Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Urais Chadema: Mchungaji ajitosa kuwavaa Lissu, Mbowe na Nyalandu
Habari za Siasa

Urais Chadema: Mchungaji ajitosa kuwavaa Lissu, Mbowe na Nyalandu

Spread the love

JOTO la mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) linazidi kupamba moto, baada ya mwanachama wa chama hicho, Leonard Manyama kujitosa katika kinyang’anyiro hicho. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam…(endelea).

Manyama ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Tegeta jijini Dar es Salaam, ametangaza vipaumbele 17 endapo chama hicho kitampitisha na Watanzania kumpa ridhaa ya kuwaongoza.

Manyama anakuwa mtia nia wa tano kujitokeza hadharani kuweka adhima hiyo ya kuomba kupitishwa ili kupeperusha bendera ya Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Wengine waliotia nia ni, mwanachama wa chama hicho, Dk. Maryrose Majige, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mchungaji Peter Msigwa, mbunge wa Iringa Mjini.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Wengine ni; Lazaro Nyalandu, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati na Tundu Lissi, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho- Bada.

Shughuli ya utiaji nia ilianza tarehe 3 hadi jana 15 Juni 2020 ambapo Mchungaji Manyama aliwasilisha barua ya kutia nia ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema.

Leo Jumanne tarehe 16 2020, Manyama amezungumza na waandishi wa habari katika Ofisi cha Chadema Tegeta jijini Dar es Salaam na kueleza mikakati mbalimbali ya jinsi atakavyoongoza ncho iwapo ataibuka mshindi.

Amebainisha vipumbele vyake 17 akiwa na msemo “Niamini Nikuvushe”

1. KUJENGA TAIFA LENYE UMOJA, UPENDO NA MSHIKAMANO

Ninataka kujenga taifa lenye umoja, upendo na mshikamano.

Kitu hiki hakijawahi kuwepo tangu mfumo wa vyama vingi kurejeshwa nchini.

Nitaondoa chuki iliyojaa mioyoni mwa Watanzania kwa kusababishwa na itikadi za vyama vyetu.

Nataka kuondoa mitazamo ya sisi watawaa na wao wapinzania. Sisi wenye nacho na wao masikini.

Nataka kuondoa hali ya kufurahia mabaya kwa wenzetu, au hali ya kupanga njama za kudhuriana wenyewe kwa wenyewe.

Ninayo dhamira ya kujenga taifa la kusaidiana fito, tujenge nyumba moja na siyo kuonyeshana ufundi wa kunyang’anyana fito tukijenga nyumba hiyo hiyo. Niamini nikuvushe.

2. MFUMO WA ELIMU

Mfumo wetu wa elimu tulio nao si rafiki sana kwa ulimwengu wa sasa. Ni mfumo unaolifanya taifa kuendelea kuwa tegemezi.

Nitaufumua mfumo wa elimu na kuimarisha elimu kwa vitendo na kuiondoa elimu yetu kwenye nadharia. Yaani “from theory based education to practical based education.”

Vijana wetu leo wanasoma kwa ajili ya kufaulu mitihani na wakishahitimu, ni vitu vichache sana hubaki vichwani mwao kama maarifa.

Ufundishaji nao ni ule ule unaolenga mitihani, na baadaye tunawashindanisha kwa kigezo cha maswali na majibu. Hii huwafanya vijana wetu kutegemea ajira kila wanapohitimu.

Elimu ya nadharia imewafanya vijana wetu wengi kukataliwa na mfumo kwa madai ya kupata madaraja ya sifuri au nne.

Wanafunzi hao wakienda elimu kwa vitendo kama VETA hufanya vizuri sana na kujipatia ajira binafsi. Mafundi gereji wengi hawajasoma katika mfumo tunaouita rasmi. Lakini wanaujuzi wa kutosha na ndio wanaotengeneza magari ya watu wanaoitwa wasomi tena wengine ni waandisi.

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Mafundi ujenzi wengi wanaojenga majumba ya watu wasomi, hawana elimu ya nadharia juu ya ujenzi. Lakini bado wanafanya vizuri. Kwa utafiti wangu, elimu kwa vitendo ikirasimishwa, italisaidia taifa. Nitafanya hivyo.

3. BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU

Nitaiboresha bodi ya mikopo ya elimu ya juu. Kwanza kabisa kwa kufuta sheria kandamizi ya mwaka 2016 ya bodi ya mikopo ya elimu ya juu pamoja na merekebisho yake ambayo ni msumari wa moto kwa wanufaika wote wa mikopo hii.

Natambua dawa ya deni ni kulipa lakini kuwa na deni lenye kujengewa mazingira ya kumlemea mlipaji inakatisha tamaa hata ulipaji wenyewe.

Tutaweka sheria mpya ambayo itaondoa ongezeko la 6% kila mwaka kwenye deni linalokuwa limebaki kama sheria ya sasa inavyotaka.

Pia, nitahakikisha tunaweka makato nafuu yasiyozidi 8% kwa mwezi badala ya 15% za sasa.

Hii ni kwa sababu natambua kwamba wanufaika wengi wa mikopo ni wa kipato cha kawaida. Tusikopeshane kwa furaha halafu tulipane kwa karaha.

4. MASLAHI YA WALIMU

Kati ya watumishi wa umma ambao wamekuwa kama wanatolewa kafara, basi ni walimu.

Ualimu imekuwa kama vile ni kazi isiyo na heshima na inayoweza kufanya na mtu yeyote.

Nitaboresha maslahi ya walimu ili kuwapa moyo wa kufanya kazi. Pamoja na bidii na kazi kubwa wanayofanya walimu wetu, lakini naamini bado wanatumika chini ya uwezo wao kutokana na kuwa na maslahi duni.

Mimi binafsi pia ni mwalimu, hivyo nitahakikisha nailinda hadhi ya ualimu na walimu.

Dk. Maryrose Majinge, kada wa Chadema aliyetangaza nia ya kuwania Urais kupitia chama hicho

Nitaboresha sifa za kujiunga na kada ya ualimu tofauti na ilivyo sasa. Yaani watu wenye ufaulu mzuri ndio watakaopewa kipaumbele cha kuwa walimu.

Pia, kwa kuwa nitakuwa nimerekebisha mfumo mzima wa elimu kwa kujikita kwenye elimu ya vitendo zaidi, naamini nitalivusha taifa kwa kuzalisha watu wengi wenye maarifa, na sio elimu ya madaftari na vitabu.

Mimi naamini kuelimika ni kupata maarifa na sio kujikusanyia vyeti.

5. UHUSIANO WA JESHI LAPOLISI NA RAIA

Ni ukweli ulio dhahiri kwamba mahusiano ya jeshi letu la polisi na raia sio wa kujivunia. Hii ni kutokana na ukweli kwamba polisi wetu wanafanya kazi katika mazingira duni sana kiasi amabacho baadhi yao wanalazimika kujiingiza katika vitendo visivyofaa kama vile rushwa.

Imefikia mahali imezoeleka kwamba kuingia kituo cha polisi ni bure, lakini kutoka ni pesa. Hili halikubaliki.

Mazingira magumu ya polisi yanawafanya wasipambane na majambazi kwa nguvu zao zote na hivyo kufanya majambazi kuendelea kuwepo hali inayodumaza uzalishaji katika baadhi ya sekta katika uchumi wetu kama vile sekta ya usafirishaji, uvuvi na baadhi ya biashara.

Nitaimarisha jeshi la polisi kwa kuwajengea makazi bora ya kuishi, kuboresha maslahi yao ikiwa ni pamoja na motisha kwa watakaokuwa wanafanya kazi za kuhatarisha maisha yao kama vile kupambana na majambazi.

Katika hili, nitapiga marufuku mapato yote ya makosa ya usalama barabarani kuingia moja kwa moja serikalini, badala yake yatakuwa mapato ya jeshi la polisi ambayo yatatumika kuboresha maslahi yao.

Lakini pamoja na hayo pia, nitahakikisha hakuna tabia ya kuwabambikia raia makosa wasiostahili.

Hali hii ikiboreka naamini tutainua uchumi wetu. Watu wetu watakuwa huru kuzalisha usiku kucha kama watakuwa na uwezo wa kufanya hivyo bila kuogopa majambazi kwa kuwa polisi wetu watakuwa wakifanya kazi kwa juhudi kubwa na weledi, wakijua kuwa maislahi yao ni bora.

6. MASLAHI YA MAJESHI YETU

Pamoja na kuyatazama maslahi ya jeshi la polisi, pia nitaboresha pia maslahi ya maaskari wetu kati majeshi yetu mengine kama vile Jeshi la Wananchi, Magereza Uhamiaji na Usalama wa Taifa na Zimamoto.

