January 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Viti Maalum Chadema: NEC yabebeshwa mzigo

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania, kueleza Watanzania ilipopata majina 19 ya wanachama walioteuliwa kuwa wabunge wa Viti Maalum kupitia chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano tarehe 25 Novemba 2020, jijini Dar es Salaam, John Mnyika ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho amesema, mwenye mamlaka ya kuteua majina hayo kwa mujibu wa Katiba ya Chadema ni Kamati Kuu ambayo mpaka sasa hajateua.

Jana Jumanne tarehe 24 Novemba 2020, Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaapisha wanachama 19 wa Chadema kuwa wabunge wa Viti Maalum kupitia chama hicho.

Baada ya kuwaapisha viwanja vya Bunge, Spika Ndugai alisema, alipokea barua ya uteuzi wa majina hayo kutoka NEC tarehe 20 Novemba 2020.

          Soma zaidi:-

Wanachama hao walioongozwa kuapishwa na Halima Mdee, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema  (Bawacha), walidai uteuzi wa majina yao ulipata baraka zote za chama hicho.

“Chadema hakijateua wabunge wa viti maalumu au wagombea ubunge viti maalumu, wala hakijawasilisha orodha yoyote ya uteuzi wa wabunge viti malaumu, NEC ieleze majina hayo imepata wapi,” amesema Mnyika na kuongeza:

“Kwa Katiba ya Chadema, mamlaka ya uteuzi wa wabunge yako kwa Kamati Kuu ya chama Ibara ya 7.7 ambayo inasema, moja ya kazi ya Kamati Kuu ya chama ni kuthibitisha uteuzi wa wagombea. Kamati Kuu ya chama haijawahi kufanya kikoa cha kuteua majina ya wabunge wa Viti Maalunu,” amesema Mnyika.

Mnyika amesema, Katiba ya Chadema inaelekeza Katibu Mkuu kuwasilisha orodha ya majina hayo NEC, jambo ambalo yeye hajalifanya.

“Pili, Katibu Mkuu wa chama mwenye mamlaka ya kimawasiliano ya kuwasiliana na NEC, sijawahi kuwasilisha orodha yoyote NEC ya wanaoitwa waliopendekezwa kuwa wabunge viti maalumu,” amesema Mnyika.

Mnyika amesema, Chadema kimeshangazwa na uteuzi huo kwa kuwa, iliwasilisha taarifa rasmi NEC kwamba, haijateua wabunge hao na kwamba, tume hiyo kupitia barua ya tarehe 10 Novemba 2020 iliijibu Chadema, ikikiri kutopokea orodha hiyo.

Mwenyekiti wa NEC, Semistocles Kaijage

Amesema, NEC kupitia kwa mkurugenzi wake, Dk. Wilson Mahera, ilikiri kwamba chama hicho hakijawasilisha majina hayo na kukitaka Chadema kufanya hivyo huku akipewa na fomu namba 8(d) ambazo zinapaswa kujazwa na wanaopendekezwa.

“Mawasiliano yangu ya mwisho NEC zilikuwa barua mbili,  barua ya kwanza tumekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara kwenye masuala mbalimbali ya uchaguzi, barua ya mwisho niliiandika  tarehe 9 Novemba 2020 kwenda kwa  mkurugenzi NEC.”

“Barua hii niliiandika baada ya mkurugenzi huyo kunukuliwa kwenye vyombo vya habari akisema, Chadema imewasilisha orodha ya viti maalumu, kwamba NEC imewasilisha bungeni majina 19 ya wabunge kupitia Chadema,” amesema Mnyika na kuongeza:

“Baada ya barua hiyo, NEC wakajibu barua hiyo kwenda Katibu Mkuu Chadema, katika barua hiyo iliyosainiwa na Dk. Mahera (Wilson Mahera, Mkurugenzi wa Uchaguzi) tareh 10 Novemba ikakiri Chadema haijawasilisha orodha yoyote.”

“Tume ikaandika barua kutoa mwito kwa Chadema kuwasilisha orodha na sio orodha peke yake pamoja na fomu namba 8(d) ambayo kipengele C inapaswa kusainiwa na katibu mkuu,” amesema Mnyika huku akionyesha fomu hizo 113 alizozipokea kutoka NEC

“Kwa hatua hiyo, NEC ijitokeze hadharani, ieleze hiyo orodha iliwasilishwa na nani, nani aliyesaini eneo la katibu mkuu ikiwa mimi sikufanya hivvyo au naibu wangu,” amesema Mnyika

Baada ya mkutano huo na waandishi kumalizika, MwanaHALISI Online lilimtafuta Dk. Mahera ili kupata ufafanuzi juu ya madai ya Mnyika, hata hivyo hakupokea simu.

Halima Mdee, Mbunge wa Chadema Viti Maalim

Badala yake, Dk. Mahera alituma ujumbe mfupi wa maneno uliosema “samahani, siwezi  kuzungumza kwa sasa.”

Hata alipoulizwa kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwamba NEC ilipata wapi orodha ya majina ya wanachama wa Chadema iliyowateua kuwa wabunge Viti maalumu, hakujibu mpaka habari hii inaandikaa.

Kilichotokea kwa Dk. Mahera ndivyo imekuwa kwa Mwenyekiti wa NEC, Semistocles Kaijage alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita pasina kupokelewa.

Jitihada za kuwatafuta wawili hao zinaendelea.

error: Content is protected !!