Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Viongozi Chadema kumaliza wiki kizimbani
Habari za Siasa

Viongozi Chadema kumaliza wiki kizimbani

Viongozi wa Chadema wakiwa mahakamani
Spread the love

VIONGOZI waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), watapanda kwenye kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuendelea kusikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili tangu Februari mwaka jana. Anaripoti Faki Sosi  … (endelea).

Kesi hiyo Na. 112 ya mwaka 2018, ilifunguliwa wiki chache baada ya tukio la kuuliwa kwa Akwilina Akwilin aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam.

Watuhumiwa husika ni mwenyekiti wa Chadema na mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dk. Vicent Mashinji na manaibu katibu wakuu John Mnyika (Bara) ambaye pia ni mbunge wa Kibamba, na Salum Mwalimu wa upande wa Zanzibar.

Wenzao ni Halima Mdee (Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) Taifa na mbunge wa Kawe; Mweka Hazina wa Bawacha na mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Kabla ya ushahidi kuanza kutolewa dhidi ya watuhumiwa hao, Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba anatarajiwa kutoa uamuzi wa kama mahakama ikubali kupokea kielelezo cha kamera ya video na mashine mbili za kurekodia (tepu) zilizotumiwa na shahidi wa saba wa upande wa mashitaka, askari polisi F5392 Charles, mwenye cheo cha koplo ambaye ni mpigapicha za video wa Jeshi la Polisi.

Shahidi huyo kupitia kwa mwanasheria wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), aliomba vitendea kazi hivyo vitambuliwe na mahakama kama sehemu ya vielelezo.

Uamuzi wa suala hilo ambao hautaathiri kuendelea kwa usikilizaji wa ushahidi, unatarajiwa kutolewa baada ya upande wa utetezi chini ya wakili Peter Kibatala, kupinga kielelezo hicho kupokelewa.

Hoja ya wakili Kibatala ni kwamba ushahidi wa kieletroniki hauwezi kupokewa mahakamani mpaka kuwepo hati mahususi ya kiapo ya utoaji wa vielelezo hivyo kama inavyoelekeza sheria ya ushahidi wa kielektroniki fungu la 18 na 19.

Baada ya hapo, Dk. Zainab Mango, Wakili Mkuu wa Serikali aliieleza mahakama kuwa Jamhuri imetimiza matakwa yote ya kisheria kuhusu utoaji wa ushahidi wa kieletroniki.

“Ni rai yetu kuwa tumefanikiwa kukidhi matakwa yote ya sheria kifungu cha 18(2) cha sheria ya ushahidi wa kieletroniki yanayotaka vielelezo vitunzwe vizuri kabla ya kuwasilishwa mahakamani,” alieleza.

Alidai kuwa matakwa ya sheria juu ya ushahidi huo ni pamoja na kutunzwa na kuhifadhiwa kwa vidhibiti vya kieletroniki na mtu aliyehusika kwenye kuchakata vielelezo hivyo, pia vifaa vilivyotumika viwe vizima na kutopata kutumika kwengineko kabla.

Dk. Zainabu alidai Kifungu 18 kinahitaji kitu kitachoithibitishia mahakama uhalisia wa vielelezo hivyo na kwamba “ushahidi unaweza kutolewa kwa maneno, nyaraka au hati ya kiapo.”

Alirejea kesi iliyotajwa na wakili Kibatala jana – Na. 29 iliyohusu Benki ya Exim na Kilimanjaro Cofee Company Limited. Iliamuliwa mwaka 2013 kabla ya marekebisho ya sheria hiyo ya ushahidi wa kieletroniki na kwamba kesi hiyo inahusiana na masuala ya kibenki kupitia kifungu cha 78(A) sambamba na fungu la 79.

Mwanasheria Dk. Zainab pia alirejea kesi ya Emmanuele Mwasonga ambayo ushahidi wa simu ulikataliwa mahakamani kwa hoja kuwa mazingira ya hifadhi ya kifaa hicho yalikuwa na kasoro kwani simu iliyorekodi sauti, ilitumika kumrushia mtu mwengine sauti na baadaye ilipotea; badala yake ikatafutwa CD na kukwekwa sauti iliyokusudiwa kuwa kielelezo na kupelekwa mahakamani.

Akishirikiana na Dk. Zainab kuiwakilisha jamhuri, Paul Kadushi, Wakili wa Serikali Mkuu, aliieleza mahakama kuwa ushahidi uliotolewa umekidhi vigezo na matakwa ya kifungu cha 18(2), (a), (b) na (c).

Alidai kuwa matakwa ya sheria yanataka kigezo cha kifaa kilichohifadhi ushahidi kuwa kinachofanya kazi wakati wote na kwa hoja yao ya pili ya kuwepo hati ya kiapo, alieleza kuwa sheria ya ushahidi kwa mashauri ya jinai kuhusu kilichorekodiwa, haishurutishi kuwepo kwa hati ya kiapo.

Alieleza kuwa katika mashauri ya madai, ni jambo la kawaida ushahidi kuwasilishwa chini ya kiapo ila kwa mashauri ya jinai mahakama inapokea kwa njia ya maneno.

“Sisi tunawasilisha kuwa kuwepo kwa hati ya kiapo sio hoja, tunaiomba mahakama yako isizingatie kabisa mapingamizi yaliyowasilishwa na wenzetu na ipokee vielelezo vilivyotolewa na shahidi,” alihitimisha maelezo yake.

Akijibu hoja hizo, Wakili Kibatala aliendeleza pingamizi lake kuwa kutoa ushahidi wa kieletroniki kunalazimu kufanywa chini ya hati ya kiapo.

“Sheria ya kieletroniki imelenga hasa mahakama kuu Kitengo cha Biashara na hata utungwaji wa sheria, hivyo umetokana na mashauri ya kibiashara kwenye mahakama hiyo. Tunabomoa hoja ya Dk. (Zainab) Mango kuwa eti kwasababu uamuzi wa kesi ya Exim Bank umefanywa kabla ya marekebisho ya sheria ya kieletroniki, sheria haielei hewani,” alidai.

Wakili Kibatala alieleza kuwa ushahidi huo ungeweza kukubaliwa kwa mujibu wa sheria labda kutoka kwenye CCTV kamera au kwa Mwandishi wa Habari lakini shahidi huyu anatoka kwao (Jamhuri).

Alidai tafsiri ya ‘au’ ‘na’ (‘And’ & ‘Or’) kwenye kifungu cha 18 imetumiwa vibaya na wakili Kadushi na kwamba hitaji la fungu la 18(a) na (b) visomwe kwa pamoja kumaanisha vielelezo vile vingetolewa endapo vinamilikiwa na washtakiwa.

Akiunga mkono hoja ya Wakili Kibatala, wakili Hekima Mwasipu alieleza kuwa shahidi wa sita ni Ofisa wa Polisi aliyekuwa chini ya Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni ambaye “ana maslahi kwenye shauri hili.”

Ni hapo Hakimu Simba alipoamua kuahirisha shauri hilo kwa ahadi kuwa litaendelea kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Julai 24, baada ya uamuzi wa pingamizi la upande wa utetezi.

Viongozi wa Chadema walikamatwa baada ya tukio lililotokea wakati wakiwa kwenye msafara wakienda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni.

Tukio hilo la Februari 16, 2018 ikiwa ni jitihada ya Chadema kupata uhakika wa vitambulisho vya uwakala kwa mawakala waliokuwa wanasimamia uchaguzi huo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!