January 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wagombea urais Chadema wabanwa mbavu

Spread the love

WAJUMBE wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamewabana watia nia wa urais kupitia chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema; Dk. Mayrose Majinge na Lazaro Nyalandu ni watia nia waliopenya katika tatu bora, ambapo leo Jumatatu tarehe 3 Agosti 2020, wamejinadi mbele ya wajumbe hao.

Mjumbe mmoja wa mkutano huo amemuuliza Nyalandu kwamba, atachukua hatua gani endapo atatoswa katika kinyang’anyiro hicho.

Akijibu swali hilo, Nyalandu amesema atakuwa tayari kushirikiana na mgombea yeyote atakayeteuliwa na Chadema kupeperusha bendera yake kwenye Uchaguzi wa Urais wa Tanzania.

“Nilipokuja Chadema, nilibatilisha kiapo nilichoapa nikiwa CCM chipukizi na kuapa kuilinda Chadema. Kwa vyovyote vile, mgombea yeyote, atakayeteuliwa na chama chetu, nitashirikiana naye si yeye bali chama ili tushinde madiwani, ubunge na urais,” amesema Nyalandu.

Awali, akijinadi mbele ya wajumbe hao Nyalandu aliwahakikishia kwamba, yuko tayari kufanya kampeni nchi nzima huku akila kiapo kwamba hatarudi CCM.

“Sitarudi tena CCM nilipotoka kwa kuwa nilikua sioni, lakini sasa naona, ni azma yangu na kusudio langu kushirikana na wanachama wa chama chetu ili tushinde.

“Nipo tayari na nimejiandaa niende katika majimbo manne kwa siku, ili tuweze kuyamaliza nchi nzima kwa kuyafikia kila jimbo hadi mwisho wa kampeni,” amesema Nyalandu.

Dk. Mayrose aliulizwa na mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, kwamba amejipanga vipi kukabiliana na rafu za kisiasa katika uchaguzi huo, ikiwemo wizi wa kura.

Akijibu swlai hilo, Dk. Mayrose amesema, ameandaa mikakati itakayofanya Chadema itangazwe mshindi kwenye uchaguzi huo.

“Nimefanya mikakati kuhakikisha tunatangazwa kwasababu tunatosha, tuna mambo ya msingi ya kueleta haki na binadamu anayahitaji na mwisho zaidi ni demokrasia ya ukombozi wa taifa inayopatikana mwaka huu 2020,” amejibu Dk. Mayrose.

Lissu aliulizwa na mjumbe wa baraza hilo kwamba, kesi alizo nazo mahakamani hazitomkosesha sifa za kugombea Urais wa Tanzania.

Akijibu swali hilo Lissu amesema, madai hayo hayana mantiki kwa kuwa yanalenga kujenga hofu.

“Wanawajazeni hofu tu, afungwi mtu hapa, mnafahamu maneno yangu kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Tanzania ninazofahamu mie, kesi ya uchochezi hata ukifungwa nayo haikufutii sifa ya kuchaguliwa rais wa Tanzania,” amesema Lissu na kuongeza:

“Hiyo kwamba, umefungwa itakuwa rahisi waulizeni mapolisi joto ya jiwe wanayopata wakiingia kwenye kumi na nane zangu, msijazwe hofu kuna vijineno vya kuwakatisheni tamaa, hakuna hoja ya kikatiba au sheria inayoweza kuninyanganya sifa za kugomeba urais mwaka huu hakuna.”

error: Content is protected !!