanamfalme huyo.

Qahtani alianza kufanya huduma zisizo za kawaida – zenye siri, kulingana na Ignatius ambaye amewahi kumchunguza mshauri huyo wa Ufalme wa Saudia.

Hiyo ndio ilikuwa kazi yake na aliisimamia bila huruma. Kuna rekodi za takriban simu nne tarehe 28 Septemba kati yake na ubalozi na Riyadh.

Simu hizo ni pamoja na mazungumzo kati ya balozi mkuu na mkuu wa usalama katika wizara maswala ya kigeni, ambaye alimwambia siri kubwa ya ubalozi huo, ni jukumu la kitaifa.

Mchana wa tarehe mosi Oktoba, maafisa watatu wa Ujasusi kutoka Saudia, walisafiri hadi mjini Istanbul. Wawili kati yao, walikuwa wakifanya kazi katika afisi ya mwanamfalme wa Saudia.

Callamard anamini kwamba walikuwa na mradi waliotarajiwa kutekeleza. Walichunguza jumba la ubalozi huo wakajua ni kipi kinaweza kufanyika na kipi hakiwezekani.

Anasema, “nikiwa mjini Istanbul nilikutana na afisa mmoja aliyekuwa jasusi wa Uturuki aliyefanya kazi kwa takriban miaka 27.

Khashoggi hajawahi kuwa mkimbizi, lakini alilitoroka taifa lake, kutokana na kusakamwa na utawala wa Saudia.

Cengiz anasema, “nilikutana naye Jamal Khashoggi, miaka 15 iliyopita kwenye ubalozi wa Saudi huko Mayfair mjini London. Tukajadiliana kuhusu shambulio la kigaidi lililotekelezwa na Al-Qaeda. Khashoggi alikuwa akimjua kiongozi wake Saudia, Osama bin Laden kwa miongo kadhaa.”

Khashoggi alikuwa akilihurumia sana lengo la kundi la Al-Qaeda kupindua utawala wa kimabavu wa mataifa ya mashariki ya kati. Lakini baadaye alizungumzia kuhusu ukatili wa kundi hilo baada ya maoni yake kuwa huru na kupigania demokrasia.

Mwaka 2007, alirudi nyumbani na kufanywa kuwa mhariri wa gazeti la Al-Watan, linalounga mkono serikali.

Lakini alifutwa kazi miaka mitatu baadaye kwa kile alichoelezea kusababisha mijadala kupita mipaka ya serikali hadi katika jamii.

Mwaka 2011, alishinikizwa na tukio la mapinduzi ya Arab Spring, na kwamba Khashoggi alikuwa akizungumzia kile alichotaja kuwa serikali dhalimu ya Saudia.

Kufikia mwaka 2017, alikuwa amepigwa marufuku kutoandika na akeleekea mafichoni nchini Marekani. Mkewe alilazimishwa kumpatia talaka.

Khashoggi alikuwa mchangiaji wa gazeti la The Washington Post ambalo aliliandikia machapisho 20 makali mwaka mmoja kabla ya kifo chake.

Wakati alipokuwa muhariri nchini Uingereza alikuwa akivuka mipaka, kulingana na David Ignatius mchangiaji mkuu wa maswala ya kigeni wa gazeti hilo na mwandishi mpekuzi.

Kile nilichoona kwa Jamal ni kwamba alikuwa akijiweka katika matatizo kila mara kwa kuzungumza kilichokuwa akilini mwake.

Ukosoaji mkubwa wa Khashoggi ulimlenga mwanamfalme mpya Mohammed bin Salman.

“Alisema kwamba hakuna kitu cha kuogopa, aliitamani nchi yake sana na kwamba mazingira kama hayo yalimfanya kuhisi vyema,” anaeleza David kuhusu maisha ya Khashoggi.

MBS, kama anavyojulikana, alipendwa na wengi katika mataifa ya magharibi. Alionekana kama mwanaharakati mkubwa wa mabadiliko akiwa na maono mapya ya taifa hilo.

