Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Wananchi hawali takwimu, wanakula uchumi
Makala & Uchambuzi

Wananchi hawali takwimu, wanakula uchumi

Spread the love

Na Saed Kubenea

MSEMAJI wa serikali, Dk. Hassan Abass, amekana madai kuwa uchumi wa taifa unayumba, mfumuko wa bei umeongezeka na mifuko ya wananchi imetoboka.

Dk. Abass anasema, uchumi wa nchi bado uko imara. Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 6.1 hadi asilimia 5.4 Mei 2017.

Kwamba, katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, ukuaji wa uchumi haujapungua asilimia 7.2, kiwango ambacho ni cha “juu katika ukanda wa Afrika Mashariki.”

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Jumanne iliyopita, Dk. Abass amesema, pamoja na uchumi wa dunia kukumbwa na mtikisiko, lakini uchumi wa Tanzania bado uko imara.

Akizungumzia uhuru wa vyombo vya habari, Dk. Abass amesema, uhuru huo umekuwa wa juu nchini kulinganisha na nchi nyingine barani Afrika.

Miongoni mwa vigezo alivyotaja kuthibitisha kuwapo kwa uhuru wa habari na vyombo vya habari, ni serikali kuridhia mikataba ya kimataifa; wingi wa magazeti, vituo vya redio na televisheni.

Kwa mujibu wa Dk. Abbas, nchini Tanzania kuna magazeti 430 yaliyosajiliwa; redio zaidi ya 140 na vituo vya televisheni 32.

Dk. Abass alikuwa akijibu madai yaliyotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa uchumi wa taifa umeyumba na mfumuko wa bei umeongezeka.

Madai ya Chadema juu ya uchumi kuyumba, yalitolewa mbele ya waandishi wa habari na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe. Sasa tujadili:

Kwanza, kuna tofauti kati ya ukuaji wa uchumi kwa wananchi mmojammoja na “malisho ya takwimu” za serikali.

Kwa mfano, serikali inazungumzia uhuru wa vyombo vya habari, uhuru kwa waandishi wa habari na uhuru kwa wahariri; kwa kuangalia idadi ya magazeti, televisheni na redio.

Aidha, serikali inahubiri uwapo wa uhuru wa kupata habari na kutoa maoni, kwa takwimu za usajili wa magazeti. Basi.

Lakini kuwapo kwa idadi kubwa ya magazeti, redio na televisheni, siyo kigezo pekee nchi kuwa na uhuru wa habari. Yawezekana vyombo vingi miongoi mwa hivyo vikawa vya chama tawala au washirika wake.

Ni sharti uhuru wa vyombo vya habari uambatane na sheria na mfumo unaowezesha waandishi kufanya kazi bila kuingiliwa au kutishwa na serikali na vyombo vyake.

Mathalani, ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu cha utawala wa Rais John Magufuli, “kumekuwepo ufungiaji magazeti.”

Aidha, mkono wa serikali umetumika kusimamisha urushaji matangazo na vitisho dhidi ya waandishi wa habari, watangazaji, wapigapicha na wahariri.

Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu, vitisho na manyanyaso dhidi ya waandishi wa habari na wahariri wao wakiwa kazini, vimezidi kushamiri.

Ndani ya mwaka mmoja na nusu, kesi zimefunguliwa dhidi ya waandishi wa habari na wananchi wa kawaida wanaomjadili rais wao.

Kama watu hawako huru hata kumsema na kumjadili rais wao, uko wapi uhuru unaohubiriwa na Dk. Abass?

Vyombo vya dola vya serikali, likiwamo jeshi la polisi limekuwa kinara wa kuzuia na kuwanyanyasa waandishi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.

Hata ndani ya Bunge waandishi wanazuiwa kupiga picha. Wanazuiwa kupata baadhi ya taarifa. Wanaishia kulishwa kile ambacho serikali inataka; siyo ambacho waandishi wanahitaji kuwafikishia wananchi.

Kwa maneno mengine, vyombo vya habari vya kujitegemea bado vinashindwa kujieleza kwa ufasaha. Waandishi wa habari waliokataa kupakatwa na serikali, hawawezi kuandika kile wanachokiamini.

