July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Viti maalum: Spika Ndugai awashangaa Chadema kulumbana

Spika Job Ndugai

Spread the love

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ‘amekishangaa’ Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuendelea na mjadala wa ama wapeleke majina ya wabunge wa viti maalum bungeni au wasipeleke. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Ndugai ametoa maelezo hayo bungeni leo Alhamisi tarehe 12 Novemba 2020, kabla ya kuahirisha shughuli za Bunge mchana jijini Dodoma akisema, bungeni kuna wabunge wa aina nne.

Amesema, kuna wabunge wa majimbo, nafasi tano za Baraza la Wawakilishi, nafasi kumi za Rais ambazo huteua anayemtaka na wale wa viti maalum.

Spika Ndugai amesema, nafasi za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi zitapatikana katika mkutano wa Bunge unaokuja lakini “Kuna vyama bado havijaleta wabunge hasa wa viti maalum, tunachoona mitandaoni huko wanalumbana, eti walete, wasilete.”

“Kwa sababu ni fursa za kina mama wanalumbana, ingekuwa za wanaume, wangekuwa wamefika hapa. Haipaswi kuwa hata mjadala,” amesema Spika Ndugai.

Akiendelea kueleza, Spika Ndugai amesema “wapiga kura wengi kina mama unawazuiaje, wewe unazuiaje, haipaswi kuwa hata mjadala. Iko fursa hupaswi kuichezea.”

Halima Mdee

Katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilinukuliwa ikisema, vyama viwili vya CCM na Chadema ndivyo vyenye sifa ya kupata wabunge wa viti maalum.

CCM imejipatia viti maalum 94 huku Chadema ikipata 19.

Hata hivyo, viongozi wakuu wa Chadema pamoja na ACT-Wazalendo, walijitokeza mbele ya waandishi wa habari na kupinga matokeo ya uchaguzi huo kwa madai uligubikwa na ukiukwaji wa sheria, kanuni na miongozo.

Vyama hivyo, vilitaka uitishwe upya uchaguzi mkuu na usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi upande wa Tanzania bara na Zanzibar huku ukiitosha maandamano ya amani yasiyokuwa na kikomo kuanzia tarehe 2 Novemba 2020.

Hata hovyo, maandamano hayo hayakufanyika na kujikuta baadhi ya viongozi wake wakishikiliwa na polisi kwa siku kadhaa kisha kuachiwa na wanaendelea kuripoti polisi kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Kutokana na hali hiyo, ndani na nje ya Chadema, kumekuwa na mjadala mkali wa ama wateue wabunge wa viti maalum au waachane navyo.

Kumekuwa na hoja mbili, ikiwamo kwamba, wakiteua wa kuwapeleka bungeni, itakuwa wanakubaliana na matokeo ya uchaguzi waliyosema haukuwa huru na haki na wengine wanasema, wasiende kwa kuwa haukuwa uchaguzi huru na haki.

Tundu Lissu, aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema katika uchaguzi huo, ni miongoni viongozi wa Chadema ambao wamejitokeza hadharani kupinga kupeleka wabunge wa viti maalum.

“Kupekela wabunge wa viti maalum ni kuhalalisha uchafuzi wa uchaguzi uliofanyika. Hivyo msimamo wa chama wa kamati kuu ni kutopeleka wabunge wa viti maalum,” alisema Lissu ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa chama hicho (bara).

error: Content is protected !!