Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge waliofukuzwa Chadema watema nyongo 
Habari za Siasa

Wabunge waliofukuzwa Chadema watema nyongo 

Anthony Komu, Naibu katibu Mkuu NCCR- Mageuzi
Spread the love

WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, waliovuliwa uanachama wa chama hicho, wamekosoa uamuzi wa kufukuzwa wakisema haukuzingatia misingi ya haki. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).

Wabunge waliofukuzwa na majimbo yao kwenye mabano ni, Anthony Komu (Moshi Vijijini), Joseph Selasini (Rombo), David Silinde (Momba) na Wilfred Lwakakatare (Bukoba Mjini).

Uamuzi wa kuwafukuza wabunge hao ulitolewa jana Jumatatu tarehe 11 Mei 2020 na John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema, wakati akitoa maazimio ya kikao cha kamati kuu ya chama hicho kilichofanyika tarehe 9-10 Mei kwa njia ya mtandao.

Chadema ilifikia uamuzi huo baada ya kuwatuhumu wabunge hao kwenda kinyume na miongozo ya chama hicho ikiwamo maagizo ya kuwataka wabunge wake wote kukaa karantini kwa siku 14 ili kuangalia kama wana maambukizo ya COVID-19 au la.

Maagizo hayo yaliyolewa tarehe 1 Mei 2020 na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema.

Hata hivyo, wabunge 15 wakiwamo hao wane waliofukuzwa walikaidi maagizo hayo na kuendelea kuhudhuria vikao vya Bunge la bajeti vinavyoendelea jijini Dodoma.

Baada ya Chadema kuwafukuzwa, wabunge wao walizungumzia uamuzi huo ambapo, Lwakatare amesema anaamini hajatendewa haki na kwamba anasubiri barua ya kutimuliwa.

Amesema, ipo haki ambayo Chadema wameikiuka katika kufikia uamuzi wake, walipaswa kumuhoji kwa kile walichokiita tuhuma dhidi yake.

“Kwa manufaa ya chama, ningependezewa japo sina haki ya kuchagua adhabu ya kupewa lakini kwa mustakabali mzuri wa chama kilichokuwa changu, ilikuwa ni busara wangenipa hata siku au hata siku walioamua kunioji hapahapa Dodoma kupitia video conference,” amesema Lwakatare

“Wangepata picha ya upande wa pili ili kupata picha kutoka upande wa pili, badala ya kusikiliza upande mmoja na wakaamua. Mimi nafikiri bado hawajanitendea haki,” ameongeza Lwakatare ambaye alikwisha kutangaza kutogombea tena ubunge

Naye Komu amesema, hukumu iliyotolewa kwake ni kubwa na kwamba haki ya kusikiliza kabla ya chama kufikia uamuzi wake, ilirukwa.

“Ili ufanyiwe hukumu kubwa namna hiyo, ni lazima natural justice (haki ya kusikilizwa) izingatiwe kwamba upewe haki ya kusikilizwa.

“Nitashangaa kama ni kweli nimevuliwa uanachama, kwa hiyo nasubiri hiyo barua ili nione mazingira ambayo yamepelekea mimi kuvuliwa uanachama na baada ya hapo ndipo ninaweza nikachukua hatua,” amesema Komu

Hata hivyo, uamuzi huo dhidi ya Komu na Selasini unaweza usiwasumbue kwani walikwisha kutangaza kujiunga na MNCCR- Mageuzi mara tu Bunge litakapovunjwa.

Kwa upande wake, Silinde ameeleza kushangazwa na hatua zilizochukuliwa na Chadema akisitiza kuwa, maslahi ya wana Momba hayapaswi kuwa chini ya mtu mmoja.

Amesema, haoni kosa kwake kuingia bungeni na kuwawakilisha wananchi kama ambavyo walimtuma, na kwamba anabiri barua hiyo ifike mikononi mwake kisha aamue nini cha kufanya.

“Ni jambo la kushangaza eti leo maslahi ya wananchi wa Momba, yaani kuwatetea wananchi wake ndio ionekane kosa kuliko kufuata kauli ya Mbowe.”

“Kwa kweli hiki kitakuwa kitu cha kushangaza, mimi niwaambie kabisa kwamba nasubiri hiyo barua, nitakapoipata nitazungumza juu ya mustakabali wangu wa kisiasa baada ya hapo,” amesema.

Mbali na wabunge hao kutimuliwa, wabunge wengine 11 wametakiwa kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua akiwamo Mriam Msabaha (Viti Maalum), ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema aliyevuliwa nyadhifa zake zote na kubaki na ubunge pekee.

Wabunge wengine ni; Susan Maselle , Joyce Sokombi, Rose Kamili, Latifa Chande, Lucy Mlowe, Lucia Mlowe, Lucy Magereli na Dk Sware Semesi (wote Viti Maalumu).

Wengine ni; Willy Qambalo (Karatu), Peter Lijualikali (Kilombero) na Japhary Michael (Moshi Mjini).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!