Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Waliounga mkono juhudi, wabunge na wateule waanguka kura za maoni
Habari za SiasaTangulizi

Waliounga mkono juhudi, wabunge na wateule waanguka kura za maoni

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania kimehitimisha mchakato wa kura za maoni kwa wabunge wa majimbo nchini humo huku ikishuhudiwa wabunge wa chama hicho zaidi ya nane wakishindwa kuongoza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Pia, waliokuwa wabunge wa upinzani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Wananchi (CUF) zaidi ya saba waliojiuzulu na kuhamia CCM kuunga mkono juhudi za Serikali wakishindwa kutetea nafasi zao.

Wabunge hao baada ya kujiuzulu kwa nyakati tofauti, walipitishwa tena na CCM kugombea nafasi hizo na kushinda lakini katika kura za maoni zilizofanyika jana na kumalizika leo Jumanne tarehe 21 Julai 2020 wameangukia pua.

Hata hivyo, kuongoza au kushindwa kura hizo za maoni si mwisho kwani huo ni mchakato wa awali ambapo kuanzia tarehe 30 Julai 2020, kutakuwa na vikao vya kamati za siasa za jimbo kwa ajili ya kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo kwa kamati za siasa za mikoa.

Baadhi ya wabunge wa CCM walioangushwa katika kura hizo za maoni ni;

Mendrad Kigola wa Mufindi Kusini aliyepata kura 4 huku msindi wa kwanza David Kihonzile akiibuka mshindi kwa kura 216 kati ya kura 615 zilizopigwa. Mshindi wa pili Dickson Lutevele aliyepata kura 162.

Venance Mwamoto wa Kilolo aliambulia kura 47 huku akiongozwa na Justin Nyamoga kwa kura 209, kati ya kura 868 zilizopigwa. Mshindi wa pili ni, Briyan Kikoti kwa kura 180.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ameshindwa kura za maoni Jimbo la Kyela Mkoa wa Mbeya kwa kupata kura 252 dhidi ya mshindi Ally Mlagila Kinanasi aliyepata kura 502. Mshindi wa tatu ni Hunter Mwakifuna amepata kura 288.

Profesa Jumanne Maghembe amepata kura 130 Jimbo la Mwanza Mkoa wa Kilimanjaro huku Anania Tadayo akiongoza kwa kura 176 na Shabibu Mruma amepata kura 56 akiwa wa tatu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameongoza kura za maoni Kasulu Mjini Mkoa wa Kigoma kwa kupata kura 405 dhidi ya mbunge anayemaliza muda wake wa jimbo hilo, Daniel Nswanzugwako aliyepata kura 80.

Mbunge anayemaliza muda wake, Misungwi Mkoa wa Mwanza, Charles Kitwanga amepata kura 260 huku aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Manyara akiongoza kwa kura 406.

Mbunge wa zamani wa Mvomero Mkoa wa Morogoro, Amosi Makalla ameongoza kura za maoni kwa kupata kura 321 dhidi ya mbunge anayemaliza muda wake, Selemani Sadiq kura 231 na Jonas Van Zeland akishika nafasi ya tatu kwa kura 112.

Balozi Diodorus Kamala wa Jimbo la Nkenge anayetetea jimbo hilo amepata kura 24 huku Florent Kyombo akiongoza kwa kura 103 na mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Asumpta Mshama akipata kura 93.

Mbunge anayemaliza muda wake wa Mafia Mkoa wa Pwani, Mbaraka Dau ameshindwa kura za maoni jimboni humo kwa kupata kura 95 kati ya 261. Mshindi ni Omari Kipanga aliyepata kura 111.

Jimbo la Ileje Mkoa wa Songwe, mbunge anayemaliza muda wake, Janneth Mbene ameshindwa kuongoza kura za maoni kwa kupata kura 39 kati ya kura zote 651 Zilizopigwa.

Katika uchaguzi huo Wilman Ndile aliongoza kwa kupata kura 172.

Waziri wa zamani wa maliasili na utalii ambaye ni mbunge wa Msalala Mkoa wa Shinyanga anayemaliza muda wake, Ezekiel Maige ameshindwa kuongoza kura za maoni kwa kupata kura 118 dhidi yaIddi Kassim aliyepata kura 327.

Khatib Mgeja amekuwa wa tatu akipata kura 75.

WATEULE WA RAIS

Pia, katika kura hizo za maoni zimewashuhudia waliokuwa wateule wa Rais John Pombe Magufuli wakishindwa kuongoza kwenye kura hizo.

Baadhi yao ni; aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amepata kura 122 jimbo la Kigamboni huku Dk. Faustine Ndugulile anayetetea nafasi hiyo akipata kura 190.

Aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amekuwa wa pili jimbo la Ilala kwa kupata kura 103 dhidi ya aliyeongoza Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Azzan Zungu aliyepata kura 148.

Patrobas Katambi, alikuwa mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini yeye alikwenda kugombea Jimbo la Shinyanga Mjini ambapo amepata kura 12  akiwa nafasi ya saba dhidi ya mbunge anayemaliza muda wake, Stephen Maselle aliongoza kwa kura 152.

Aliyeshika nafasi ya pili ni; Jonathan Manyama Ifunda kura 65 huku Gasper Kileo akishika nafasi ya tatu kwa kura 51.

Aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, David Kafulila amekuwa wanne Jimbo la Kigoma Kusini akipata kura 64.

Kati ya mwaka 2010-2015, Kafulila alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia NCCR-Mageuzi ambapo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, alishindwa na Hasna Mwilima wa CCM.

Mwaka 2016, Kafulila alihamia Chadema na mwaka 2012 akatangaza kuhamia CCM ambapo mwaka 2018, Rais Magufuli alimteua kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe.

Katika kura hizo za maoni, Mwilima ameongoza kwa kura 273 akifuatiwa na Nashon Bidyanguze kwa kura 143 na January Kizito akipata kura 117 nafasi ya tatu.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, Kippi Warioba yeye amepata kura kura za jimbo la Kawe, Dar es Salaam kwa kupata kura tatu kati ya 475.

Aliyeongoza ni Furaha Jacob aliyepata kura 101 akifuatiwa na Angela Kiziga kura 85 na wa tatu, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kura 79.

WALIOUNGA MKONO JUHUDI

Baadhi ya waliokuwa wabunge wa upinzani na kuhamia CCM ni, David Silinde wa Momba kupitia Chadema ambaye yeye ametia nia jimbo la Tunduma Mkoa wa Songwe kupitia CCM.

Katika kura za maoni, Silinde amepata kura 118 dhidi ya Aden Mwakyonde aliyeongoza kwa kupata kura 250, akifuatiwa na Daniel Sichalwe aliyepata kura 20.

Zuberi Kuchauka aliyekuwa CUF jimbo la Liwale kasha kuhamia CCM na kugombea tena ambapo alishinda, kwenye kura za maoni amekuwa wa tatu akipata kura 71 dhidi ya Faith Mitambo aliyeongoza kwa kura 363 na Halifa Kajukila akishika nafasi ya tatu kwa kura 48.

Abdallah Mtolea wa Jimbo la Temeke na Maulid Mtulia wa Kinondoni zote walikuwa CUF na kuhamia CCM ambapo wote kwenye kura za maoni wameshindwa kuongoza.

Abbas Tarime ameongoza Kinondoni kwa kura 171 akifuatiwa na Iddi Azzan aliyepata kura 77 na Mtulia akipata kura 11.

Dk. Vincent Mashinji

Mtolea yeye amejikuta akipata kura 22 na aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo la Temeke, Abbas Mtemvu akiongoza kwa kura 203 kati ya 367.

Aliyekuwa mbunge wa Arumeru Mashariki kupitia Chadema, Joshua Nassari ambaye amejiunga na CCM hivi karibuni, amejikuta akipata kura 23 nafasi ya nne.

Aliyeongoza ni mbunge wa sasa anayemaliza muda wake, Dk. John Pallagyo aliyepata kura 536 akifuatiliwa Dan Pallagyo kura 63.

Wengine waliopata kura chini ya kumi jimbo la Arusha Mjini ni; Samson Mwigamba na Wakili Albert Msando ambao walijiunga na CCM wakitoka ACT-Wazalendo.

Meya wa zamani wa Arusha, Kalist Lazaro aliyejiuzulu umeya na kujiunga CCM alipata kura moja Arusha Mjini huku aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji akipata kura mbili Jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam.

Mbunge anayemaliza muda wake, Julius Kalanga wa Monduli ambaye awali alikuwa Chadema kasha kurejea CCM amepata kura 162 dhidi ya Fredrick, mtoto wa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyeongoza kura za maoni kwa kupata kura 244.

Peter Lijualikali wa Kilombero Mkoa wa Morogoro aliyekuwa Chadema akahamia CCM na Katani Ahmed Katani wa Tandahimba Mkoa wa Mtwara kupitia CUF wote wameshindwa kuongoza maeneo yao wakipata kura chini ya 20.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online na MwanaHALISI TV kwa habari zaidi

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

Habari za Siasa

CCM yakemea ufisadi, yaipa kibarua TAKUKURU

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekemea vitendo vya ubadhirifu wa...

Habari za Siasa

Bajeti ya Ikulu 2024/25 kuongezeka, bunge laombwa kurudhia Sh. 1.1 trilioni

Spread the love  WIZARA ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa...

error: Content is protected !!