Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge wa Lipumba wasusiwa na wapinzani bungeni
Habari za SiasaTangulizi

Wabunge wa Lipumba wasusiwa na wapinzani bungeni

Wabunge wa UKAWA wakiwa wamevalia nguo nyeusi wakiwa nje ya ukumbi wa bunge
Spread the love

SPIKA wa Bunge,  Job Ndugai amewapiga vijemba wapinzani muda mfupi baada ya kumalizika kazi ya kuwaapisha wabunge 8 wa viti maalum walioteuliwa na Cuf kupitia Mwenyekiti  Ibrahim Lipumba anayetambulika na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, anaandika Dany Tibason.

Ndugai amesema kuna haja ya wapinzani kusoma katiba ya nchi na kusema kwamba wanaodhani yeye ni dhaifu, waangalie kichotokea baada ya kutia saini na kukubali kupokea wabunge hao hatua mbayo imesababisha waliokuwapo kukosa sifa baada ya kufukuzwa na Lipumba

”Kuna baadhi yenu mnasema mimi ni dhaifu, sasa ngalieni kilichotokea hapa someni katiba vizuri na kuielewa,” amesema

Ndugai aliwaapisha wabunge hao wa viti maalum kabla ya kipindi cha maswali na majibu huku wakisindikizwa na wabunge wa CCM.

Katika tukio hilo Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga alionekana kuwa kituko kutokana na muda wote kuungana na wabunge wa CCM na wabunge wapya ambao walikuwa wakiitwa kuapishwa.

Aliyekuwa wa kwanza kuapishwa alikuwa ni  Alferedina Kahigi ambaye alionekana kula kiapo huku akiwa na hofu kwa kushindwa kusoma vyema baada ya kuonekana kusitasita kama mwanafunzi wa darasa la kwanza.

Wengine walioapishwa na Spika ni Kiza Husein Mayeye, Nuru Bafadhili,Rikia  Ahmrd Kassim, Shamsia Mtamba,Sonia Magogo na Zainab Ndolwa Amir.

Muda mfupi baada ya Spika Ndugai, kumaliza kuwaapisha wabunge hao wa viti maalum,alimwagiza katibu wa Bunge kuwapatia fomu ili kuweza kuchagua kamati wanazopenda kuzitumikia ikiwa ni pamoja na kuanza kushirikia katika kamati kuanzia siku ya kuapishwa kwao.

“Nawapongeza wabunge ambao wameapishwa leo na ninamwagiza katibu wa Bunge kuwapatia fomu wabunge wapya ili waweze kujaza kwa lengo la kuchagua kamati ambazo wanataka kuwepo na wataanza mara moja leo leo.

“Kilichofanyika leo kwa kuwaapisha wabunge hawa wapya kinatukumbusha utii wa kikatiba na kiapo kwa ujumla wake kwa katiba ya nchi yetu pia katiba inaongelea suala la uwepo wa vyama vya siasa uwepo wa mbunge unahusiana na siasa na taratibu katika chama chake” alisema Ndugai.

Baada ya kusema hayo Spika alisema kuwa wabunge ambao wameapishwa taratibu zote zimefuatwa na zimekamilika.

SPIKA AJITAPA

Pamoja na mambo mengine Spika wa Bunge Job Ndugai amejitapa kuwa kiti chake kina nafasi yake na siyo kiti dhaifu kama wanavyosema baadhi ya wabunge wa upande fulani.

Ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kumalizika kuwaapisha wabunge wa viti maalum na kutoa maelekezo mbalimbali huku akisema kuwa siku za karibuni kuna maadhi ya vyombo vya habari ambavyo viliandika kuwa Spika ni dhaifu.

“Wapo baadhi ya wale wanaosema kuwa Spika ni dhaifu sasa udahifu wangu ndipo unapoonekana,mwisho wa siku spika siyo dhaifu.

“Hata wale ambao wapo upande ule wanaoendelea kusema kuwa Spika ni dhaifu wataona udaifu wangu lakini nataka kusema kuwa spika ana nafasi yangu “after low” yanapotokea maamuzi ndipo utakapoona kuwa kuwa Spika siyo dhaifu.
NDANI YA UKUMBI.

Katika kipindi hicho cha kuwaapisha wabunge kwa upande wa upinzani, ni wabunge watatu tu ambao walikuwa ukumbini.

Wabunge ambao walikuwa ukumbini kwa nafasi ya upinzani ni wa Jimbo la Kinondoni, Maulidi Mtulya (CUF),mbunge wa Mtwara mjini Nachuma Mafutaa (CUF) na Mbunge wa Kaliua, Maghadalena Sakaya(CUF).

Wabunge wengine kutoka Chadema,NCCR-Mageuzi,ACT-Wazalendo pamoja na wabunge wa CUF hawakuwepo ndani ya ukumbi wa bunge.

Licha ya kutokuwepo ukumbini  wabunge wa CCM pamoja walionekana kuwalaki na kuwashangilia wabunge wapya wa CUF walioapishwa na Spika.

MAONI YA WABUNGE

Wabunge  wote ambao hawakubaliani na kitendo cha Spika kuwaapisha wabunge wapya walivalia nguo nyeusi kwa madai kuwa wapo katika maombolezo ya msba wa kuminya demokrasia.

Mbunge wa Ukonga,Mwita Waitara (Chadema), alisema kuwa wabunge wameshuhudia serikali kwa kushirikiana na CCM ikiminya demokrasia bila kuwa na aibu.

Alisema kuwa kwa sasa wabunge walioapishwa wanatambuliwa kama wabunge wa Lipumba na siyo wabunge wa CUF kama wanavyopotosha Umma.

Mwita alisema kitendo cha kuwaapisha wabunge hao bila kusikiliza pande zote mbili ni dalili mbaya ya uminywaji wa demokrasia nchini.

“Hawa ni wabunge wa CCM na Lipumba pamoja na msajili wa vyama vya siasa kwani kilichofanywa na spika ni maelekezo na si vinginevyo” alisema Mwita.

Mwita alisema kuwa Prof.Lipumba anafanya vujo ndani ya chama chake kwa kulindwa na kufadhiliwa na serikali ya CCM.

Naye mbunge wa Tunduma,David Silinde (Chadema) alisema Ukawa ya ukweli haikubaliani na kitendo kilichofanywa na Spika cha kuwaapisha wabunge wa viti maalum ambao walipendekezwa na Prof.Lipumba.

Alisema kinachofanywa na serikali, msajili wa vyama vya siasa pamoja na ushabiki wa Serikali ya CCM ni jambo ambalo linaonesha udhaifu mkubwa wa kusimamia haki.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!