Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge wa Viti Maalum Chadema, waanza kuondoka 
Habari za Siasa

Wabunge wa Viti Maalum Chadema, waanza kuondoka 

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepata pigo jingine, kufuatia hatua ya wabunge wake wawili, Suzana Maselle (Mwanza) na Joyce Sokombi (Mara), kutangaza kuondoka kwenye chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

“Tumeamua kuondoka Chadema, mara baada ya kumaliza kipindi chetu cha ubunge, Juni mwaka huu,” ameeleza Masele, mbele ya waandishi wa habari, leo Ijumaa, mjini Dodoma.

Amesema, uamuzi wao wa kuondoka Chadema, umetokana na chama hicho, kutawaliwa na ubinafsi, matumizi mabaya ya rasimali za chama na ubabe wa kiongozi mkuu wa chama hicho.

Wabunge wote wawili – Maselle na Sokombi, wameomba kujiunga na chama cha NCCR- Mageuzi, ambacho katika siku za karibuni, kimekuwa kama kimbilio na wanasiasa wengi wanaotoka Chadema.

Amesema, Chadema kimekuwa kwa kasi kubwa kutokana na kuungwa na wananchi wengi kutokana na kazi nzuri iliyokuwa inafanywa bungeni na wabunge wake katika vita dhidi ya ubadhirifu na ufisadi.

Amesema, hata wao walivutika kuingia bungeni ili waweze kuwa sehemu ya hao askari waliomstari wa mbele kwenye mapambano hayo.

“Tulipofika bungeni tulikuta hali ni tofauti sana.  Uongozi wetu yaani KUB haukutoa fursa hiyo kwetu; badala yake, alikuwa na wateule wake wachache ambao hao ndio waliaminika zaidi na ndio waliopewa kila fursa ya kuiwakilisha kambi,” ameeleza.

Kutokana na hali hiyo, Maselle amesema, “sisi tulijikuta tukiwa wasindikizaji na wasikilizaji zaidi. Tulivumilia. Tukijua kuwa ni muhimu kuendeleza umoja wetu na pili kujifunza na kila tulipopata fursa tulionyesha uwezo wetu na kubainisha malalamiko yetu.

Amesema, “maoni ya kutokuridhishwa na hali kama hiyo, yalitufanywa tutengwe na kupuuzwa zaidi.  Pamoja na yote hayo michango iliyotolewa na hao wateule mingi ni vijembe ambavyo vilituondoa kwa kiwango kikubwa kwenye agenda yetu.”

Anasema, “hali hii imekuwa mbaya zaidi baada ya Esther Bulaya, kuteuliwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi yetu na kujipa mamlaka yaliyopitiliza.

“Kabla ya hapo, palikuwepo na kafursa kakuulizwa na kujipendekeza. Wakati huu, ni amri tu. Kwa  kifupi, maamuzi mengi ni ya kibabe na yenye kudharau watu wengine, na kwa bahati mbaya kiongozi mkuu wa chama na ambaye pia ni KUB haonyeshi kuchukua hatua kurekebisha hali hii,” ameeleza Maselle.

Akizungumzia suala la kutoingia bungeni, wabunge hao wawili wamesema, “suala la kutoingia bungeni kwa siku 14 lilianzishwa na Mheshimiwa Esther Bulaya, ambaye kwa sasa inawezekana ndiye Mshauri Mkuu wa mwenyekiti Freeman Mbowe kwa mambo ya chama na Bunge.

“Kwamba, mheshimiwa Bulaya ndiye aliyeanza kutoa maelekezo kwa wabunge kuwa wasiingie bungeni kwa siku 14, lakini wabunge wakahoji mamlaka ya kufanya hivyo ameyatoa wapi?

“Baadhi ya wabunge akiwamo wale waandamizi kabisa, wakataka kiitishwe kikao cha Kambi ya Upinzani ili tuweze kujadili jambo hilo kwa mapana kwa kuweka bayana hasara na faida zake.”

Aidha, wabunge hao wanasema,  katika mjadala huo, Mbowe alisema, “hili ni wazo, hivyo tuendelee kujadiliana. Lakini  ghafla ndani ya kama nusu saa hivi, na wakati huo, wabunge walioanza kujadili wakiwa hawajafika hata 10, Mbowe akaja tena kitu kinachoitwa, “Waraka wa KUB,” ambako kukaelezwa kuwa ni marufuku kwa wabunge wa Chadema kuingia bungeni, kukaribia maeneo ya viwanja vya Bunge na kuondoka Dodoma.”

