Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Ujinga, udikteta unatesa Afrika
Makala & Uchambuzi

Ujinga, udikteta unatesa Afrika

Bobi Wine
Spread the love

RAIA wa nchi za Afrika wanazo sababu nyingi za kutamani na hata kupanga kubadili tawala zao zilizoasi. Ni mabadiliko ambayo yatawezesha kufikia kilele cha uhuru na haki zilizominywa na watawala hao. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Bara la Afrika limechongwa katika taswira hasi dunia, taswira hiyo hujengwa na baadhi ya watawala ambao kwao vichwa vyao ndio Katiba za nchi zao. Mifumo ya tawala zao inalenga kukidhi matakwa ya fikra zao pekee.

Baadhi ya viongozi wa mataifa hayo wanakosa sifa ya kuwa viongozi wa wananchi na badala yake kubaki katika kundi la viongozi wanaoongoza kwa ajili yao na vizazi vyao pekee kwa kutumia rasilimali za nguvu za wanananchi.

Bakora kubwa inayotumiwa na viongozi wa Afrika ni Katiba mbovu ambazo ziliandaliwa kwa sababu maalumu za kulinda fikra na hisia zao pale wanapotaka kuchukua hatua kinyume na matakwa ya wananchi waonaowaongoza. Vitisho na matukio ya kuogofya yamekuwa sehemu ya tawala zao.

Hata katika zile nchi ambazo Katiba imetoa mwanya kwa baadhi ya mambo kutendeka, viongozi hao kwa dhamira ya kutumikia fikra zao, bado wameendelea kuminya mianya hiyo na kusababisha machungu zaidi kwa raia wake.

Afrika ina safari ndefu, usalama wa safari hiyo ili kufikia nchi ya ahadi utatokana na utayari wa raia waliodhamiria kukataa kuminywa ama kubanwa katika mambo yao ya msingi ikiwa ni pamoja na uhuru wa kuongea, uhuru wa kiuchumi na demokrasia ya kweli.

Kukosekana kwa vitu hiyo vitatu katika nchi yoyote duniani kunatoa uhalali wa kuanza kwa harakati ili kuitafuta haki hiyo. Nchi kadhaa Afrika zimekuwa zikipuuza sauti za wananchi, watawala wamekuwa na tabia ya kubeza malalamiko na hata kutoa majibu ya kebehi na mepesi kwa wananchi jambao ambalo hutia petroli hisia za wananchi na hatimaye kulipuka.

Matatizo ya Afrika yanafanana kwani yote yameegemea kukosekana kwa uhuru wa kuzungumza, uhuru wa kiuchumi pamoja na demokrasia ya kweli, kutokana na kukosekana vitu hiyo, sababu za maandamano katika mataifa ya Afrika pia zinafanana zikilenga maisha bora, uhuru wa kuzungumza na demokrasia ya kweli.

Afrika ina mifano michache ya raia wake waliochoka kudhulumiwa, kuminywa uhuru wao, kunyanyaswa, kupotezwa na hata kuuawa bila sababu na hatimaye kuchukua hatua kuzuia uvunjaji huo wa haki.

Miongoni mwao ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ethiopia, Misri, Kenya, Uganda, Cameroon ambapo kumekuwepo na maandamano na hata mauaji ya wenyewe kwa wenyewe kutokana na serikali zao kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Mivutano ya madaraka na utaratibu mbovu unaosimamiwa na vyama tawala Afrika imekuwa ikitoa msukumo hisia za kufanya maandamano yanayolenga kubali mfumo kandamizi.

Afrika na baadhi ya watawala wake wamekuwa wakitumia tume za chaguzi ili kuendelea kuwepo madarakani. Haya yanadhihiri katika nchi mbalimbali ambapo tume hizo zimekuwa zikipendelea mamlaka zilizopo madarakani jambo ambalo mara nyingi limekuwa likiibua vuruga na hata mauaji.

Haya yameweza kudhihiri miongoni mwa nchi kadhaa za Afrika ikiwemo Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kusababisha vurugu.