Hata hivyo, nyumbani Saudia alikuwa akiwasaka na kuwakabili wapinzani; na Khashoggi alikuwa mmoja wao kutokana na machapisho yake.

Metin Ersoz ni mtaalamu kuhusu Saudia na misheni zake maalumu. Yeye anasema, huduma za ujasusi zilianza kuwa na nguvu nchini humo baada ya Mohammed Bin Salman kuwa mwanamfalme.

Anasema, “walianza operesheni za kuteka watu na kuwakabili wapinzani, Khashoggi alichelewa kutambua tisho hilo na kuchukua tahadhari.”

Mapema tarehe 2 Oktoba 2018, ndege ya kibinafsi ilitua katika uwanja wa ndege wa Istanbul. Ndani ya ndege hiyo walikuwapo raia tisa wa Saudia, akiwemo mwanapatholojia aliyefahamika kwa jina la Dk. Salah al-Tubaigy.

Baada ya kugundua ni akina nani na wanakotoka, Callamard anaamini hilo ndio kundi lililotekeleza mauaji. Anazidi kufafanua kuwa wawili kati yao watu hao walikuwa na pasipoti za kidiplomasia.

Erosz anasema kwamba ujumbe kama huo – wenye operesheni maalum – ungehitaji ruhusa kutoka kwa mfalme wa Saudia ama mwanamfalme.

Raia hao wa Saudia waliigia katika hoteli ya Movenpick, ambayo haipo mbali na ubalozi huo.

Kabla ya mwendo wa saa nne kanda za video za CCTV zinamuonyesha afisa mmoja wa kundi hilo la mauaji akiingia katika ubalozi huo wa Saudia.

Ukisikiliza kanda hizo, Kennedy anaamini kwamba Maher Abdulaziz Mutreb ndio mtu aliyesimamia operesheni hiyo.

Mutreb alionekana mara kwa mara akisafiri na mwanamfalme, akiwa nyuma nyuma pamoja naye kama afisa wake wa usalama.

”Katika simu hizo zilizopigwa kati ya balozi na bwana Mutreb, tulipata ujumbe kwamba Khashoggi atakuwa akizuru ubalozi huo siku ya Jumanne”, kulingana na Kennedy.

Jioni ya tarehe 2 mwezi Oktoba, Khashoggi alipokea simu ikimtaka kufika katika ubalozi huo wan chi yake, ili kupata makaratasi yake aliyohitaji.

Huku yeye na Cengiz wakielekea katika ubalozi huo, kulikuwa na mawasiliano ya kushangaza ya simu yaliokuwa yakiendelea kati ya bwana Mutreb na mwanapatholojia al-Tubaigy.

”Anazungumzia kuhusu jinsi atakavyochunguza mwili wa marehemu. Unaweza kuwasiki wakicheka,” Kennedy anaeleza akimnukuu Tubaigy akisema, yeye husikiliza muziki anapokata wafu ”na mara nyengine mimi huvuta sigara na kunywa chai.”

Kwa mujibu wa Kennedy, ”baadaye kanda hizo zinafichua kile daktari huyo anachofaa kufanya. Ni mara ya kwanza maishani mwangu, nitalazimika kukata vipande vipande,” anakumbuka akisema. Hata iwapo wewe ni mchinjaji unamtundika mnyama mahali kabla ya kumchinja.”

Ofisi ya juu katika ubalozi huo ilikuwa tayari imetayarishwa. Sakafu yake ilifunikwa kwa kutumia plastiki. Maafisa wote wa ubalozi wa Uturuki walipewa siku ya kupumzika.

”Walikuwa wakizungumza, ‘je ni lini Khashoggi atawasili na walikuwa wakisema: ‘Je mnyama huyo wa sadaka amewasili? Hivyo  ndivyo walivyokuwa wakimuita,” anasimulia Kennedy.

Alikuwa ananisomea kutoka katika kitabu chake, Tisho katika sauti.

Mwendo wa saa saba, kanda hizo za CCTV zilimuonyesha Khashoggi akiingia katika jengo hilo. Nakumbuka tulielekea huko tukiwa tumeshikana mikono na tupofika katika jumba la ubalozi huo Jamal alinipatia simu zake na kusema: Tuonane baadaye mpenzi, nisubiri hapa, alisema Cengiz.

