Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Uchaguzi 2020: Kamati Kuu ACT-Wazalendo yaweka msimamo 
Habari za Siasa

Uchaguzi 2020: Kamati Kuu ACT-Wazalendo yaweka msimamo 

Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo
Spread the love

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimetangaza kwamba, kitalinda ushindi wake kwa gharama zozote katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Katika maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho yaliyotangazwa leo tarehe 22 Juni 2020, Ado Shaibu ambaye ni Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, amesema kamati hiyo imeagiza chama hicho kulinda ushindi wake kwa gharama yoyote.

Msimamo huo umetolewa baada ya kamati hiyo kujadili Ripoti ya Sekretarieti ya ACT-Wazalendo kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, katika  kikao chake kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.

“Kamati Kuu ya chama imesisitiza msimamo wa chama, kuwa uchaguzi mkuu wa 2020 utakuwa wa kufa na kupona. Chama kitahakikisha kinaulinda ushindi wake kwa mbinu zote halali na kwa gharama zozote,” amesema Ado.

Pia amesema, kamati hiyo imeridhia uamuzi wa viongozi wa ACT-Wazalendo kufanya mazungumzo na vyama vya siasa vya upinzani, vyenye nia ya dhati kushirikiana katika uchaguzi huo.

“Kamati Kuu imeridhia chama kufanya mazungumzo ya ushirikiano na vyama makini vya upinzani, ili kuingo’a CCM madarakani na kuleta mabadiliko yatakayowaletea Watanzania maendeleo,” amesema Ado.

Na kwamba, kamati hiyo imeagiza wasimamizi wa mchakato wa uchaguzi huo ndani ya ACT-Wazalendo, kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa kufuata misingi ya chama hicho.

“Kamati Kuu imewaagiza wasimamizi wote wa mchakato wa uchaguzi wa kila ngazi kuhakikisha kuwa uteuzi wa wagombea wa ACT Wazalendo unafanyika kwa kufuata misingi ya chama; uhuru, haki, usawa na uwazi,  ili kusimamia demokrasia kwa vitendo kama ulivyo utamaduni wa ACT Wazalendo,” amesema Ado.

Wakati huo huo, Ado amesema Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo imefungua rasmi mchakato wa uteuzi wa wagombea wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, utakaoanza tarehe 1 hadi 13 Julai 2020.

Akitangaza ratiba ya mchakato huo, Ado amesema tarehe 11 Julai 2020 Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo itafanya mkutano wake, kisha utafuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho, kitakachoketi tarehe 1 Agosti 2020.

Mkutano Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo utakaofanyika tarehe 2 Agosti 2020, utahitimisha mchakato huo kwa kuwapitisha wagombea urais wa pande zote mbili, Tanzania na Zanzibar.

“Hivyo basi, ninapenda kuchukua fursa hii kuwatangazia wanachama wote wa ACT Wazalendo wenye nia ya kugombea kwenye nafasi za Udiwani, Ubunge, Uwakilishi na Urais wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakachukue fomu ifikapo tarehe 01 Julai 2020 hadi 13 Julai 2020,” amesema Ado.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!