January 27, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Tundu Lissu: Kazi ya kudai haki inaendelea vizuri

Tundu Lissu akipokewa na mke wake

Spread the love

TUNDU Antipas Lissu, aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu uliyopita, bado yuko kwenye makazi yake nchini Ubelgiji na anasema, “mapambano yanaendelea.”

Lissu ambaye aligombea nafasi hiyo, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yuko nchini Ubelgiji alikosema, amekwenda kujinusuru maisha yake.

Katika mahojiano yake na mwandishi wa habari hizi, Lissu amesema, “anasema, “pamoja na kuwapo kwangu ughaibuni, lakini mapambano ya kudai haki, utawala wa sheria na demokrasia katika nchi yangu, siwezi kuyasahau.”

Amesema, “hata huku niliko, bado ninafanya kazi ya kisiasa. Ninazunguuka maeneo mbalimbali, kuomba jumuiya za kimataifa, kushinikiza utawala wa Rais John Magufuli, kushinikiza kuheshimu haki za binadamu.”

Amesema, kama nilivyoeleza wakati naondoka nchi mwangu, kwamba siendi nje ya nchi kukimbia mapambano; bali nakwenda Ubelgiji kutafuta uwanja mwingine wa kudai haki. Amesema, “naomba kueleza sasa, kwamba kazi hiyo, inakwenda vizuri.”

Mwanasiasa huyo machachari nchini Tanzania aliondoka jijini Dar es Salaam, kuelekea Ubelgiji, alikokuwa akiishi karibu miaka miwili kwa ajili ya matibabu, tarehe 10 Novemba 2020.

Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, Lissu alisindikizwa na maofisa wa ubalozi wa Ujerumani na Marekani.

Lissu alidai kuwa amelazimika kuondoka nchini kufuatia kupokea vitisho juu ya usalama wake, hali iliyomfanya yeye na wasaidizi wake watatu, kukimbilia nyumbani kwa balozi wa Ujerumani, jijini Dar es Salaam, kuomba hifadhi.

Alitoa madai hayo, mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa 28 Oktoba 2020. Katika uchaguzi huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilimtangza mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli kuwa mshindi.

Lissu alitangazwa kupata kura 1.9 milioni, huku Magufuli akipata kura 12 milioni. Watu 15 milioni walipigakura.

error: Content is protected !!