Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Uchaguzi mkuu 2020: Wanawake wajitokeza, rasimu ya Warioba yakumbukwa
Makala & Uchambuzi

Uchaguzi mkuu 2020: Wanawake wajitokeza, rasimu ya Warioba yakumbukwa

Halima Mdee
Spread the love

JUMATANO ya tarehe 28 Oktoba 2020, Watanzania wenye sifa za kupiga kura, watakuwa na fursa ya kujitokeza kuwachagua madiwani, wabunge na Rais. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Huu ni uchaguzi wa kwanza tangu uliporejea mfumo wa vyama vingi na mwaka 1992 na uchaguzishirikishi kufanyika mwaka 1995 kufanyika katikati ya wiki yaani Jumatano kwani mara zote ulikuwa ukifanyika Jumapili.

Tayari vyama mbalimbali vya siasa nchini, vinaendelea na michakato ya kuwapata wagombea udiwani, ubunge, uwakilishi na urais huku ikishuhudia kwa mara ya kwanza, ongezeko la wanawake.

Hata hivyi, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) ikisema, ili kuwe na mabadiliko na usawa, kunahitajika kuhitimishwa kwa mchakato wa katiba kwa kuanzia na Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu Joseph Warioba.

Wanawake wamejitokeza kwa wingi katika vyama mbalimbali kugombea nafasi za udiwani, ubunge na urais, ikiwa ni tofauti na chaguzi zilizopita ambapo mwitikio ulikuwa hafifu.

Mwitikio huo wa wanawake umechagizwa na baadhi ya taasisi kutoa elimu mbalimbali za kuhamasisha usawa wa kijinsia katika makundi mbalimbali.

Mmoja wa mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Adelina Msafiri anasema, inatia faraja kuona wanawake wengine wamejitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.

“Tunachokiomba tu, sisi wanawake wenyewe tuungane mkono kwani mimi huwa sielewi kwa nini sisi wanawake tuko wengi lakini tukigombea tunashindwa lakini sasa mwaka huu tupeane nguvu,” anasema Adelina

Rasimu ya Warioba yaikumbukwa 

Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk. Ananilea Nkya anasema, Tanzania ni nchi ya uongozi ambapo nafasi za uongozi huwa ni za wanaume na wanawake kwa pamoja.

Hata hivyo, Dk. Ananilea anasema, wingi huo wa wanawake kujitokeza unachangiwa kwa sehemu kubwa na juhudi ya mashirika mbalimbali kutoa elimu kwa wanawake ili waweze kushiriki uchaguzi na kuwa viongozi.

“Mwanamke asipendelewe kutokana na yeye kuwa mwanamke, wananchi wanahitaji kupata viongozi watakowawatumikia bila kujali ni mwanamke au mwanaume,” amesema Dk. Ananilea.

Dk. Joyce Bazira Mtaalamu wa Mawasiliano akitoa mada kwa waandishi wa habari

Mkurugenzi huyo wa zamani wa Tamwa, amesema ili kuwepo kwa mabadiliko na uwiano sawa kuliko kubaki kama ilivyo, vyama vya siasa vinapaswa kuhakikisha vinahitimisha mchakato wa katiba kwa kuanzia Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji mstaafu Joseph Warioba.

Anasema, katika rasimu hiyo, kulikuwa na mapendekezo ya asilimia 50 kwa 50 katika majimbo ya uchaguzi “kuliko sasa, wanaume wataendelea kuwa wengi na hata katika uchaguzi huu ndiyo kitatokea, vyama vionyeshe vitakwenda kufanya nini juu ya mabadiliko ya katiba kwa kuanza na Rasimu ya Jaji Warioba.”

“Tena rasimu hiyo ilisema itakuwa na wabunge wachache lakini kwa sasa wabunge wataendelea kuwa wengi na wenye fedha ndiyo watakuwa wanapata fursa kwani fedha wanazo. Ili tuhitimishe hili tufanye mabadiliko ya Katiba kwa kuangalia mapendekezo yaliyomo kwenye rasmu ya Jaji Warioba,” anasema

Mchango wa vyombo vya habari

Mtaalamu wa masuala ya mawasiliano, Dk. Joyce Bazira anasema vyombo vya habari, vinamchango mkubwa wa kuhakikisha mfumo dume unapungua kama siyo kuondoka.

Dk. Bazira alitoa wito huo wakati akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari hivi karibuni katika mradi unaofadhiliwa African Women Development Fund wa AWDF wenye kauli mbiu ya ‘wanawake sasa.”

Anasema, habari zinazoandikwa katika magazeti, mitandao ya kijamii au televisheni zinapaswa kuwa na mtazamo chanya na kuepuka kuwaweka nyuma katika kila mambo.

Waandishi wa Habari

Dk. Bazira anasema, vyombo vy habari vikiwa na uelewa chanya wa masuala ya wanawake, kutakuwa na fursa kubwa ya habari kuhusu wanawake kupewa kipaumbele na kutokutumika kama kujaza nafasi.

“Vyombo vya habari, vina wajibu wa kuweka uelewa chanya wa masuala ya wanawake kama kuandika habari zenye mafanikio yaliyofanywa na wanawake walioshika au kuwahi kushika madaraka,” anasema Dk. Bazira

“Wanawake wanakuwa waoga kushiriki katika siasa kama uchumi, elimu na vikwanzo mbalimbali. Waandishi wanapaswa kwenda mbele zaidi kujua nini kiko nyuma ya woga huo,” anasema mtaalamu huyo

Bawacha: Wanaume mtuunge mkono

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho tarehe 4 Agosti 2020 anasema, chama hicho kimehakikisha wanawake wanapewa fursa ikilinganishwa na mwaa 2010.

Mdee ambaye amekuwa mbunge wa Kawe kwa miaka kumi mfululizo kuanzia 2010-2020 amesema, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, wanawake waliojitokeza walikuwa watatu na yeye pekee akaibuka mshindi jimbo la Kawe.

“Tunawajibu wa kuhamaisha wanawake wagombee ili kuhakikisha tunashinda. Kura za maoni ngazi udiwani na ubunge tumefanya vizuri, kilichobaki tunapaswa kuhakikisha tunafanya vizuri.”

“Ushindi wa kura za maoni ngazi ya ubunge na udiwani si kazi ya kubahatisha. Mwaka 2010 tulikuwa watatu tunagombea majimbo, nikachomoza mimi. 2015 tulipewa tisa tukachomoza sita,” anasema Mdee.

Mdee anatumia fursa hiyo kuwaomba wanaume, “mtuunge mkono wanawake walioshinda kura za maoni, tunaomba mtuunge mkono pia.”

Anasema, Bawacha limekwisha zindua, Sera ya wanawake wa Chadema ambapo ni “chama cha kwanza Tanzania na Afrika kutoa msimamo wake wa kisera kuhusu mambo yanayohusu wanawake.”

“Katika Ilani, kuna mambo yametoka katika sera na kuingizwa katika Ilani na Chadema ikishinda uchaguzi mkuu, yatachukuliwa haya kwenda sera,” anasema Mdee

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!