JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha nchini Tanzania, limewakamata watu watatu wakituhumiwa kuchoma moto ofisi za chama kikuu cha upinzani nchini humo Chadema, Kanda ya Kaskazini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).
Ofisi hizo zilichomwa moto usiku wa kuamkia tarehe 14 Agosti 2020 na watu wasiojulikana na kusababisha uharibifu wa mali.
Leo Alhamisi tarehe 3 Septemba 2020, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Salum Hamduni ametoa taarifa kwa umma kuhusu tukio hilo akisema linawashikilia watu watatu ambao watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kamanda Hamduni amewataka watuhumiwa hao ni, Deogratius Malya, aliyekuwa mlinzi wa ofisi hiyo, Leonard Nkukula, dereva wa Chadema na Proster Makonya ambaye ni afisa mhamasishaji wa chama hicho makao makuu.
“Baada ya kukamilika kwa upelelezi, jalada la kesi hii limepelekwa ofisi ya taifa ya mashtaka kwa ajili ya kulisoma na kulitolea maamuzi au maelekezo ya kisheria ikiwa ni pamoja na kuandaa hati ya mashtaka,” amesema Kamanda Hamduni.
“Watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria,” amesema.
Leave a comment