January 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Vigogo hospitali za serikali kikaangoni, Waziri Gwajima…

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania, imeagiza mamlaka husika kuzifanyia uchunguzi hospitali zote za umma, ili kubaini sababu za kukwama kwa mfumo wa utoaji huduma za afya nchini humo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Agizo hilo limetolewa jana Jumatano tarehe 30 Desemba 2020 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Waziri huyo wa afya ametoa agizo hilo baada ya kubaini madudu katika hospitali hiyo, yanayodaiwa kukwamisha watumishi wa afya kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika utoaji wa huduma za afya.

“Na kwa sababu hizi, hospitali zinafanana, nimepita kwingi tutaweza kujua siri za kuwa na watumishi waliomo ndani na hawafanyi kazi na tunawalipa mshahara, ni kitu gani?” amehoji Dk. Gwajima.

Madudu yaliyotajwa na Dk. Gwajima ni pamoja na matumizi mabaya ya mapato ya hospitali hizo na uzembe wa watendaji, unaosababisha hospitali kushindwa kujiendesha sambamba na kutoa huduma za afya kwa wananchi.

“Kuna matatizo matatu, moja watumishi walioko kazini walioajiriwa na maafisa utumishi wanafuatiliwa kuona wanafanya kile walichoajiriwa nacho? Tuna wahandisi wa baiolojia kwa nini vifaa havitengenezwi?” amehoji Dk. Gwajima.

Dk. Gwajima amehoji “Hela tunazozipata kutoka kwa wateja tunao wahudumia tunazitumiaje?”

Amesema ukaguzi huo utaisaidia Serikali kubaini chanzo cha changamoto hiyo.

“Kwa hiyo nini kinaendelea hapo kitatajwa kwenye hiyo ripoti, lengo kubwa kuhakikisha uzalishaji, yaani ufanisi wa uendeshaji wa mifumo yetu huku inakuwa imara,” amesema Dk. Gwajima.

Aidha, Dk. Gwajima amesema, matokeo ya ripoti ya ukaguzi hiyo yataisaidia Serikali kubaini viongozi na watumishi wa afya wazembe, huku akiahidi kuwaondoa kazini watakaobainika kutotimiza majukumu yao kikamilifu.

“Kuanzia sasa hivi, huko niendapo huko kwengine, sitarajii kukutana na mambo kama haya yaani, kule watu wajipange sababu vitu vyote viko ndani ya uwezo wao. Kitendo cha kwenda kitengo kingine nikakuta mazingira kama haya yanaendelea ina maana hatusikilizani,” amesema Dk. Gwajima.

Dk. Gwajima amesema “Tukiagizana tunaacha kwenye vyombo vya habari, utendaji unakuwa wa mazoea, tunakwenda kuchukua hatua tuwapatie watu wengine ambao wanaweza kuongoza hospitali kwa kasi kubwa zaidi kulingana na wakati.”

Akizungumzia ziara yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dk. Gwajima amesema kuna baadhi ya huduma za afya hazitolewi hospitalini hapo kutokana na uzembe wa uongozi wake.

“Huduma saa nyingine hazipatikani kwa sababu nyingine hata hazipo, yaani watu wanatengeneza mazingira ndani ya hospitali ya kutoendeleza huduma,” amesema Dk. Gwajima.

Amesema hospitali hiyo inapoteza wateja wengi hususani wa ugonjwa wa macho, kutokana na ubovu wa vifaa tiba.

“Tumeenda kwenye macho, tumeona mashine ipo inahitaji Sh.18,000 ili iweze kutengenezwa itengeneze miwani. Mtaalamu yupo lakini hatengezi miwani. Anapata mshahara wetu, atutengenezee miwani, tatizo anasema wateja wanaoakuja ni wengi wanaohitaji miwani lakini inabidi awapeleke nje,”amesema Dk. Gwajima.

Dk. Gwajima amesema, changamoto hizo zinachochewa na matumizi mabaya ya fedha zinazokusanywa.

“Mtumishi ameajiriwa ili afanye aliyoajiriwa nayo alipwe mshahara, hafanyi tataizo ni nini? Hawezeshwi, uongozi upo, hela zinapatikana zinakwenda wapi?” Dk. Gwajima amehoji.

Kutokana na changamoto hiyo, Dk. Gwajima ametoa siku 30 kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, kumpa taarifa ya mapato na matumizi yake kuanzia mwezi Januari hadi Desemba 2020.

“Ufanyike ukaguzi maalumu wa pesa zilizopatikana kuanzia Januari hadi Desemba 2020, zilitumikaje mpaka zikashindwa kuelekezwa kwenye mtu wa macho na maeneo mengine ambayo hayafanyi huduma. Zilitumika wapi mpaka tukalipa watu mishahara ambao walitakiwa watufanyie kazi lakini hawatufanyii,” ameagiza Dk. Gwajima.

Dk. Gwajima amesema “Nimewapa siku 30, hadi tarehe 30 Januari 2021 (Hospitali ya Mwananyamala),wawasilishe ripoti  hiyo. Nimekwepa kuchukua hatua haraka, inawezekana sivyo tunavyofikiria.”

“Nataka ripoti ije ituambie ili mtu atakapochukua hatua unakuwa unajiamini kwamba nilienda,  nikakuta hivi akashindwa kunijibu.”

Waziri huyo wa afya ameagiza, uongozi wa hospitali za umma kufanyia kazi changamoto zinazo kwamisha utoaji huduma, ili kushawishi wananchi kutibiwa katika hospitali hizo.

“Kuna huduma katika vitengo mbalimbali lazima zishughulikiwe, vinginevyo tutakuwa na watu wanaokuja kwenye vituo vyetu  ambao hawana uwezo. Wale wenye bima zao na uwezo wao watakwenda vituo vya nje, sababu huku huduma hazipatikani,” amesema Dk. Gwajima.

error: Content is protected !!