Wahariri Tanzania wataka uwazi wa CCM uhamie NEC, Mahakama na Bunge

Spread the love

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limetoa pongezi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuruhusu kurushwa moja kwa moja (live) kwenye vyombo vya habari, mikutano yake huku ikitoa ushauri kwa maeneno mengine kama Bunge, Mahakama na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuiga mfano huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea)

CCM ilifanya mikutano miwili, wa Halmashauri Kuu (NEC) tarehe 10 Julai 2020 uliokuwa na ajenga mbalimbali ikiwemo kumchangua mgombea urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 pamoja na kumpitisha Dk. John Pombe Magufuli kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mara ya kwanza, mkutano huo wa NEC ulirushwa moja kwa moja ‘live’ na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo tukio la uhesabuji wa kura ambapo Dk. Hussein Ali Mwinyi aliibuka mshindi kwa kupata kura 129 sawa na asilimia 78.65, Shamsi Vuai Nahodha kura 16 na Dk. Khalid Salum Muhamed akipata kura 19.

Pia, mkutano mkuu uliofanyika tarehe 11 Julai 2020, nao ulirushwa moja kwa moja na vituo mbalimbali vya habari.

Jana Jumapili tarehe 12 Julai 2020, TEF ilitoa taarifa kupitia kwa Deodatus Balile, Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa hiulo ikipongeza uamuzi huo wa CCM.

“Tumefarijika zaidi kwa waandishi wa habari kuruhusiwa kuwamo ndani ya ukumbi wa mkutano tangu mwanzo wa mkutano hadi ulipofungwa,” alisema Balile

“Kadhalika, tumevutiwa na utaratibu mpya na wa aina yake, ambao umewezesha kura za wagombea urais ndani ya CCM kwa Zanzibar na Muungano kuhesabiwa ‘live’ huku vyombo vya habari vikishuhudia.”

Alisema, hii ni hatua inayoongeza uwazi na kuziba mianya ya malalamiko.

“Hakuna anayeweza kulalamika au kuwa na mashaka kuhusu kura za mgombea Urais wa Zanzibar, kwani wafuatiliaji wa matangazo ya moja kwa moja walioko ndani na nje ya nchi, walishuhudia jinsi washindani walivyokuwa wakikabidhiwa kura zao kadri zilivyokuwa zinahesabiwa.”

“Hatua hii imeondoa uwezekano wa kutiliwa shaka uteuzi wa mgombea urais wa CCM Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi. Sisi Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) tunaamini utaratibu huu umefuta mianya ya mtu/watu kulalamika kuwa huenda kura zake/zao ‘zilichezewa.’” Alisema Balile

TEF ilisema, vivyo hivyo kwa kura za mgombea urais wa Muungano kupitia CCM, zamu hii ilipotangazwa kuwa amepata asilimia 100, pia hakukuwa na mashaka kwani vyombo vya habari vilishiriki hatua zote kuwahabarisha wananchi mchakato huo wa uteuzi.

Ilisema, kila aliyefuatilia anakuwa kwenye nafasi ya kukiri uhalisia wa mambo yalivyokuwa na kuondoa dhana iliyokuwapo awali kuhusu kile kilichowahi kubatizwa jina la kura za ‘itifaki’.

“Ni ushauri wetu kwamba utaratibu huu wa CCM ambacho ni chama tawala, uhamie kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Mahakamani na Bungeni, kwani mambo wanayojadili ni kwa maslahi ya taifa letu wa watu wake,” alisema

“Vyombo vya habari vikiwa mshirika mkubwa katika kuimarisha amani, usalama na kukuza uchumi kwa kusukuma maendeleo ya nchi, vinatekeleza wajibu wake huo vyema zaidi pale vinapopata fursa za kuripoti uhalisi wa mambo,” alisema Balile kwenye taarifa hiyo

Deudatus Balile, Kaimu M/kiti TEF

Alisema, vyombo hivi vinapoanika ukweli kwa mtindo huu, hata wanaopinga au wenye nia na malengo ya kupotosha hushindwa kwa kuona aibu. Kimsingi, ukweli hufuta fitina.

“Tunaomba sasa CCM ihamishie uwazi wa aina hii serikalini kwa kuruhusu Sheria ya Haki ya Kupata Habari ya Mwaka 2015 ifanye kazi vyema na wananchi waitumie fursa hiyo kusema ukweli badala ya kubanwa kila kona hali ambayo huwasukuma baadhi yao kusambaza majungu kupitia kwenye mitandao ya kijamii,” alisema

Balile alisema, “TEF tunasema, hongera Rais John Magufuli, Mwenyekiti wa CCM kwa uamuzi huu na hongera Dk. Hussein Ally Mwinyi kwa kuteuliwa na chama chenu, hivyo nyote kuwa wagombea kwa nafasi ya urais wa Muungano na Zanzibar sawia.”

“Tunaamini kama mlivyowaasa washindani wenu waendeshe kampeni za kistraabu, basi nanyi mtaendesha kampeni za kistaabu, na kukubali matokeo kwa njia ya kura za wazi (live) katika ngazi ya urais, ubunge na udiwani kama tulivyoshuhudia katika mikutano yenu,” alisema

About Kelvin Mwaipungu

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!