Wadaiwa sugu kodi ardhi watahadhalishwa – MwanaHALISI Online
William Lukuvi, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
William Lukuvi, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Wadaiwa sugu kodi ardhi watahadhalishwa

WADAIWA sugu wa kodi ya ardhi Kanda ya Ziwa wametahadharishwa kulipa mapema madeni yao wanayodaiwa kwa kipindi kirefu kabla ya Juni 30, mwaka huu, anaandika Moses Mseti.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake mkoani Mwanza, Joseph Shewiyo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa, amesema kuwa kama hawatafanya hivyo hatua nyingine za kutaifisha mali zao zitafanyika mara moja.

“Tunaendelea kutekeleza na kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwafikia wadaiwa na kuwatumia ilani zenye nakala za kodi wanayodaiwa tayari kuna wengine wamelipa wale ambao hawakulipa tumewafikisha mahakamani.

“Tunadai kodi kwa mujibu wa sheria na ina utaratibu wake, halmashauri zote za Kanda ya ziwa zinaendelea na juhudi mbalimbali ikiwemo kuhakikisha wote wanaodaiwa wanalipa, ambao hawajaingizwa kwenye mfumo wa malipo wanaingizwa na kupewa kiasi cha kodi wanayotakiwa kulipa…kodi yetu inatozwa kulingana na ardhi, thamani ya ardhi, mahali ilipo, ukubwa na matumizi yake,” amesema Shewiyo.

Kamishna Shewiyo, amesema kwa kipindi cha Mei mwaka huu jumla ya watu 310 waliofanyiwa uhakiki mkoani Mwanza na walifikishwa mahakamni, kati ya hao wamiliki wa ardhi waliojitokeza mahakamani ni 156, ambao hawakujitokeza ni 154 na waliolipa ni 102, huku akidai maeneo mengine ni Musoma watu 210 na Bukoba watu 300.

Hata hivyo, Shewiyo amesema watu 310 waliofikishwa mahakamani walikuwa wanadaiwa zaidi ya Sh bilioni 2 na kwamba hatua hizo zimeweza kukomboa kiasi cha fedha Bilioni 1.9 ambazo kimelipwa na zimeshapelekwa serikalini na kwamba wananchi wameitikia wito vizuri.

Mushi Meshack, Mmoja wa wakazi wa Jiji la Mwanza, akizungumzia utekelezaji wa agizo hilo amesema wananchi wengi hasa wa maeneo ya pembezoni mwa mji hawajapata elimu ya kodi hiyo na kuiomba Serikali kusitisha kwanza tozo ili kutoa elimu kwa wananchi.

“Kwa mfano mimi hili suala ndiyo nalisikia leo, wengi hatuna elimu kabisa hasa tuliopo nje ya miji kwahiyo inabidi kwanza watoe elimu iwafikie watu wengi ndipo waangalie namna ya kutoza faini kwa watakaokaidi,” amesema.

Mei 27, mwaka huu Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa ilianika majina 157 ya wadaiwa wa kodi ya ardhi mkoa wa Mwanza wakiwamo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, marehemu Liberatus Barlow, mfanyabiashara Jumanne Mahende, aliyekuwa Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mwanza, Respick Ndowo, Taasisi na mashirika ya umma ikiwemo Tanesco, TRL, Bakwata, Chama kikuu cha ushirika Nyanza (NCU) na benki ya NBC tawi la Mwanza wakitakiwa kufika mbele ya baraza la  ardhi na nyumba la mkoa huo kutokana na kutolipa kodi.

Hivi Karibuni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliwataka wamiliki wote wa viwanja na mashamba yaliyopimwa ambao hawajalipa kodi hiyo kuhakikisha wanalipa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, mwaka huu ili wasichukuliwe hatua mbalimbali za kisheria ikiwemo kushtakiwa mahakamni, mali zao kupigwa mnada na kufutiwa miliki zao.

WADAIWA sugu wa kodi ya ardhi Kanda ya Ziwa wametahadharishwa kulipa mapema madeni yao wanayodaiwa kwa kipindi kirefu kabla ya Juni 30, mwaka huu, anaandika Moses Mseti. Akizungumza na wanahabari ofisini kwake mkoani Mwanza, Joseph Shewiyo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa, amesema kuwa kama hawatafanya hivyo hatua nyingine za kutaifisha mali zao zitafanyika mara moja. “Tunaendelea kutekeleza na kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwafikia wadaiwa na kuwatumia ilani zenye nakala za kodi wanayodaiwa tayari kuna wengine wamelipa wale ambao hawakulipa tumewafikisha mahakamani. “Tunadai kodi kwa mujibu wa sheria na ina utaratibu wake, halmashauri zote za Kanda ya ziwa zinaendelea…

Review Overview

User Rating: Be the first one !
0

About Moses Mseti

Visit Us On FacebookVisit Us On TwitterVisit Us On Youtube