UTAFITI wa rushwa ya ngono katika taasisi za elimu ya juu uliohusisha vyuo vikuu viwili vya Dar es Salaam na Dodoma, umewasilishwa leo tarehe 4 Disemba 2020, jijini Dodoma. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Mtafiti wa rushwa ya ngono nchini, Dk. Juvinary John amesema katika utafiti huo, jumla ya watu 589 walihojiwa juu ya uelewa wa rushwa ya ngono.
Ameanisha makundi yaliyohojiwa kuwa wanafunzi asilimia 81.6, watumishi asilimia 91.4 walieleza uwepo wa rushwa ya ngono Katika taasisi za elimu ya juu.
Kuhusu uwepo wa rushwa ya ngono, watumishi asilimia 68.6 walisema ‘ndio,’ watumishi asilimia 31.4 walisema ‘hapana,’ wanafunzi asilimia 57.5 walisema ‘ndio’ huku wanafunzi asilimia 42.5 walisema ‘hapana.’
Aidha, ameeleza sababu za kuwepo kwa rushwa ya ngono kuwa, kundi la wanafunzi mwitikio wao walisema ni pamoja na ukosefu wa maadili asilimia 63, ushawishi wa mtu mwenye mamlaka asilimia 27.7, mfumo wa utoaji taarifa kutokuwa rafiki asilimia 9.3.
Amebainisha mbinu zinazotumika kwenye rushwa ya ngono katika elimu ya juu ni pamoja na kutoa alama za chini na vitisho vya kutofaulu.
Ofisa Uhusiano kutoka taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini Doreen Mapwani pamoja na mkurugenzi wa uzuiaji rushwa wa Taasisi hiyo, Sabina Seja wamesema, taasisi hiyo inaendelea kutoa ushirikiano katika mapambano dhidi ya rushwa hususan rushwa ya ngono.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk. Ombeni Msuya amesema, chuo kimeimarisha kamati zote kwa kusimamia madaraja ya jinsia ambapo kuna masanduku 106 ya kutoa maoni juu ya changamoto.
Naye Mkurugenzi wa Taaluma na Jinsia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Lulu Mahan amesema, chuo hicho kimekuwa kikitoa adhabu kwa watumishi wanaobainika kujihusisha na rushwa ya ngono ikiwa ni pamoja na kuwafukuza.
Mkakati wa utafiti wa kupambana na rushwa ya ngono ulianza tarehe 18 Juni 2020.
Leave a comment