Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Upinzani una faida kubwa kwa Nchi – Aman Karume
Habari za SiasaTangulizi

Upinzani una faida kubwa kwa Nchi – Aman Karume

Aman Abeid Karume, Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Spread the love
DK. Aman Abeid Karume, rais mstaafu wa Zanzibar amesema, kukosekana kwa wawakilishi wa vyama vya upinzani bungeni na  Baraza la Wawakilishi, kunachochea Serikali kuwa dhaifu kusimamia kazi zake. Anaripoti Erasto Masalu, Zanzibar … (endelea).

Amesema, hata kinachoonekana sasa ndani ya Serikali ya Zanzibar, kwa kiasi kikubwa, msingi wake mkuu, ni kutokuwapo kwa uwakilishi wa upinzani kwenye Baraza la Wawakilishi na serikalini katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Amesema, “malalamiko ya sasa juu ya kuwapo kwa madai ya ufisadi, ubadhilifu na wizi wa fedha za Serikali Visiwani Zanzibar, kwa kiasi kikubwa, yanatokana na kukosekana kwa upinzani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.”

Ameongeza, katika nchi inayoongozwa na mfumo wa vyama vingi, kuruhusu chama kimoja kutawala kila kitu, kunawafanya wajisahau na hivyo, kuruhusu kuwapo kwa mwanya wa  vitendo vya wizi, ubadhilifu na ufisadi wa mali za umma.

Amesema, “…hivi karibuni nimesoma kwenye magazeti, kwamba Rais Mwinyi (Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk. Alli Hussen Mwinyi) anaeleza, tena kwa masikitiko, kwamba kila alipopagusa anakuta kuna mushkeri. Haya ndio matunda ya kukosekana kwa upinzani ndani ya serikali iliyopita.

“Tumefika hapo kwa sababu, wale wakosoaji hawakuwepo. Tulikosa Checks and balances (mizania ya mgawanyo wa madaraka). Umeshafahamu? Hayo ndio matunda, kwamba Checks and balances, ni muhimu sana,” anaeleza rais huyo wa sita wa Zanzibar.

Dk. Karume ambaye ndiye mwasisi wa mwafaka wa Zanzibar, uliozaa serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUKI), alikuwa akirejea kilichotokea Visiwani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Katika uchaguzi huo, kilichokuwa chama kikuu cha upinzani wakati huo – The Civic United Front (Chama cha Wananchi), pamoja na mgombea wake wa urais, Maalim Seif Sharif Hamad, waliamua kutoshiriki uchaguzi wa marudio wa Machi 2016.

Hatua ya Seif na wenzake, kususuia uchaguzi huo, kuliwafanya kujiondoa rasmi kwenye Baraza la Wawakilishi na serikalini.

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Maalim Seif na chama chake, waliamua kuchukua hatua hiyo, baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kuamua kufuta uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015 na matokeo yake, kinyume na sheria na taratibu za kuendesha chaguzi.

Jecha alidai kuwa alifikia maamuzi ya kufuta uchaguzi, baada ya kugundua kuwa Maalim Seif, aliiba kura. Alisema, ZEC iligundua kuwapo kwa kura 15,000 za ziada, nje ya zile zilizochapishwa.

Maalim Seif amekana madai hayo. Amemtuhumu Jecha kuendesha uchaguzi kwa kutanguliza maslahi ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Karume ni mtoto wa aliyekuwa rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume. Sheikh Karume, alifariki dunia tarehe 7 Aprili mwaka 1972, kwa shambulio la risasi.

Rais mstaafu Karume anasisitiza kuwa kitendo cha Maalim Seif kukaa kando, hakikusaidia Zanzibar.

Maalim Seif Sharrif Hamad Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa

Anasema, “wao kukaa kando, ni unfortunately (bahati mbaya) kwa maendeleo ya nchi yetu.  Kwa sababu wameiacha hali imekuwa tete sana, hofu ilikuja tena, wengine wakaona tunarudi kulekule. Nafurahi sasa, Maalim Seif ameamua kuingia tena serikalini.”

Amesema, vyama vya upinzani vina umuhimu mkubwa katika kusaidia Serikali kujisahihisha na kudumisha utawala bora, na kwamba kinachotokea sasa Zanzibar, ni matunda ya kutokuwapo kwa upinzani imara katika kipindi kilichopita.

Hata hivyo, rais Karume hakuzungumzia lolote kuhusiana na kilichotokea Bara katika uchaguzi mkuu uliopita, lakini kwa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (NEC), hakutakuwapo Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, jambo ambalo linaweza kuchangia kutokea yale ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Bunge, ili kuwapo Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, ni sharti upinzani upate asilimia 12.5 ya viti vya Bunge.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!