Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene akijibu hoja mbalimbali za wizara yake

Wabunge waungana wasusia miswada, Simbachawene azomewa

BILA kujali itikadi za vyama vyao vya siasa wabunge wameitaka Serikali kuondoa bungeni miswada mitatu ya Sheria ya Petroli, Muswada wa Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa mwaka 2015 na Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika taasisi za uchimbaji Tanzania wa Mwaka 2015. Anandika Dany Tibason … (endelea).

Mbali na wabunge hao kuikataa miswada hiyo Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene alijikuta katika wakati mgumu wa kuzomewa na wabunge pale ambapo alionekana kutaka kutetea miswada hiyo ijadiliwe bungeni.

Mbali na Simbachawene kuzomewa naye Naibu wa Nishati na Madini, Charles Mwijage nusura amrushie makonde Mbunge wa Igunga, Dk. Dalal Kafumu baada ya kupinga mswada huo kwa madai hauna tofauti na sheria za Uganda yaani “Copy and Paste” isipokuwa limeondolewa neno Uganda tu.

Baada Dk. Kafumu kutoa kauli hiyo Mwijage alionekana kukerwa na jambo hilo na kunyanyuka katika kiti chake bila kupewa ruhusa na mwenyekiti wa kikao huku akiwa anafoka na kurusha mikono kwa jazba.

Wiki iliyopita Bunge lilielezwa kuwa Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi, una lengo la kutekeleza Sera ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi ambao dhumuni lake kuu ni kuhakikisha kwamba mapato yatokanayo na tasnia ya mafuta na gesi yanakusanywa na kutumiwa katika namna ambayo haihatarishi uimara wa kiuchumi wa nchi.

Mfuko wa mapato yatokanayo na Mafuta na Gesi, unapendekeza kuanzishwa kwa madhumuni ya kupokea na kugawa mapato yatokanayo na mafuta na Gesi kwa kuzingatia malengo makubwa matatu ambayo ni kuhakikisha uimara wa kifedha na kiuchumi, kugharamia masuala ya uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, kuimarisha maendeleo ya kijamii na kulinda rasilimalikwa ajili ya vizazi vijavyo.

Akiwa wakwanza kuchangia, Mbunge Singida Mashariki Tundu Lissu (Chadema), amesema ni bora wabunge wote wakarejea katika historia ya nchi kwa kupitisha miswada kwa hati ya dharura ambapo miswada miwili iliwasilishwa Machi mwaka 1997 ambayo ni muswada wa kuondoa kodi na uwekezaji ambao kwa sasa unawaumiza watanzania.

Amesema jambo la kusikitisha ni pale ambapo muswada huo kifungu cha 261 ambacho kinaanisha kuwa hakutakuwa na haki ya kuhoji mikataba ya zamani.

Nae Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge(CCM), ambaye aliwahi kuwa mwanasheria mkuu wa serikali katika awamu ya tatu amesema miswada hiyo inahitaji muda ili kujadiliwa kwa kina kwani kinyume na hivyo Serikali haiwezi kufaidika hata kidogo.

Chenge amesema wataalumu wanawajibu kutoa taarifa kuhusu ni mapungufu yapi kwa sheria ya awali ya miaka 1980 na sio kukimbilia kuja na miswada mipya ambayo inaonekana kuwa haikidhi hitaji.

Kwa upande wake Mbunge wa Ubungo ,John Mnyika(Chadema) akichangia amesema iwapo miswada hiyo itapita ni dhahiri kuwa kuna nguvu ya uongozi na sio utashi wa wabunge hivyo hauna sifa ya kuwasilishwa.

Mbunge huyo amesema ni lazima wabunge wakawa na mawazo ya kufikiria vizazi vijavyo badala ya kufikilia uchaguzi zaidi.Aidha, amesema kuna uwezekano mkubwa serikali ikawa na msukumo wa Benki ya Dunia WB na misukumo mingine kama hiyo na inawezekana kuna miswada mingine mibovu ambayo imeisha sahiniwa.

“Kinachoonekana ni kile kinachodaiwa kuwa kuna msukumo wa MCC, WB na kuwa Rais anataka upite ili aonekane kuwa ameshiriki kuandaa sheria hiyo”amesema Mnyika.

Akichangia katika semina hiyo Mbunge wa Viti Maalum CCM, Dk. Mary Mwajelwa amesema Serikali iweke bajana kuwa ni kitu gani kinasukuma muswada huo kuletwa kwa dharura wakati ni jambo kubwa lenye maslahi kwa Taifa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti naomba Serikali iachane na muswada huo kwani elimu haijatolewa lakini pia wabunge kiakili hawapo hapa akili zipo majimboni,” amesema

Mbunge wa Wawi, Hamad Mohamed Rashid amesema haipo sababu ya Serikali kulazimisha suala hilo kwani kwa sasa akili za wabunge hazipo hapa Bungeni.

Naye mbunge wa Ole,Rajab Mohamed Mbarouk (CUF), amesema hakuna sababu yoyote ya miswada hiyo kuihusisha serikali na Zanzibar kwani mpaka sasa Zanzibar imeisha jipanga katika suala la uchimbaji wa mafuta.

“Hata juzi wakati Rais anavunja baraza la Wawakilishi amesema Zanzibar katika uchimbaji wa mafuta na gesi tutatumia sheria zetu na wala si la kujadiliwa hivyo nashangaa kuona ninyi mnaliweka katika mambo ya muungano toeni Zanzibar bakisha Tanzania” amesema Mbarouk.

Akichangia miswada hiyo Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), amesema miswada hiyo imewapa changamoto wabunge ila ni vema ikaahirishwa ili kusubiri utulivu wa wabunge.

