Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Uchaguzi Mkuu 2020: NEC, vyombo vya usalama viwabane wanaodhalilisha wanawake
Habari za Siasa

Uchaguzi Mkuu 2020: NEC, vyombo vya usalama viwabane wanaodhalilisha wanawake

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben
Spread the love

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyombo vya dola nchini Tanzania, vimetakiwa kuchukua hatua kali dhidi ya wanasiasa na watu wanaotoa lugha za udhalilishaji kwa wanawake wanaoshiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)

Pia, jumuiya za wanawake ndani ya vyama vya sisasa, vimetakiwa kuvunja ukimya na kuhakikisha hoja za rushwa mbalimbali ikiwemo ya ngomo inazungumzwa katika kila vikao vya jumuiya na vikao vingine muhimu.

Hayo yamesemwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) pamoja na Global Peace Foundation (GPF) katika tamko lao kuelekea uchaguzi mkuu.

Akisoma tamko hilo leo Jumatano tarehe 12 Agosti 2020 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben amesema, asasi hizo ziliendesha midahalo kutoka vyama vya siasa, viongozi wa dini, wanawake wanasiasa na waandishi wa habari chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake Afrika, (AWDF) kupitia mradi wa ‘Wanawake Sasa.’

Rose amesema, kupitia midahalo hiyo, wamebaini bado kuna changamoto zinazosababisha ushiriki mdogo wa wanawake katika siasa na kuvitaka vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, kuondoa changamoto hizo.

Amebainisha baadhi ya changamoto zinazowakabili wanawake katika siasa ni lugha dhalilishi zinazowavunja moyo wanawake wanaogombea au walio katika nafasi za uongozi pamoja na familia zao kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

“Wanawake wanaogombea nafasi za uongozi, hukutana na changamoto ya lugha dhalilishi wakati wa kampeni na hata wakati wa utendaji wao wa kazi ili tu kuwakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma.”

“Kama tunataka uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia, ni muhimu kwa tume ya uchaguzi na vyombo vya usalama kupiga marufuku na kutoa adhabu kali kwa wanasiasa watakaotoa lugha hizi dhidi ya wanawake,” amesema Rose

Rose amesema, katika midahalo hiyo, wamebaini kuwepo kwa rushwa ya kifedha katika shughuli za kawaida za siasa na hasa wakati wa chaguzi mbalimbali za ndani ya vyama, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

“Hii ni pamoja na tabia za wajumbe wanaotegemewa kupiga kura kuwa na hulka ya kudai au kujenga mazingira ya kupewa “kitu kidogo” ili waweze kutoa ushirikiano kwa mgombea.”

“Hii inaathiri wanawake ambao wengi wao hawana kipato cha kutosha hasa wanawake vijana,” amesema.

Rose amesema “tumebaini uwepo wa vitendo vya kuomba au kutengeneza mazingira ya rushwa ya ngono kwa baadhi ya wanaume wenye dhamana za kusimamia michakato ya chaguzi au mamlaka ndani ya vyama vya siasa.”

Amesema, changamoto hiyo husababisha wanawake kudhalilishwa na kuharibiwa ndoto zao za kisiasa na wakati mwingine familia au wenzi wao kuwazuia kushiriki katika siasa.

Mkurugenzi huyo amesema, hayo na mengine mengi, yanachangia wanawake, kuvunjika moyo hivyo kutoshiriki shughuli za siasa au kukosa nafasi za uongozi pale wanapokuwa na msimamo wa kutotoa rushwa.

“Katika hili tunapenda kutoa rai kwa wanawake wenzetu kukataa kabisa kudhalilishwa na kutojihusisha na vitendo vya rushwa ya fedha au ngono,” amesema

“Pia, tunashauri jumuiya za wanawake ndani ya vyama vya sisasa kuvunja ukimya na kuhakikisha hoja za rushwa katika siasa inazungumzwa katika kila vikao vya jumuiya na vikao vingine muhimu.”

Rose amesema “tunaviomba vyama vya siasa viweke utaratibu madhubuti na wa siri wa kutoa taarifa za vitendo hivi na kuwe na kamati huru ndani ya vyama zisizofungamana na yeyote zitakazoratibu upokeaji, ufuatiliaji na utoaji adhabu kwa wale ambao bado wanaendekeza vitendo hivi vya kuwadhalilisha wanawake.

Cecilia Augustino Mwanga wa Demokrasia Makini

Kuhusu ushiriki wa wanawake, Rose amesema ni jambo zuri kwamba kati ya wagombea 16 waliojitokeza kuchukua fomu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuteuliwa kugombea urais, wanawake ni wawili huku nafasi ya wagombea wenza wakiwa watano.

Wagombea hao ni Queen Cathbert Sendinga wa Chama cha ADC na Cecilia Augustino wa Demokrasia Makini.

Rose amevitaka, vyama vya siasa kuwateua wanawake waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali kama za udiwani, ubunge na uwakilishi ili wagombee kwenye uchaguzo huo.

“Tunapenda kuvipongeza vyama vya siasa ambavyo vimetoa nafasi za wanawake kugombea nafasi za udiwani na ubunge na hata urais katika kura za maoni.”

“Mwaka huu wanawake wengi wamejitokeza. Tungependa kuviomba vyama vya siasa kuhakikisha wale wanawake wenye uwezo wasimamishwe kugombea nafasi hizo,” amesema

Katika hilo, Rose amesema, “tunawaomba wananchi wote kuwachagua wanawake waliosimamishwa kugombea nafasi za ubunge na udiwani na wengine wapewe nafasi za teuzi mbalimbali.”

Ametumia fursa hivyo, kuvikumbusha vyama kuendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake ambao hawakupata nafasi mwaka huu ili waweze kusimama na kugombea chaguzi zijazo ndani ya vyama vyao, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Qeen Cuthbert Sendiga-ADC

“Kadhalika tunapenda kuwaasa wanawake kuepuka kugawanywa na zile kauli kuwa, ‘hawapendani’ badala yake waendelee kushirikiana na kupeana fursa mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na masuala ya kijamii,” amesema

“Kauli hizi za kuwa ‘wanawake hatupendani’ si za kweli bali zimekuwa zikitumika katika jamii kuwagawa wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi,” amesisitiza

Rose amegusia kauli zilizotolewa na Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli, viongozi wa vyama mbali mbali na tume ya taifa ya uchaguzi kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa ni huru, haki na wa amani.

“Tunawakumbusha wagombea wote kuhakikisha kuwa hawatoi kauli zozote za uvunjifu wa amani, kuchochea vurugu, kuwagawa watu kwa dini au makabila yao au matusi na udhalilishaji wa kijinsia kwa wagombea wengine,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!