January 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Tuhuma Mil. 1 yawafikisha kortini mganga mkuu, mfamasia Rombo

Spread the love

DK. Christon Nkya, aliyekuwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Rombo mkoani Kilimanjaro na mfamasia wa zamani wa halmashauri hiyo, Remig Massawe, wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali ikiwamo kughushi na kujipatia Sh.1.58 milioni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea)

Dk. Nkya ambaye kwa sasa ni mstaafu na Massawe ni mfamasia wa Halmashauri ya Mbozi mkoani Songwe, walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Rombo tarehe 2 Juni 2020.

Katika taarifa yake kwa umma, iliyotolewa jana Ijumaa tarehe 5 Juni 2020 na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Kilimanjaro, Fidelis Kalungura alisema, watuhumiwa hao walifiksihwa mahakamani kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Alisema, watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka wa Takukuru, Furahini Kibanga na kufunguliwa kesi ya jinai Na.1/2020 mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Regina Futakamba.

Wawili hao, wanashtakiwa kwa makosa matatu, kughushi kinyume na kifungu cha 33, 335(a) na 337 vya sheria ya kanuni za adhabu, matumizi mabaya ya mamlaka kinyume na kifungu cha 31 na kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22.

“Vyote vya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007. Jumla ya fedha inayohusika ni Sh.1,588,000,” alisema Kalungura.

Alisema, washtakiwa wote wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na mahakama ya kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika, watakaotia saini bondi ya Sh.1 milioni kila mmoja.

error: Content is protected !!