Kwa upande wake wa Mbunge wa Nzega Dk. Khamis Kigwangalla amesema kutokana na taratibu za kupitisha miswada hiyo ni lazima wabunge wawepo ili wapate muda wa kujadili suala hilo.

Mbunge wa Igunga, Dk. Dalaly Kafumu (CCM), aliitaka Serikali isiiwasilishe katika Bunge linaloendelea kwa kile alichosema kuwa haikuandaliwa katika mazingira yanayokubalika pia mswaada huo umekopiwa kutoka Uganda na haujafanya kazi vizuri.

“Sheria hii ya petrol haifai kabisa kwa sababu ina kasoro nyingi na ‘imekopiwa’ kutoka sheria ya Uganda ambayo nimeichukua kwenye mtandao ila hata kushirikishwa hatujashirikishwa ndio mimi nauona hapa,” amesema.

“Jamani kwa maslahi ya Watanzania hii sheria kwa maoni yangu, naomba isiwasilishwe katika Bunge hili ili upatikane muda wa kuiandaa vinginevyo italiangamiza taifa ambalo linategemea eneo hilo kwa sasa,” amesema Dk. Kafumu.

Amesema iwapo nchi inatakiwa kupiga hatua inahitajika kuwepo kwa misingi sahihi ya kuandaa sheria ambazo zinatija kwa jamii kinyume na hivyo ni dhahiri kizazi kijacho kitaangamia.

Kafumu amesema ni wazi gesi inahitajika lakini itakuwa haina maana iwapo sheria itakuwa na mapungufu mengi ambayo yanaweza kurekebishika.

Mbunge huyo ambae ni Kamishna wa madini amesema rasilimali za mafuta, madini na gesi ni rasilimali za dunia hivyo ni vyema kuweka masharti ambayo yanakubalika kidunia ili wawekezaji waweze kushiriki.

“Unajua sheria hii pamoja na kuwa na maeneo mazuri ila inaipa mapungufu mengi mfano kitendo cha Kampuni ya Mafuta ya Taifa (TPDC), kwa kupata asilimia 25 ya hisa kwa kila kampuni ila lingine ambalo ni la ajabu ni kuwa kampuni za uwekezaji zikipata gesi ni lazima muuzaji awe TPDC hii haiwezekani,” amesema.

Amesema iwapo hakutakuwa na mabadiliko ni dhahiri kuwa wawekezaji watashindwa kuja kuwekeza kwani wataamini kuwa rasilimali hioyo ni mali ya Serikali jambo ambalo halipo katika ulimwengu wa sasa.

Kwa upande wake Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), aliishangaa Serikali kwa kile alichosema kuwa haoni sababu za kuiwasilisha bungeni miswada hiyo kwa hati ya dharura.

Kutokana na hali hiyo, amesema mpango huo uahirishwe kwa kuwa wabunge wengi hawako tayari kuizungumzia kwa kuwa akili zao zinafikiria majimbo yao ya uchaguzi.

Akitoa ufafanuzi wa Muswada wa Sheria ya Petroli, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amesema kuna umuhimu wa kuipitisha kwa kuwa sheria za mwaka 1980 na ya mwaka 2008, zinatoa mwanya kwa taifa kutonufaika na gesi na mafuta kwa kuwa zilitungwa wakati ambao Tanzania haikuwa na nishati hiyo.

Akizungumzia maoni ya wabunge Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene, amesema miswada hiyo ni mizuri ila kuna dalili za watu kupanga mkakati wa kuukwamisha kwa maslahi yao.

Simbachawene amesema miswada hiyo ingeweza kuleta tija kwa Taifa ila anashangaa kuona viongozi wanatumia nafasi zao kukwamisha jambo ambalo hawatendei haki wananchi.

Waziri huyo alijikuta akimshutumu Mbunge wa Igunga Dk, Kafumu kuwa yeye alihusika katika mikataba ya madini ambayo leo inaligharimu Taifa.

“Najua huu ni mpango ambao unafanywa na watu baadhi, nashindwa kuelewa ni kwanini wanapinga ambapo mchangiaji mmoja alikuwa kamshina wa madini na kutuingiza kwenye mikataba mibaya kwa Taaifa,” amesema.

Akihitimisha mjadala huo Mwenyekiti wa Kamati Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa CCM amesema kimsingi amepokea michango ya wabunge ambapo asilimia kubwa waliochangia wameonesha dhahiri kutaka miswada hii isubiri bunge lijalo.

Aidha, amesema yeye amefanya kazi yake na atawasilisha Spika ili aweze kuchukua uamuzi ambao unastahili kwani ndiye mwenye mamlaka.

“Unajua waheshimiwa sauala hili ni zito lakini ni muhimu muswaada huo upite halafu bunge lijalo litafanyia marekebisho ambayo yanahitajika,” alimalizia Ndassa.

Miswada hiyo imekuwa ikipingwa na wabunge pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya mafuta na gesi

BILA kujali itikadi za vyama vyao vya siasa wabunge wameitaka Serikali kuondoa bungeni miswada mitatu ya Sheria ya Petroli, Muswada wa Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa mwaka 2015 na Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika taasisi za uchimbaji Tanzania wa Mwaka 2015. Anandika Dany Tibason … (endelea). Mbali na wabunge hao kuikataa miswada hiyo Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene alijikuta katika wakati mgumu wa kuzomewa na wabunge pale ambapo alionekana kutaka kutetea miswada hiyo ijadiliwe bungeni. Mbali na Simbachawene kuzomewa naye Naibu wa Nishati na Madini, Charles Mwijage nusura amrushie makonde Mbunge wa…

Review Overview

User Rating: Be the first one !
0

About Dany Tibason

Visit Us On FacebookVisit Us On TwitterVisit Us On Youtube