July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Tundu Lisu: Nitagombea urais

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

TUNDU Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maaendeleo (Chadema)-Bara, amesema atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, ataandika barua ya kuomba ridhaa ya chama chake kugombea kiti cha urais kwenye uchaguzi huo na kwamba, wakiona inafaa na kumpitisha, yupo tayari kupeperusha bendera ya chama hicho

Akizungumza na Mwanahalisi Online leo Jumatano tarehe 3 Juni 2020, lililotaka kujua kama anao mpango wa kugombea urais ndani ya chama chake.

“Nilikuwa nasubiri baraza za chama, nitaandika barua ya kuomba ridhaa ya chama changu nigombee urais,” amesema Lissu

Mapema leo Jumatano, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ametangaza kufunguliwa kwa milango kwa wanachama wa chama hicho, wanaotaka kuwania urais kuandika barua kwa katibu mkuu.

Mnyika amesema, milango hiyo imefunguliwa kuanzia leo hadi tarehe 15 Juni 2020 kisha baada ya hapo, watakaokuwa wamejitokeza watapelekwa kamati kuu ya chama hicho kwa hatua zaidi za ndani.

Baada ya tangazo hilo la Mnyika, MwanaHALISI ONLINE limezungumza na Lissu kwa simu akiwa nchini Ubelgiji ambaye amesema, “kama mwanachama mtiifu wa Chadema, nilikuwa nasubiri uongozi wa chama unaohusika, utoe baraka zake kwa wanachama kuanza mchakato wa uchaguzi.”

Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki amesema, “kwa vile hizo baraka zimekwisha kutolewa na kwa vile nimekuwa natajwa tajwa na najitaja taja, basi nitafanya kitu ambacho nimekuwa nakisemasema.”

Lissu ambaye amewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) amesema, “nitamwandikia barua rasmi katibu mkuu wa chama ili kutoa tangazo rasmi kwake.”

“Na vilevile, nitazungumza na umma wa Watanzania na wengine wanaotutakia mema baada ya kuwa nimetangaza nia rasmi na kwa uchache, maswala muhimu ninayoyaona katika uchaguzi huu kwenda mbele,” amesema.

Katika kusisitiza hilo, Lissu amesema, “Nafikiri nitafanya hivyo ndani ya muda huu ambao umetolewa na chama wa kufanya hivyo na kwa vyovyote vile sitawachelewesha.”

Akijibu swali aliloulizwa na MwanaHALISI ONLINE anarejea lini nchini, Lissu amesema, “suala la kurejea nchi linashughurikiwa na wakati mwafaka utakapofika wananchi watapata taarifa.”

Amesema, sheria za Tanzania hazijazungumzia mtu akiwa nje ya nchi hiyo kwa kipindi fulani hatoweza kugombea hivyo hana wasiwasi na hilo.

“Kama nitakuwa mgombea urais kwa niaba ya chama lazima nitakuja Tanzania,” amesema

Lissu amekuwa nje ya Tanzania tangu tarehe 7 Septemba 2017, aliposafirishwa kwenda Hospitali ya Nairobi, Kenya kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma.

Mwanasiasa huyo alifikwa na mkasa huo, akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge lililokuwa likiendelea jijini humo.

Alipata matibabu Nairobi hadi tarehe 6 Januari 2018 alipohamishiwa Ubelgiji aliko mpaka sasa kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo, Lissu amekwisha kusema, amepona na anachosubiri ni kuhakikishiwa mazingira salama ya maisha yake ili yasije kujitokeza kama yaliyomkuta awali.

error: Content is protected !!