IDADI ya miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere iliyotokea jana tarehe 20 Septemba 2018 imeongezeka kutoka watu 79 hadi 136. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Idadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro wakati akizungumza na wanahabari.
Jana tarehe 20 Septemba 2018 siku ambayo ajali hiyo ilitokea majira ya mchana, miili ya watu takribani 44 iliokolewa kutoka Ziwa Victoria, huku watu 37 walifanikiwa kuokolewa wakiwa hai.
Zoezi la ukoaji wa miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo linaendelea kufanywa na Vikosi Maalum vya uokoaji vya Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Watanzania (JWTZ) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Sirro amesema watafungua jalada la uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini ukweli wa ajali hiyo ikiwemo chanzo chake.
Baada ya kutokea ajali hiyo, kumekuwepo na tofauti ya idadi ya abiria waliokuwemo kwenye kivuko hicho, huku kukiwepo madai ya kwamba kivuko hicho kilibeba zaidi ya abiria 200, idadi iliyo kubwa ukilinganisha na uwezo wa kivuko hicho wa kubeba abiria wasiozidi 100.
Kivuko cha MV Nyerere kilizama katika Ziwa Victori kikitokea Bugorora kisiwani Ukerewe kuelekea Kisiwa cha Ukara.
Leave a comment