Maselle na Sokombi wanasema, “sisi tukajiuliza, kama ilikuwa ni kufungua mjadala, kwa nini sasa kabla ya hatujamaliza kujadili, kunatolewa amri? Uamuzi wa awali wa Mhe Bulaya ukawa ndio uamuzi wa Chama na sisi wote tukalazimishwa tufungwe nao.”

Akizungumzia matatizo yanayoikabili Chadema, Maselle amesema, “shida kubwa ya Chadema ni kusikiliza baadhi ya watu na kudharau wengine na kwamba pale ambako mtu anahoji, mambo yanavyoendeshwa, unaitwa Msaliti, msumbufu, ama mpinzani wa Mwenyekiti.

“Kwamba, unachotakiwa ukiwa Chadema, kila wasemacho wateule wachache ni sharti ukitekeleze.”

Ametaja kero nyingine kubwa iliyopo ndani ya chama hicho ukiondoka hayo, “ni pamoja na ubaguzi, ubabe na dharau ni kutokuwapo uwazi kwenye matumizi ya rasimali za chama, ikiwamo matumizi ya ruzuku na fedha za michango tuliyochanga sisi wenyewe wabunge.”

Maselle anasema, kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, wabunge ni wenezi wakuu wa chama, lakini katika kutekeleza majakumu yao, wamekuwa wakimbana na maswali ambayo ni vigumu kuyajibu, hasa kuhusiana na matumizi ya fedha za ruzuku.

Amesema, “huko nyuma kabla hatujawa wabunge maswala haya yalikuwa wazi sana yalijadiwa na wanachama kwa kila ngazi. Wanachama walifurahia chama chao bila manung’uniko kwa kuwa walifahamu hali ya chama chao.  Siku hizi agenda hiyo haipo tena hivyo manung’uniko ni makubwa.”

Amesema, sisi wabunge wa Chadema tulikuwa tunachanga Sh. 1,560,000 kwa wabunge wa Viti Maalum kila mmoja na Sh. 520,000 kwa mbunge wa jimbo kila mwezi.

“Hapa hoja siyo kuchanga, kwanza ni takwa la kikatiba, hoja ni jinsi fedha hizo za michango ambayo tuliambiwa zitatumika kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, jinsi zilivyotumika nje ya mipango iliyokusudiwa, na bila idhini ya vikao vyenye mamlaka hiyo.

“Inasemekana fedha hizo kwa kiasi kikubwa zimetumika kwa manufaa ya watu binafsi kama mradi wa mashamba ya mpunga huko Ifakara Mkoani Morogoro ambapo Mbowe alikwenda kuanzisha kilimo hicho kwa kutumia pesa za chama bila hata business plan na kuingia katika hifadhi ya serikali na kuvurumishwa na hivyo zaidi ya sh. 800,000,000 kutoka fedha hizo zikapotea.  Haya yanauma sana.

“Sisi mpaka tulipoacha kuchanga tukitaka kwanza maelezo ya matumizi ya fedha tulizokwisha changia tulikuwa tayari tumeshachanga zaidi ya Sh. 56 milioni, kila mmoja,” wameeleza Maselle na Sokombi.

Wamesema, “ndani ya Chadema kuna mgawanyiko mkubwa unaotokana na baadhi ya watu kujiona wao ni bora kuliko wengine na kwa bahati mbaya sana, jitihada zote za kutaka kuondokana na hali hii, ili tubaki tukiwa wamoja tunapoelekea uchaguzi mkuu zinaonekana zimeshindikana.

“Kwa mtazamo wetu, kuna uwezekano mdogo sana kuwa ndani ya Chadema watu watarudi na kuwa wamoja na kuaminiana tena. Tukiri kwamba dhana nzima ya kupendana na kuaminiana imeondoka na badala yake tunatuhumiana, kubaguana na kujengeana uadui dhidi yetu wenyewe.

“Tumejitakia nakujiongeza kufika kwenye mgogoro ambao unakiboa chama kwa kasi kubwa.  Viongozi wamelewa madaraka wakasahau michango ya wenzao haikuwa sahihi kuruhusu mtu kama Edward Lowasa, Fredrick Sumaye, Anthony Komu na Joseph Selasini, kwamba wametukanwa na wanasiasa wanaojiita makamanda.”

Sokombi na Maselle, wamekuwa wabunge wa kwanza wa Viti Maalum kutoka Chadema katikati ya mkutano wa Bunge la bajeti na kujiunga na NCCR- Mageuzi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!