Natambua kazi kubwa na ya weledi wanayofanya, hivyo nitayaboresha maslahi yao. Wakiniamini, nitawavusha.

7. UZALISHAJI KUPITIA JESHI LA KUJENGA TAIFA

Nitalifanya jeshi la kujenga taifa kuwa jeshi maalum la uzalishaji wa chakula nchini.

Badala ya kuwa jeshi la kufunza vijana na kuwaweka kwa miaka zaidi ya mitatu wakisotea ajira kwenye majeshi mengine kama jeshi la wananchi, polisi au magereza.

Nitalifanya jeshi la kujenga taifa liwe ajira ya vijana kwa ajili ya kilimo. Nataka tuilishe Afrika kwa sababu ardhi ya kutosha tunayo, maji tunayo na utashi wa kisiasa kama rais ninao.

8. GHARAMA ZA UENDESHAJI SERIKALI

Kwa sera yetu ya chama ya utawala wa majimbo, nitalisimamia jambo hilo kwa weledi mkubwa sana ili kuleta maendeleo ya haraka.

Nitapunguza gharama za kuendesha serikali kwa kufuta vyeo visivyo na umuhimu wowote zaidi ya kuongeza tu mzigo kwa serkali ambao ni mzigo kwa wananchi.

Nitafuta vyeo vya wakuu wa mikoa na wilaya ambavyo kimsingi havina tija kwa taifa kwa kuwa ni vyeo vya kisiasa ambavyo sasa vimejaza makada na wapambe wa wakubwa.

9. WANANCHI WA KIPATO CHA CHINI

Nataka kuwainua wananchi wa kipato cha chini ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiitwa majina ya udhalilishaji kwamba ni wanyonge.

Kwa kuwaita wanyonge, ndio maana watawala wetu wamekuwa wakiwanyonga kwa kuwatumia kama daraja la kuwavusha wakati wa kuomba kura, na baada ya hapo kuwatwisha mzigo mkubwa wa gharama za maisha bila kuwakumbuka.

Nitarasimisha maeneo yao haraka iwezekanavyo ili kuwapatia hati na kuyaongezea thamani maeneo hayo. Hii itawasaidia kupata mikopo katika taasisi za kibenki.

Nitaondoa mara moja usumbufu uliopo wa kurasimisha maeneo ya wananchi wa kipato cha chini. Katika utawala wangu sitaki kuwa na wananchi wanyonge.

Nitawainua wananchi wenzangu katika uchumi wao. Kwa maana hiyo nitaondoa kodi kwa wafanyabiashara wenye kipato
kisichofikia milioni tano kwa mwaka ili kuwajengea mazingira rafiki ya kuinua kipato chao.

10.MAMLAKA YA MAPATO (TRA)

Mamalaka yetu ya mapato, ndicho chombo chetu kikuu cha ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Natambua kazi kubwa wanayoifanya pamoja na changamoto nyingi wanazokutana nazo.

Natambua kwa sasa wanafanya kazi kwa ‘pressure’ kubwa sana. Nitaiboresha TRA.

Kwanza nitaunda kikosi kazi kwa ajili ya kutoa elimu kwa walipa kodi kuliko ilivyo hivi sana. Kikosi hicho pia kitahusika na ukusanyaji wa madeni sugu pamoja na kuwajengea mazingira rafiki ya ulipaji kodi.

Watawafuatilia wadaiwa sugu na wale wanaokwepa kodi kwa makusudi ili kuwaelimisha na hatimaye kuwafanya kulipa kodi. Nitahakikisha 5% ya madeni sugu na yale yanayokuwa yameibuliwa na kikosi kazi hiki nitakachounda inakuwa ni sehemu ya motisha kwa wafanyakazi wote wa TRA.

Hii itaondoa rushwa miongoni mwa watendaji wa TRA na pia kuongeza bidii na moyo wa kufanya kazi.

11.SEKTA YA UTALII

Nitaboresha upya sekta ya utalii. Siridhishwi na utendaji kazi wa sekta nzima ya utalii. Siridhishwi na namna tunavyojitangaza kama taifa.

Udanganyifu wa mataifa jirani kwamba mlima Kilimanjaro uko kwao, ni matokeo ya utendaji mbovu katika sekta hii ya utalii.