Khashoggi alijua kwamba simu zake zitachukuliwa katika eneo la mlango wa ubalozi huo na hakutaka Wasaudi kuwa na simu yake ili kusoma taarifa zake za faragha.

Kanda hizo zinafichua kwamba anaonekana akipokelewa ndani ya ubalozi na kuambiwa kuna agizo la polisi wa kimataifa ambao wanataka kumkamata na kwamba ni sharti arudi Saudia.

Anasikika akikataa kumtumia ujumbe mwanawe ili kuhakikisha kuwa familia yake ipo salama.

Kunyamazishwa kwa Jamal baadaye kunaanza.

“Kuna wakati ambapo ungeweza kumsikia Khashoggi mwenye hofu na baadaye kugundua kwamba kitu hatari kilikuwa karibu kifanyike”, alisema Kennedy.

Anaendelea kusimulia, kuna kitu kinachotisha hususan sauti yake inapobadilika. Unyama huo utausikia vizuri unaposikiliza kanda hizo.

Callamard hajui iwapo Khashoggi alifahamu njama hizo za Saudi. Sijui kama alifikiria kwamba anaweza kuuawa, lakini nadhani alikuwa akifikiri kwamba huenda wakamteka.

Anauliza: “Je, mnataka kunidunga sindano?” Anajibiwa  ndio. Kennedy anasema kwamba alimsikia Khashoggi akiuliza mara mbili iwapo anatekwa na baadaye anaendelea kusema vipi jambo kama hili linaweza kutokea katika ubalozi?

Callamard anasema, “sauti utakazosikia baada ya hilo ni kana kwamba anaminywa pumzi. Pengine kwa kutumia karatasi ya Plastiki katika kichwa chake.”

”Mdomo wake pia ulifungwa kwa kutumia nguvu pengine kwa kutumia mkono ama kitu chengine. Kennedy anaamini kwamba baadaye daktari huyo wa kupasua mfu anachukua zamu kufuatia agizo la kiongozi wa operesheni hiyo.

Unasikia sauti kwamba wacha amkate, na anasikika kama bwana Mutreb. Baadaye mtu anapiga kelele, “kwisha na mtu mwengine anapiga kelele ondoa ondoa. Weka hii katika kichwa chake funga. Nilifikiri kwamba walimkata kichwa chake.”

Baada ya takribani kupita muda wa nusu saa tangu Khashoggi alipomuacha nje ya jengo la ubalozi mchumba wake, Bi. Cengiz, anasema, “nilianza kufikiri kuhusu hatma yangu na jinsi ndoa yetu itakavyokuwa. Tulikuwa tukipanga sherehe ndogo.

Mwendo wa saa tisa CCTV zinaonyesha gari la ubalozi likiondoka na kuwasili katika makao ya balozi ambapo ni barabara mbili kutoka hapo.

Watu watatu wanaonekana wakiingia na sare za ofisini wakibeba mifuko ya plastiki. Callamard anaamini walikuwa wakibeba vipande vya mwili wa Khashoggi. Haikuchukua muda mrefu, gari hilo linaondoka.

Nje maelezo ya kutisha wakati wa mauaji hayo, kuna swali linaulizwa na limeelezwa na baadhi ya vyombo vya habari, hasa kuhusu kutumika kwa msumeno kukatakata vipande vidogo vidogo mwili wa Khashoggi.

Kennedy anasema, “sikusikia sauti za kukata na msumeno, ningefananisha na kifaa cha kukata kinachotumika wakati wa upasuaji.”

Lakini anasema, kulikuwa na sauti kama ile ya nyuki. Majasusi wa Uturuki wanaamini kwamba hiyo ndio iliokuwa sauti ya msumeno. Mwendo wa saa tisa na dakika 53, kanda za CCTV ziliwaonyesha maafisa wawili wa mauaji hayo wakiondoka katika ubalozi huo.