Pili, akihutubia Bunge la bajeti, Julai mwaka huu, waziri wa fedha na mipango, Dk. Philip Mpango alisema, kasi ya ukuaji wa uchumi Afrika Mashariki ilishuka kutoka asilimia 6.5 mwaka 2015 hadi asilimia 5.3 mwaka jana.

Alisema, kuporomoka kwa uchumi ulimwenguni, kumetokana na kushuka kwa bei ya bidhaa na kudorora kwa uchumi wa dunia.

Lakini Dk. Abass anasema, kuporomoka kwa uchumi wa dunia, hakukuathiri uchumi wa nchi. Hakujazorotesha mapato ya serikali wala kuathiri ajira za wananchi.

Sasa kama makusanyo yameongezeka, uchumi umeimarika na uwezo wa serikali wa kuhudumia wananchi umeboreshwa, kwa nini serikali haijaweza kuajiri wafanyakazi wapya?

Iwapo makusanyo yameongezeka kutoka Sh. 925 bilioni mwaka 2015 hadi kufikia Sh. 1 trilioni mwaka 2017, thamani ya shilingi imekuwaje? Siyo kweli kwamba wakati huo, shilingi iliuzwa kwa dola 1900 na sasa inauzwa kwa Sh. 2240?

Kwanini serikali inashindwa kuwalipa watumishi wake kwa wakati? Kwa nini imeshindwa kuwapandisha madaraja na kuwalipa stahiki zao?

Kwa nini serikali imeshindwa kutekeleza bajeti yake iliyopitishwa na Bunge? Rekodi zilizopo bungeni zinaonyesha serikali imetekeleza bajeti ya maendeleo chini ya asilimia 40 ya kile kilichopangwa.

Ikiwa mapato yameongezeka na utegemezi wa serikali umepungua, kwa nini serikali imeshindwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu?

Kwa nini jambo hili ambalo lilielezwa hata na Rais Magufuli kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, nalo limeshindwa kufanyika?

Au Dk. Abass hafahamu kuwa serikali inaposhindwa kugharimia elimu ya vijana wake na wakati huo inasema uchumi umeimarika, inapoteza uhalali wa kuaminika na hata kutawala?

Tunatarajia Dk. Abass afahamu kuwa kipaumbele cha nchi maskini yenye uongozi bora ni kuwekeza katika elimu ili ipate wataalamu wa kutosha kuikwamua katika umaskini. Hafahamu hilo?

Kama mapato yameongezeka, uchumi umeimarika na serikali inakaribia kujitegemea, kwa nini imeshindwa kujenga viwanda inavyodai ndio kipaumbele chake?

Kama mapato yameongezeka, uchumi umeimarika na mfumuko wa bei umepungua, kwa nini deni la taifa linaongezeka kila uchao?

Kwa nini serikali imeshindwa kulipa wazabuni wa ndani hadi wengine kufilisika? Hii nyongeza ya makusanyo inayoelezwa, inakwenda wapi?

Hata hicho kinachoitwa, “kuongezeka kwa bajeti ya wizara ya afya na hasa kwenye dawa,” kinaonekana ni upikaji wa takwimu.

Hoja ni kiasi cha fedha kilichopelekwa wizarani kutoka hazina kuu ya taifa. Kwamba serikali inasema, bajeti hiyo imeongezeka kutoka Sh. 30 bilioni mwaka 2015/16 hadi Sh. 251 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2016/17.

Lakini taarifa za wizara mbele ya kamati ya Bunge, hadi Machi mwaka huu, wizara ilikuwa imepokea Sh. 314.673 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.

Hiyo ni sawa na asilimia 40 tu ya fedha zote zilizotengwa na Bunge kwa ajili ya wizara ya fedha.

Katika mazingira hayo, hapo kuna ongezeko la fedha au takwimu? Nani anaweza kuwa na uhakika wa asilimia kwa mia kuwa zilizotengwa katika bajeti ya sasa zitapelekwa?

Kama msemaji wa serikali anasema, elimu ni bure bila kueleza jinsi wazazi wanavyochangia kiasi kikubwa cha fedha huko shuleni kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma, yumkini hataeleweka.

Tatu, tangu kumalizika uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015, kumekuwa na mkakati mahususi wa kutetea Rais Magufuli na serikali yake.

Katika baadhi ya maeneo kumeonekana kuwapo mkakati unaokwenda kinyume na sheria na hata katiba ya Jamhuri.