Nitalishughulikia jambo hilo, ili kuimarisha mapato ya utalii na kulinda vivutio vetu. Tunakosa mapato mengi. Kwa mujibu wa takwimu za shirika/baraza la safari na utalii za dunia (World Travel and Tourism Council (WTTC) utalii wa bara la Africa ulikuwa kwa kiwango cha wastani wa 5.6% kwa mwaka 2018 kulinganisha na makadirio ya dunia ya wastani wa 3.9%.

Hii inaonyesha utalii wa bara la Afrika unakuwa kwa kasi kubwa. kwa mujibu wa shirika la utalii la Umoja wa Mataifa (United Nations World Tourism Organization), Afrika ilipata watalii milioni 67 mwaka 2018.

Nchi iliyoongoza kwa Afrika ni Morocco (12.3m) ikifuatiwa na Misri (11.3m). Tanzania tulipata watalii milioni 1.5 tu. Hili halikubaliki kulinganisha na vivutio vya utalii tulivyo navyo.

12. UVUVI, MIFUGO NA KILIMO

Kwangu mimi sekta hizi ni muhimu sana kwa taifa na ndio zinaajiri watanzania wengi wa kipato cha chini. Nitaboresha sekta ya uvuvi kwa kuwa kama taifa tunapoteza sana.

Kwanza, nitaimarisha ulinzi kwa wavuvi wetu wadogo wadogo ambao wengine wamekuwa wakivamiwa na majambazi.

Lakini pia nitaimarisha soko la mazao yote ya samaki ili kuinua uchumi wa wavuvi. Nitaweka mazingira rafiki ya mikopo kwa zana za uvuvi kuwawezesha wavuvi wadogo wadogo kuvua kwa ubora na kwa mfumo wa kisasa.

Pili, nitaboresha sana sekta ya mifugo. Nalenga kujenga kiwanda kikubwa cha nyama kinachoweza kuihudumia Afrika Mashariki kwa sababu sisi tunaongoza kwa kuwa na mifugo mingi katika ukanda wetu huu.

Nitaimarisha pia soko la ngozi na mazao nmengine. Sitakubali makazi ya watu kuendelea kurundikiwa ngozi zinazotoa harufu kali kwa watu kama ilivyo katika maeneo ya Mbagala rangitatu jijini Dar es Salaam.

Aidha nitaimarisha sekta ya kilimo. Kwa bahati nzuri sana tumekuwa tukipata mvua za kutosha mara nyingi mpaka kutusababishia mafuriko.

Tutajenga mabwawa makubwa ya uvunaji maji ili kuyatumia maji hayo kwa kipindi chote cha mwaka.

Mabwawa hayo yatajengwa na serikali kuu, na kukabidhiwa kwa serikali za majimbo husika ili wananchi waweze kuyatumia kwa ajili ya umwagiliaji.

Sasa kwa vile maeneo mengi yakiwemo mashamba ya wananchi yatakuwa yamerasimishwa, itakuwa rahisi kwa wananchi kuchukua mikopo kwenye taasisi za kibenki na kujinunulia mashine za umwagiliaji na zana nyingine, hivyo kulima kwa kipindi chote cha mwaka.

13. SEKTA YA MADINI NA NISHATI
Kwanza kabisa nitalitoa taifa kwenye mikataba mikubwa ya kimataifa kama MIGA CONVENTIONS.

Hii itasaidia kuboresha mikataba ya madini na wawekezaji bila hofu ya kushitakiwa kwenye mahakama za kimataifa.

Ninalenga kuipitia mikataba yote ya madini kwa kuwa sijaridhishwa kabisa na kilichofanyika katika sekeseke la ACACIA.

Nitapandisha kiwango cha umiliki wa hisa za serikali katika mikataba hiyo kuliko hivi sasa. Lengo ni kutengeneza mazingira ya wote kufaidi (win win situation).

Silengi kugombana na wawekezaji bali kuzilinda rasilimali za nchi yetu kwa faida yetu na vizazi vyetu.

Nitahakikisha kila penye migodi panakuwa na maendeleo ya moja kwa moja yanayotokana na vipaumble vya wananchi (community based development), mfano barabara, afya, umeme, maji nk. Katika utawala wangu haitasikika hata mara moja kwamba wananchi wanaozunguka mgodi wamekufa kwa sababu ya sumu za migodini au utiririshaji wa maji katika makazi yao.