Mfano polisi wa kisumu nchini Kenya baada ya matokeo ya uchaguzi, walilazimika kutumia nguvu kuwakabili wafuasi wa Muungano wa NASA chini ya Raila Odinga wakiamini mgombea wao kuibiwa kura.

Hatua hiyo ilitokana na Wakenya kutokuwa na imani na tume yao ya uchaguzi (IEBC). Vurugu hizo zilitokea baada ya Odinga kutuhumu kuibiwa kura huku tume ikinyooshewa kidole.
Sehemu kubwa ya Afrika chaguzi zake haziendeshwi kwa uhuru na haki, upungufu huu unachagizwa na udhaifu wa Katiba na utashi wa tawala zinazofuata sheria.

Inapotokea jitihada za viongozi wa upinzani ama taasisi za haki pamoja na msukumo kutoka kwa raia, viongozi waliopo madarakani hufanya jitihada za waziwazi kupiga hatua nyuma bila kujali athari zake.

Utayarishwaji mbovu wa uchaguzi, ndio unatoa msukumo mkubwa wa kuingia kwenye misukosuko. Baadhi ya viongozi wa Afrika hawaheshimu Katiba, lengo kuu ni kuendelea kusalia madarakani.

Chaguzi zinachukuliwa na watawala hao kama kiini macho ili kukidhi matakwa ya kimataifa, basi! Wengine wamekuwa wakibaki madarakani kwa hila.

Angalia DRC chini ya Rais Joseph Kabila alivyoliweka mashakani taifa hilo. Haki ya wananchi wa Kongo ilikuwa kupata kiongozi mpya tangu Desemba mwaka jana, sasa ameinua mikono.

Rais Kabila anaendelea historia chafu ya DRC tangu kupata kwake Uhuru mwaka 1957, nchi hiyo haijatuli. Msingi wa machafuko ya mara kwa mara ni kutokuwepo kwa utayari wa viongozi kufuata matakwa ya Katiba.

Ukiiangalia Uganda nayo imetumbukia kwenye mfano mbaya wa nchi za Afrika katika kiminya Uhuru wa kuzungumza, ukuru wa demokrasia ya kweli na hata kusiginya Katiba. Sakata la Bobi Wine ni kielelezo halisi ya siasa za ovyo Uganda.

Tangu mwaka 1986 Uganda imekuwa chini ya Rais Yoweri Museveni, rais huyu amekuwa akiichezesha Katiba ili kulinda matakwa yake. Msuguano na maandamano Uganda yanatiwa msukumo na utashi wa Rais Museven kutaka kuendelea kusalia madarakani ‘milele’.

Fikra na hisia za Rais Museven ni kwamba, Uganda mpaka sasa haina mtu sahihi wa kuiongoza isipokuwa yeye, harakati zake za kuondoa kikwazo cha umri wa kugombea urais zinaelekea kufanikiwa, lengo kuu likiwa ni kupata mwanya wa kugombea urais mwaka 2021.

Mwendo ni ule ule kwa Serikali ya Rwanda ambapo tayari Rais Paul Kagame aliyeingia madarakani mwaka 1994 baada ya mauaji ya Kimbari, anaiongoza nchi hiyo kwa awamu ya tatu. Hii ni baada ya kubadili Katiba ya nchi hiyo ili kumpa mwanja wa kuendelea kusalia madarakani.

Uchochezi mkubwa wa machafuko na kuminywa haki kidemokrasia huasisiwa na Katiba ambayo ndio huzaa tume za uchaguzi dhaifu. Afrika yetu inaangamia kila kukicha kwa utovu wa viongozi juu ya Katiba zao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 28 watumishi UDSM yaliwa na nzige, madumadu

Spread the loveGEORGE Francis anasikitika; anatembea akiwa na mawazo mengi, hajui la...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nimekumbuka Samia wa miaka 3 iliyopita

Spread the loveWAKATI naandaa makala ya safu hii wiki hii, nimejikuta nakumbuka...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Hakuna fedha za Rais

Spread the loveKUNA mambo machache mazuri ya kujifunza kutoka kwa Margaret Thatcher,...

error: Content is protected !!