”Nilifuata nyayo zao katika barabara kupitia kamera zilizokuwepo ambazo zilionyesha njia iliokuwepo kati ya ubalozi na katikati ya mji wa zamani wa Istanbul.

”Mtu mmoja anaonekana amevalia mavazi ya Khashoggi, lakini akiwa na viatu tofauti. Mwengine ambaye sura yake imejificha anaonekana akibeba mfuko wa plastiki.”

Wanaelekea katika msikiti maarufu mjini Istanbul kwa jina Blue Mosque. Wanapotoka mtu aliyevalia nguo za Khashoggi amebadilisha nguo hizo. Wanapanda teksi na kurudi katika hoteli yao, wakitupa mifuko ya plastiki iliodaiwa kubeba nguo za Khashoggi katika jaa moja karibu kabla ya kuelekea katika barabara ya chini na kurudi katika hoteli ya Movenpick.

”Kuna kiwango cha juu cha mipango ya mauaji hayo ili kuonyesha kwamba hakuna kitu kibaya kilichotokea dhidi ya Khashoggi,” alisema Callamard. Wakati wote huu Cengiz alikuwa akisubiri nje ya ubalosi huo.

”Nilisubiri na kusubiri hapo hadi saa tisa na nusu. Halafu nilipogundua kwamba ubalozi umefungwa, nilianza kukimbia ili niingie. Nilijiuliza kwa nini Jamal hakutoka.

“Babu mmoja aliniambia kwamba haelewi ninachozungumzia. Mwendo wa saa kumi na dakika 41, Cengiz alikuwa na wasiwasi na kumpigia simu rafiki wa zamani wa Khashoggi,” anaeleza.

Alimpatia nambari yake iwapo pengine alikuwa katika tatizo lolote. Dkt Yasin Aktay ni mwanachama wa chama tawala cha Uturuki akiwa na mawasiliano na watu maarufu.

”Nilipokea simu kutoka kwa mtu mwenye nambari nisiojua, sauti yenye wasiwasi mkubwa kutoka kwa mwanamke ambaye sikuwa nikimjua,” alisema. ‘

Yasin alipiga simu kwa afisi ya ujasusi ya Uturuki na kuielezea afisi ya rais Tayyip Erdogan. Kufikia mwendo wa saa kumi na mbili unusu jioni, wanachama wa kundi hilo la mauaji walikuwa ndani ya ndege ya kibinafsi iliokuwa ikielekea Riyadh, chini ya saa 24 baada ya kuwasili.

Siku iliofuata, Serikali za Saudi na Uturuki zilitoa taarifa tofauti zinazokinzana kuhusu kile kilichotokea katika ubalozi huo.

Saudia ilisisitiza kuwa Khashoggi alikuwa ameondoka ubalozi huo. Uturuki ilisema kwamba bado yungali ndani.

Maafisa wa ujasusi wa Uturuki walikuwa tayari wakishutumu kuhusu rekodi hizo ikiwemo simu zilizopigwa siku nne kabla ya Khashoggi kutoweka.

Je, walijua kwamba maisha yake yalikuwa hatarini , na iwapo ni kweli kwa nini hawakuomuonya?

Sidhani walijua, hakuna ushahidi kwamba walikuwa wakisikiliza moja kwa moja kile ambacho kilikuwa kikitokea.

Kulingana na Callamard, ujasusi kama huu hufanyika kila siku, na ni wakati ambapo kuna tukio kubwa ambapo kanda kama hizo huchunguzwa.

Ni kwa sababu bwana Khashoggi aliuawa na kutoweka ndio maana walichunguza kanda hizo. Ersoz ananiambia kwamba mwenzake wa Ujasusi alisikiliza kanda hizo moja baada ya nyengine na kusikiliza kati ya saa 4,000 na 5000 ili kutafuta siku muhimu na dakika 45 zilizowasilishwa kwa Callamard na Kennedy.

Siku nne baada ya kifo cha Khashoggi, kikosi chengine cha Saudia kiliwasili kikidai kuchunguza kilichotokea. Callamard anaamini kilikuwa kikosi kilichowasili ili kufagia na kuficha yaliotokea.

