Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Uhamiaji wakabidhiwa nyumba 103, Majaliwa awapa ujumbe
Habari Mchanganyiko

Uhamiaji wakabidhiwa nyumba 103, Majaliwa awapa ujumbe

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea funguo, kutoka kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kama ishara ya kukabidhiwa nyumba 103, kwa akijili ya Makazi ya Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nichini, zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Juni, 2, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Spread the love

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameitaka Idara ya Uhamiaji kutambua wajibu wao wa kutoa huduma iliyobora na inayokidhi matarajio ya wateja ambao ndiyo waajiri wao. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Majaliwa ametoa wito huo leo Jumanne tarehe 2 Juni 2020 wakati akiikabidhi Wizara ya Mambo ya Ndani ya nyumba 103 zenye gharama ya zaidi ya Sh. 5 bilioni kwa ajili ya makazi ya Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji.

Nyumba hizo zimejengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Iyumbu jijini Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi ulitolewa na Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.

Taarifa iliyotolewa kwa umma na ofisi ya waziri mkuu imesema, baada ha ya kukabidhi nyumba hizo, Majaliwa amesema, makazi hayo yawe chachu kwa Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nchini katika kutambua wajibu wao wa kutoa huduma iliyobora na inayokidhi matarajio ya wateja ambao ndiyo waajiri wao.

“Uamuzi huu wa Mheshimiwa Rais ambao leo hii tunashuhudia utekelezaji wake kupitia makabidhiano haya, utasaidia kuwafanya Maafisa na Askari wa Uhamiaji kukaa katika makazi yao tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo waliishi uraiani,” amesema.

Kamishina Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala, akionesha ishara ya funguo, baada ya kukabidhiwa nyumba 103, kwa akijili ya Makazi ya Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nichini, zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Juni, 2, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Amesema, “Ni ukweli usiofichika kuwa makabidhiano ya nyumba hizi baina ya Shirika la Nyumba la Taifa na Idara ya Uhamiaji ni moja kati ya vielelezo vya utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ya kuwapatia Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nyumba 103.”

Pia, Waziri Mkuu amesema “Nyote mtakubaliana nami kwamba leo ni siku muhimu kwa sekta ya nyumba kwani ujenzi wa nyumba za namna hii ni muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwenye Taasisi za Serikali sambamba na kuboresha ufanisi wa wafanyakazi wetu.”

“Vilevile, utekelezaji wa mradi huu umetoa ajira zipatazo 1,000 ikiwa ni sawa na ajira 800 za mafundi na ajira 200 kwa watoa huduma za chakula yaani mama lishe.”

“Upatikanaji wa ajira hizo umechangia kuongeza kipato kwa walengwa na kusaidia kujikwamua dhidi ya umaskini,” amesema

Amesema ujenzi wa majengo hayo ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/20 inayosisitiza ujenzi wa majengo ya ofisi na makazi kwa watumishi wa umma kwa lengo la kuipunguzia Serikali gharama kubwa ya kodi ya pango pamoja na kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa watumishi wa umma katika kuwahudumia Watanzania.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Shirika la Nyumba la Taifa, kuendelea na kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba za makazi pamoja na biashara kwani lengo la Ilani ya CCM ya mwaka 2015 ni kuliwezesha NHC kuwa Mwendelezaji Miliki Mkuu.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema watendaji wa shirika hilo wanapaswa kuongeza kasi ya ukusanyaji kodi ili kuongeza mapato ya shirika.

“Serikali kwa upande wake, itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa shirika katika kutatua changamoto zinazokabili utekelezaji wa malengo ya shirika hili,” amesema

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka pamoja na kufanikisha maboresho mbalimbali kama vile Uhamiaji Mtandao ambapo sasa huduma za pasipoti, vibali vya ukaazi, viza, usimamizi na udhibiti wa mipaka vinafanyika kwa njia ya kielektroniki.

“Utekelezaji mzuri wa mageuzi ya Uhamiaji Mtandao umewezesha idara hii kupata tuzo ya ushindi wa pasipoti yenye ubora duniani kwa mwaka 2019,” amesema

Waziri Mkuu amesema ushindi huo, umelipatia sifa na heshima kubwa Taifa Kimataifa.

“Halikadhalika, nimefurahishwa na taarifa kuwa ujenzi wa Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji, Dodoma nao unaendelea vizuri. Ninawahimiza endeleeni hivyo kwa mustakabali wa ustawi wa Taifa letu.”

Awali, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dk. Anna Makakala aliishukuru Serikali kwa kuwezesha Idara ya Uhamiaji, kupata nyumba 103 za makazi kwa ajili ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji kwani hatua hiyo ni kielelezo cha vipaumbele vya Serikali katika kuboresha makazi ya askari wa vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi kwa ujumla.

“Aidha, tunalipongeza pia Shirika la Nyumba la Taifa, kwa kubuni mradi mkubwa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya makazi ya wananchi kwa kujenga na kuuza nyumba kwa bei nafuu, ambapo nasi tumekuwa wanufaika wa mradi huu. Gharama za nyumba 103 za makaazi ya watumishi wa Idara ya Uhamiaji, ni kiasi cha Sh. 5.306 bilioni,” amesema

Amesema upatikanaji wa nyumba hizo utasaidia Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji kuishi katika maeneo yao maalum, badala ya ilivyokuwa hapo awali ambapo walilazimika kutafuta nyumba za makazi uraiani.

“Sambamba na hilo, itasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu, kwani itakuwa ni rahisi kuwapata askari walio katika eneo moja mara wanapohitajika,” amesema

Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi,Jenerali Venance Mabeyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Dk. Maulid Banyani, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo  na Maafisa wengine wa Serikali.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

error: Content is protected !!