Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wanawake wanavyotishia Uchaguzi Mkuu 2020
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Wanawake wanavyotishia Uchaguzi Mkuu 2020

Qeen Cuthbert Sendiga-ADC
Spread the love

KWA mara ya kwanza, Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu katikati ya wiki, Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 tangu mfumo wa vyama vingi uliporejea tena mwaka 1992. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)

Tangu mfumo wa vyama vingi uliporejea na uchaguzi mkuu wa kwanza ulioshiriki vyama vingi mwaka 1995, ulikuwa ukifanyika siku ya Jumapili.

Tayari michakato ndani ya vyama vya kuwapata wagombea udiwani, uwakilishi, ubunge na urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nawa Zanzibar inaendelea.

Ni uchaguzi ambao unatarajia kushuhudia ongezeko la wanawake wengi katika nafasi mbalimbali hususan za udiwani, ubunge na uwakilishi wakichuana kutafuta rifaa ya wananchi kupitia sanduku la kura.

Kwa nafasi ya urais, kati ya vyama 16 vilivyokwisha kuchukua fomu za uteuzi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wanawake ni wawili na wagombea mwenza ni watano.

Wagombea hao ni, Queen Cathbert Sendinga wa Chama cha ADC na Cecilia Augustino wa Demokrasia Makini.

Cecilia Augustino Mwanga wa Demokrasia Makini

NEC itafanya uteuzi wa wagombea urais tarehe 25 Agosti 2020 kisha kampeni za uchaguzi huo zitaanza 26 Agosti hadi 27 Oktoba 2020.

Visiwani Zanzibar, kati ya wagombea 32 waliochukua fomu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanawake walikuwa watano lakini mwisho wa mchakato, Dk. Hussein Ali Mwinyi alipitishwa kuwania nafasi hiyo.

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, tayari kimekwisha kuteua wagombea 230 wa ubunge kati ya majimbo 264.

Kati ya wagombea hao 230, zaidi ya wanawake 50 wamepitishwa na chama hicho kuwania ubunge ikiwa ni mara ya kwanza, Chadema inapitisha idadi kubwa ya wanawake kusimama majimboni.

Dk. John Magufuli-CCM

Vivyo hivyo, inatarajiwa kujitokeza katika vyama vingine kikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho bado hakijateua wagombea ubunge na uwakilishi.

Katika kura za maoni kwa vyama vyote, wanawake wamejitokeza kwa wingi ikiwa ni tofauti na chaguzi zilizopita ambapo walikuwa wakichangamkia fursa ya viti maalum.

Kujitokeza kwa wingi kwa wanawake, kunaweza kutoa ushindani mkali kwenye uchaguzi mkuu na huenda idadi ya wabunge wa majimbo, wawakilishi na madiwani wakaongezeka.

Tamko la asasi za kiraia

Wakati hayo yakiendelea ndani ya vyama, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TamwaA), Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) pamoja na Global Peace Foundation (GPF) wametoa tathimini ya kile walichobaini na kuomba malaka husika kuvifanyia kazi.

Lengo la asasi hizo za kiraia zilizoendesha midahalo kutoka vyama vya siasa, viongozi wa dini, wanawake wanasiasa na waandishi wa habari chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake Afrika, (AWDF) kupitia mradi wa ‘Wanawake Sasa’ ni kuhakikisha mwanamke anashirika vyema pasina vikwazo vyovyote kwenye uchaguzi huo mkuu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben

Akisoma tamko la pamoja la asasi hizo hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben anasema kupitia midahalo hiyo, wamebaini bado kuna changamoto  zinazosababisha ushiriki mdogo wa wanawake katika siasa na kuvitaka vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, kuondoa changamoto hizo.

Amebainisha baadhi ya changamoto zinazowakabili wanawake katika siasa ni lugha dhalilishi  zinazowavunja moyo wanawake  wanaogombea au walio katika nafasi za uongozi pamoja na familia zao kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

“Wanawake wanaogombea nafasi za uongozi, hukutana na changamoto  ya lugha dhalilishi wakati wa kampeni na hata wakati wa utendaji wao wa kazi ili tu kuwakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma.”

“Kama tunataka uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia, ni muhimu kwa tume ya uchaguzi na vyombo vya usalama kupiga marufuku na kutoa adhabu kali kwa wanasiasa watakaotoa lugha hizi dhidi ya wanawake,” anasema Rose.

Rose amesema, katika midahalo hiyo, wamebaini kuwepo kwa rushwa ya kifedha katika shughuli za kawaida za siasa na hasa wakati wa chaguzi mbalimbali za ndani ya vyama, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

“Hii ni pamoja na tabia za wajumbe wanaotegemewa kupiga kura kuwa na hulka ya kudai au kujenga mazingira ya kupewa “kitu kidogo” ili waweze kutoa ushirikiano kwa mgombea.”

“Hii inaathiri  wanawake ambao wengi wao hawana kipato cha kutosha hasa wanawake vijana,” anasema.

Rose anasema “tumebaini uwepo wa vitendo vya kuomba au kutengeneza mazingira ya rushwa ya ngono kwa baadhi ya wanaume wenye dhamana za kusimamia michakato ya chaguzi au mamlaka ndani ya vyama vya siasa.”

Anasema, changamoto hiyo husababisha wanawake kudhalilishwa na kuharibiwa ndoto zao za kisiasa na wakati mwingine familia au wenzi wao kuwazuia kushiriki katika siasa.