Ubalozi huo ni eneo la Saudia kulingana na sheria ya kimataifa na kwa wiki mbili Saudia haikuruhusu wachunguzi wa Uturuki kuingia.

”Kufikia wakati ambapo walikuwa wakikusanya ushahidi, hakukuwa na kitu, hata chembechembe za DNA za bwana Khashoggi hazikuwepo licha ya yeye kuwepo ndani yake,” alisema Callamard na kwamba eneo hilo lilisafishwa kabisa.

Hata hivyo, jioni ya siku hiyo, mamlaka ya Uturuki iliambia vyombo vya habari kwamba Khashoggi aliuawa katika ubalozi wa Saudia.

”Jamal hakuhitaji kufanyiwa hivyo, alihitaji mema zaidi”, alisema Cengiz. Jinsi walivyomuua kuliua matumaini yangu yote.”

Ndani ya ubalozi kukiwa na kinga ya kidiplomasia, kunauweka utawala wa Uturuki katika wakati mgumu wa kuingia kuchunguza mauwaji hayo.

Pamoja na shinikizo kutoka kwa mamlaka ya Uturukji, Saudia ilikataa kukiri mauaji hayo , ikisema kwamba kulikuwa na vita ndani ya ubalozi huo na kuamua ilikuwa operesheni ngumu.

Lakini maandamano nje ya Ubalozi wa Saudia nchini Uturuki baada ya kutoweka kwa Jamal Khashoggi, kuliifanya Uturuki kufichua kile ilichojua kwa vyombo vya habari vya kimataifa.

Baadaye waliwaalika wawakilishi wa CIA na mashirika mengine machache ya ujasusi, ikiwemo M16, kusikiliza kanda hizo, na kuthibitisha kwamba Khashoggi aliuawa na raia wa Saudia.

Shirika la kijasusi la CIA lilitamatisha kwa kusema kwamba kulikuwa na uwezekano kwamba huenda Mohammad bin Salama aliagiza mauaji hayo. Waliwaelezea pia wabunge ambao walibaini kilichotokea.

Mwezi Januari mwaka huu, serikjali ya Saudia iliwashtaki watu 11 mjini Royadh, ikiwemo Mutreb na Dkt al-Tubaigy lakini sio aliyepanga mauaji hayo Saud al-Qahtani.

”Hajawahi kuhojiwa wala kuchunguzwa kutoa ushahidi. Nimeambiwa kwamba ametengwa na kila mtu ikiwemo familia yake lakini bado anawasiliana na mwanamfalme.”

”Ripoti ya Callamard kwa baraza la haki za kibinadamu katika umoja wa kimataifa ilifikia hitimisho lake. Hakuna ishara chini ya sheria ya kimataifa kwamba uhalifu huu unaweza kuchukuliwa kivyovyote vile isipokuwa mauaji ya serikali,” alisema Keddy.

”Kitu kibaya kinachoogofya kilifanyika katika ubalozi huo. Jamii ya kimataifa ina jukumu la kusisitiza uchunguzi wa kiwango cha juu kufanyika,” anaeleza na kusisitiza kuwa ufichuzi huu wa kanda za mauaji ya Khashoggi unapaswa kuchukulkiwa hatua za haraka na jamii ya kimataifa.

Uturuki imetaka kurudishwa kwa wale waliohusika ili kushtakiwa mjini Istanbul, lakini Saudia imekataa.

Serikali ya Saudia ilikataa kufanya mahojiano na kipindi cha BBC cha Panorama, lakini ilisema ilishutumu mauaji hayo na kwamba ilikuwa tayari kuwawajibisha waliohusika.

Ilisema kwamba mwanamfalme wa Saudia hahusiki kamwe na uhalfu ilioutaja kuwa mbaya zaidi

Katika maneno yake ya mwisho, Hatice Cengiz alionya kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa mauaji ya Jamal Khashoggi.

”Sio janga tu kwangu, lakini kwa umma wote , watu wote wanaofikiria kama Jamal na waliokuwa na msimamo kama yeye,” ameeleza Cengiz.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

error: Content is protected !!