January 27, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Vigogo TPA wasimamishwa, bandari tano kuchunguzwa na CAG

Bandari ya Dar es Salaam

Spread the love

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum Bandari za Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara, Tanga na Kyela kutokana na kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Pia, Majaliwa amewasimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Nuru Mhando pamoja na Meneja wa Matumizi ya Fedha wa TPA, Witness Mahela ili kupisha uchunguzi utakaofanywa na CAG wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha zinazowakabili.

Waziri mkuu amechukua hatua hiyo baada kupokea ripoti ya Ukaguzi Maalum uliofanywa na CAG katika hesabu ya Bandari ya Kigoma kwa mwaka 2017/2018 na 2018/2019.

Lengo la ukaguzi huo lilikuwa kujiridhisha kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma.

Majaliwa alitoa maagizo hayo jana Jumapili, tarehe 27 Desemba  2020 katika kikao chake na Waziri na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania na Menejimenti ya TPA, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kilichofanyika katika ofisi za TPA jijini Dar es Salaam.

Alisema, taasisi hiyo imebeba taswira ya uchumi wa Taifa, lazima kazi ifanyike vizuri.

Majaliwa aliitaka Bodi ya Bandari Tanzania, ihakikishe mamlaka hiyo inafanyakazi kwa weledi na isisite kuchukua hatua kwa mtumishi atakayebainika kutenda makosa na isimbebe kwa namna yoyote.

Alisema miongoni mwa mambo yasiyoridhisha yanayofanywa na mamlaka hiyo ambayo yanaikosesha Serikali mapato ni pamoja na msamaha wa kodi ya zaidi ya Sh.2 bilioni iliyoutoa kwa kiwanda cha saruji cha Mbeya licha ya kukataliwa na kamati ya misamaha.

Majaliwa alisema, licha ya kuongezeka kwa makusanyo lakini kati ya fedha inayokusanywa asilimia 70 tu ndiyo inayoongia serikalini na kiasi kilichobaki kinaishia mifukoni jambo ambalo halikubaliki.

”Ripoti ya CAG ya Bandari ya Kigoma haijatufurahisha imeonesha mambo mengi mabovu.”

Alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida, TPA iliidhinisha malipo ya Sh.8.2 bilioni kwenda Bandari ya Kigoma kwa ajili ya kwenda kufanya malipo mbalimbali huku ukomo wa bandari hiyo ni Sh.7.4 bilioni, fedha hizo zilitumika kufanya malipo yasiyostahili kwa watu mbalimbali akiwemo mfanyabiashara wa duka la ujenzi mjini Kigoma, Eliya Mtinyako aliyelipwa zaidi ya Sh.900 milioni.

“Malipo haya yamefanyika huku kukiwa hakuna nyaraka zinazoonesha kama alilipwa kwa sababu zipi kwani mfanyabiashara huyo aliyelipwa hakuwahi kutoa huduma yoyote kwa mamlaka hiyo na wala si mzabuni. Pia amelipwa bila ya kuwepo kwa nyaraka za madai.”

Alisema licha ya upotevu huo wa fedha katika bandari hiyo ya Kigoma, pia Mhasibu wa Bandari ya Kigoma, Madaraka Madaraka alifuta madeni ya zaidi ya Sh.1 bilioni waliyokuwa wakidaiwa wateja bila ya kufuata taratibu na kuishababishia Serikali hasara.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema ripoti hiyo ya CAG, imebainisha uwepo wa malipo hewa ya zaidi ya Sh.2 bilioni ambazo zimelipwa bila ya kufuata taratibu za malipo na wahasibu walipoulizwa walidai ni maelekezo kutoka makao makuu ya TPA.

Alisema walipofanya ukaguzi walibaini uwepo wa hundi 150 ambazo tayari zimesainiwa na wahusika wote na zimebaki wazi na mtu yeyote anaweza kujaza jambo ambalo ni kinyume na taratibu za Serikali kwani hazitakiwi kuwa hivyo.

“Huu ni mpango wa wizi, mamlaka kubwa kama hii hatuwezi kuacha hivi, hii fedha iliyopotea tungeweza kujenga zahanati, tungewapa TATURA (Wakala wa Ujenzi wa Barabara Mjini na Vijijini), wangejenga barabara nyingi tu. Mheshimiwa anapoelekeza fedha zipelekwe bandari ni kwa ajili ya kuboresha bandari yetu na lazima zitumike vizuri.”

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu,

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu alimuagiza DCI, Robert Boaz ahakikishe Mtinyako na Madaraka wanatafutwe popote walipo na kukamatwa.

Pia, aliagiza watumishi wote waliosimamishwa kazi wachunguzwe haraka na ikibainika kwamba hawana hatia warejeshwe kazi na wakikutwa na hatia hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Majaliwa alimuagiza Mkurugenzi wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo afanye uchunguzi kuhusu Kalibilo ambaye ameonekana kuingiziwa kiasi kingi cha fedha bila ya kuwepo nyaraka zinazoonesha sababu za mtumishi huyo kulipwa fedha hizo.

“Agosti anaonekana alilipwa Sh.55 milioni, Septemba Sh.53 milioni, Oktoba Sh.37 milioni na Novemba Sh.19 milioni 19, lazima atafutwe popote alipo ijulikane fedha hizo alilipwa kwa ajili gani.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu alirudia agizo lake alilolitoa wiki iliyopita alipofanya ziara katika bandari ya Kagunga ambapo aliiagiza TPA ihakikishe ifikapo Januari Mosi 2021 Bandari ya kimkakati ya Kagunga iliyoko katika Kata ya Kagunga wilayani Kigoma iwe imeanza kutoa huduma.

Mradi wa ujenzi wa bandari ya kimkakati ya Kagunga ulikamilika 2017, ukihusisha ujenzi wa jengo la abiria pamoja na la mizigo, nyumba ya kuishi mtumishi na jengo maalumu lakini hakuna mtumishi katika bandari hiyo ambayo ujenzi wake uligharimu Sh.3.8 bilioni

error: Content is protected !!