Hii itasaidia kulinda uhusiano kati ya wananchi na wawekezaji.

Nalenga pia kuwajengea mazingira rafiki wawekezaji wa ndani ili kupunguza rasilimali zetu kwenda nje (Reduce outflow of resources).

Pia, nitahakikisha kama nchi tunakuwa na uwezo wa kuprocess mchanga wa madini maarufu kama makinikia ambao umekuwa ukipelekwa nje.

Tuna makaa ya mawe ya kutosha kuzalisha kiwango cha joto kinachohitajika cha 15000c. kinachokosekana kwa sasa ni utashi wa kisiasa na dhamira ya dhati na uzalendo wa kweli. Mimi nitafanya hivyo.

14. RUSHWA

Bado rushwa ni adui mkubwa sana wa taifa letu. Ni kweli kuna jitihada kidogo zimefanyika. Lakini rushwa iliyopo sasa ni yale wanaoujua kula na watawala au walio vipenzi wa watawala.

Au katika taasisi za serikali ambazo wafanyakazi wanafanya kazi kubwa lakini wanaona kama vile hawathaminiki kwa kuboreshewa maslahi yao.

Sasa kwa sababu rushwa ni mfumo, tutapitisha sheria kali dhidi ya wala rushwa na kuhakikisha zinatekelezwa bila ubaguzi.

15.SEKTA YA MICHEZO

Nitaboresha sekta ya michezo. Katika hili nitahakikisha kila serikali ya jimbo inakuwa na viwanja bora vya michezo kuliko ilivyo hivi sasa ambapo viwanja vilivyopo vimeporwa katika umiliki na hali yake ni mbaya.

Lakini pia, ninalenga kuwaruhusu wanamichezo kuwa na uraia wa nchi mbili. Hii itasaidia kuwafanya vijana wetu wengi walioko nje ya nchi waweze kuzichezea timu zetu za taifa.

Mfano katika mchezo wa soka pekee tuna vijana zaidi ya 20 walioko nchi mbali mbali duniani ambao kwa sababu tu ya uraia wameshindwa kulitumikia taifa letu kwa kuwa wengi wao tayari wana uraia wa mataifa hayo wanakocheza soka.

Kumbuka michezo kwa sasa ni ajira, lakini pia ni idara muhimu katika kutangaza utalii wa nchi na hivyo kuliongezea taifa mapato.

Nitaweka mkakatai maalumu kwa ajili ya kuwawezesha vijana wetu kufanya majaribio katika nchi za nje katika michezo mbali mbali.

Hii itakuwa kampeni ya nchi nzima. Nataka watanzania wajue kwamba kila Mtanzania ni Watanzania. Yaani palipo na mafanaikio ya mmoja wetu ni mafanikio yetu sote kama taifa.

Wenzetu wako hivyo. Nitaondoa ubinafsi na ukiritimba ulipo katika sekta ya michezo nchini.

16. MAADILI YA TAIFA

Taifa letu linakabiliwa pia na changamoto ya maadili, sio kwa vijana tu bali hata watu wazima.

Hii inasababisha taifa kutembea kwenye laana ya Mungu kwa sababu ya dhambi.

Nitapiga marufuku kabisa mavazi ya nusu uchi, shughuli za uchangudoa na ushoga zinazofanyika japo sio rasmi, lugha za matusi hadharani pamoja na uchafu mwingine.

Nataka kulirejesha taifa katika baraka za Mungu na sio kufungamana na misingi ya kuzimu. Kuwa na taifa lenye hofu ya Mungu ili tuweze kubarikiwa.

17.HALI YA KISIASA.

Nitajenga taifa lenye misingi bora ya kisiasa. Nitaimarisha demokrasia ya kweli katika taifa.

Taifa lenye kukosoana bila kuuana, taifa lenye kupingana kwa hoja bila kupigana. Katika hili nitapunguza pia mamlaka ya rais ili kuliweka taifa katika hali ya kupatana na kuondoa matamko yenye hali ya maamrisho.

Majadiliano hujenga umoja wakati maamrisho hujenga hofu. Taifa hili ni letu sote. Pia nitahakikisha rasimu ya katiba mpya ilyoiwekwa kapuni na watawala wetu inafufuliwa na kupitishwa mara moja kuwa katiba kwa kuwa naamini yale ndio yalikuwa mawazo ya wananchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!