 

Kwa mfano, ndani ya Bunge, kumeshuhudiwa wabunge wa upinzani wakisimamishwa kuhudhuria mikutano ya Bunge, kinyume cha kanuni na Katiba.

Tumeona baadhi ya uamuzi bungeni ukitolewa bila kuzingatia kanuni, katiba na miongozo ya mabunge ya Jumuiya ya Madola. Tunaona Bunge likiwekwa kwenye “kwapa la serikali,” kinyume cha Katiba.

Ibara ya 63 (2) ya Katiba inaeleza wazi, kuwa “Bunge ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano chenye madaraka, kwa niaba ya wananchi, kusimamia na kuishauri serikali na vyombo vyake vyote katika kutekeleza majukumu yake.”

Lakini Bunge limekuwa likiibeba serikali hata katika maeneo ambayo haibebeki; na au ambako kila mmoja anaona serikali inabebwa.

Mathalani, ni katika sakata la wanafunzi 7,000 (elfu saba) wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), walioamriwa na serikali kurudi nyumbani.
Wabunge, bila kujali itikadi za vyama vyao, walisimama bungeni kutaka maelezo kutoka serikalini juu ya vijana hawa kufukuzwa katika maeneo ya chuo. Serikali ilibebwa na bunge.

Bunge lilitaka maelezo kutoka serikalini, kilichosababisha wanafunzi hawa kuamriwa kurudi nyumbani kwa “hati ya dharura.” Lilitaka kufahamu, wanarudishwa nyumbani kwa mazingira yapi?

Alikuwa Juma Nkamia, mbunge wa Chemba (CCM), aliyeanza kulitaka Bunge kusitisha shughuli zake ili lijadili “suala la dharura” linalohusu wanafunzi hao.

Alikataliwa na Naibu Spika kwa hoja kuwa amekosea vifungu vya kanuni.

Bali, Joshua Nassari, mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), alisimama na kutaja kanuni sahihi inayoruhusu Bunge kusitishwa ili kujadili jambo la dharura. Naye maombi yake yalitupwa.

Uamuzi huu haukuwafurahisha baadhi ya wabunge. Waliamua kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.

Hoja ilikuwa ikiwa miongozo yote miwili imekataliwa – ule wa Nkamia aliyekosea kanuni na ule wa Nassari aliyejielekeza kwenye kanuni – kanuni hizo za Bunge zimetungwa kwa ajili ya nini?

Nayo taasisi isiyokuwa ya kiserikali inayoitwa, Lumumba Alliance Club of Tanzania (LAC), ilijipa kazi ya kutetea Rais Magufuli.

Mahmoud Hussein, anayejiita mkuu wa kitengo cha fedha cha taasisi hiyo, alinukuliwa Agosti 2016 akisema, “wanasiasa wanaombeza Magufuli, ni hatari kwa usalama wa nchi.”

Mahmoud alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama nchini, kutopuuzia watu au taasisi zinazomkosoa au kumpinga rais. Akataka zichukuliwe hatua madhubuti za kuwadhibiti.

Hussein na tasisi yake, wamedai Rais Magufuli ameondoa rushwa serikalini; amerudisha nidhamu, amepambana na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka; na hivyo hastahili kupingwa wala kukosolewa.

Lakini hadi sasa, utetezi wake umeshindwa kufanya kazi. Umeishia kuibua madai mapya kila uchao – juu ya kuporomoka kwa uchumi na kuwapo kwa utawala unaokandamiza demokrasia.

Hivyo basi, ni vema serikali ingekiri mapungufu, kuliko kukana kila kitu. Hilo lingesaidia wananchi kufahamu kipi kimefanyika kwa ufasaha na kipi hakijafanyika.

Kitendo cha serikali kuendelea kukana hata kinachoonekana machoni mwa wananchi, ni kuidhalilisha serikali yenyewe.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 28 watumishi UDSM yaliwa na nzige, madumadu

Spread the loveGEORGE Francis anasikitika; anatembea akiwa na mawazo mengi, hajui la...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nimekumbuka Samia wa miaka 3 iliyopita

Spread the loveWAKATI naandaa makala ya safu hii wiki hii, nimejikuta nakumbuka...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Hakuna fedha za Rais

Spread the loveKUNA mambo machache mazuri ya kujifunza kutoka kwa Margaret Thatcher,...

error: Content is protected !!