Mkurugenzi huyo amesema, hayo na mengine mengi, yanachangia wanawake, kuvunjika moyo hivyo kutoshiriki shughuli za siasa au kukosa nafasi za uongozi pale wanapokuwa na msimamo wa kutotoa rushwa.

“Katika hili tunapenda kutoa rai kwa wanawake wenzetu kukataa kabisa kudhalilishwa na kutojihusisha na vitendo vya rushwa ya fedha au ngono,” amesema.

“Pia, tunashauri jumuiya za wanawake ndani ya vyama vya sisasa kuvunja ukimya na kuhakikisha hoja za rushwa katika siasa inazungumzwa katika kila vikao vya jumuiya na vikao vingine muhimu.”

Rose amesema “tunaviomba vyama vya siasa viweke utaratibu madhubuti na wa siri wa kutoa taarifa za vitendo hivi na kuwe na kamati huru ndani ya vyama zisizofungamana na yeyote zitakazoratibu upokeaji, ufuatiliaji na utoaji adhabu kwa wale ambao bado wanaendekeza vitendo hivi vya kuwadhalilisha wanawake.

Kuhusu ushiriki wa wanawake, Rose anavitaka, vyama vya siasa kuwateua wanawake waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali kama za udiwani, ubunge na uwakilishi ili wagombee kwenye uchaguzo huo.

“Tunapenda kuvipongeza vyama vya siasa ambavyo vimetoa nafasi za wanawake kugombea nafasi za udiwani na ubunge na hata urais katika kura za maoni.”

“Mwaka huu wanawake wengi wamejitokeza. Tungependa kuviomba vyama vya siasa kuhakikisha wale wanawake wenye uwezo wasimamishwe kugombea nafasi hizo,” anasema.

Katika hilo, Rose anasema, “tunawaomba wananchi wote kuwachagua wanawake waliosimamishwa kugombea nafasi za ubunge na udiwani na wengine wapewe nafasi za teuzi mbalimbali.”

Anatumia fursa hivyo, kuvikumbusha vyama kuendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake ambao hawakupata nafasi mwaka huu ili waweze kusimama na kugombea chaguzi zijazo ndani ya vyama vyao, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Kadhalika tunapenda kuwaasa wanawake kuepuka kugawanywa na zile kauli kuwa, ‘hawapendani’ badala yake waendelee kushirikiana na kupeana fursa mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na masuala ya kijamii,” anasema.

Msimamo wa viongozi wa dini

Taasisi za za dini nchini – Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) zilikutana ili kujadiliana amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu.

Kikao hicho kilifanyika tarehe 8 Agosti 2020 jijini Dar es Salaam ambapo walisema, haki ndio msingi wa amani na Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC), itekeleze wajibu wake wa kusimamia haki pasi na kusikiliza sauti kutoka katika chama chochote.

Viongozi wa dini walipokutana na Rais Jakaya Kikwete

Kwenye kikao hicho ambacho pia kilijadili haki, wajibu wa kijamii na ushiriki wa wanachi katika uchaguzi huo Augustino Charles, Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar alisema, amani inajengwa kwa haki.

“Naamini kwamba amani inajengwa kwa haki, kunapokuwa na haki ambayo ndio msingi, amani itakuwepo. Amani tunayozungumzia wakati huu wa uchaguzi ni kwamba kila chama kiwe na nafasi sawa na kingine,” anasema

Sheikh Hamis Mataka, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata alisema, mkutano huo unaangazia haki na wajibu wa kijamii na ushiriki wa wananchi katika uchaguzi mkuu ujao.

“Tunahitaji amani kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi. Viongozi wa dini ni wadai wa uchaguzi, wanasiasa viongozi wa uchaguzi, Tume ya Uchaguzi wadau wa uchaguzi, wapiga kura wadau wa uchaguzi, kila mmoja anapaswa kutenda wajibu wake,” alisema Sheikh Mataka

Dk. Fredrick Shoo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) alisema, amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu ni jambo la muhimu.

“Ningeliomba kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi ijue imepewa dhamani kubwa sana na Watanzania, na wao ndio wenye kusimamia kwa uhuru, haki na uwazi ili uweze kwenda kwa utulivu.”

“Maana yake ni kuhakikisha kwamba haki za wagombea wote pasipo kuangalia chama zinalindwa, lakini pia haki za wapiga kura zinalindwa, na hapa tume ya uchaguzi ina kazi kubwa sana,” alisema Dk. Shoo.  

Kauli ya Rais Magufuli

Ijumaa tarehe 14 Agosti 2020, Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli akizungumza katika maadhimisho ya miaka 13 ya moto kwenye Mkutano Mkuu wa Kanisa la Assembly of God (TAG) jijini Dodoma, alisema Serikali anayoingoza imejipanga kuhakikusha uchaguzi unakuwa huru na haki.

Rais Magufuli alisema “uchaguzi ni zoezi muhimu katika kupata viongozi kwa njia ya kidemokrasia” na kuwaomba viongozi hao wa kiroho kutumia nafasi walizonazo kuhimiza waminini kushiriki katika uchaguzi huo.

“Hatuna budi kumwomba Mwenyezi Mungu atupatie viongozi wenye maono, wachapa kazi na wazalendo kwa Taifa letu, tusiangukie mikononi mwa viongozi wabadhirifu, wabinafasi au vibaraka,” alisema Rais Magufuli.

Kiongozi huyo wa nchi alitoa wito kwa wanasiasa wenzake “tujipange kufanya kampeni za kistaarabu, tusitumie lugha za kuwatisha wananchi wetu, niwaombe Watanzania tuwakatae wanasiasa wanaohibiri chuki na kutoa maneno ya vitisho.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!