Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa TLS yatoa tamko kupinga mahabusu kufanyishwa kazi
Habari za Siasa

TLS yatoa tamko kupinga mahabusu kufanyishwa kazi

Spread the love

CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimeiomba Serikali ya Tanzania, kusitisha mpango wake wa kufanyisha kazi mahabusu, kwa kuwa unakwenda kinyume na Katiba ya nchi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Tarehe 31 Mei 2020, Serikali ya Tanzania kupitia George Simbachawene, Waziri wa Mambo ya Ndani, alisema Serikali iko mbioni kuanzisha mfumo ambao utawawezesha mahabusu kufanya kazi, ikiwemo kazi za kilimo, ili wapate chakula.

Simbachawene alisema Serikali iko katika mjadala wa kuangalia namna gani mahabusu watafanya kazi tofauti na wafungwa, huku akisisitiza kwamba, hawatafanyishwa kazi za kutweza utu wao.

“Hatutaki kuwatumia kwa ajili ya kuwafanyisha kazi zinazotweza utu wao, wao wana adhabu wanazotumika lakini tunataka kuwatumia kuzalisha, tutawafanyisha kazi kama watu wengine wanavyofanya kazi hilo lazima lieleweke na sio tunataka kuwatumia mahabusu kama wafungwa,“ alisema Simbachawene

“Ingawa  kuna mjadala mkubwa, ila matumizi ya mahabusu na kuwaangalia huo mjadala bado upo tunaendelea kuchakata lakini tutakuja na majibu na mapendekezo kisha tutashirikiana, lakini tunataka kuwatumia kwa nia njema ya kuzalisha sababu imeandikwa katika vitabu vitakatifu asie fanya kazi na asile,” alisema

Dk. Rugemeleza Nshala, Rais wa TLS jana Ijumaa tarehe 5 Juni 2020 alitoa tamko akizungumzia kauli hiyo ya Waziri Simbachawene akisema, utekelezwaji wa mpango huo, utakuwa ni kinyume na misingi ya haki za binadamu.

“Nchi yetu inatakiwa kuwa katika mstari wa mbele katika kukuza, kuheshimiwa haki za watu na wanadamu na si kurudi katika zama za kikoloni ambapo mtuhumiwa hakuthaminiwa kwa kuchukuliwa kama mkosaji, hadi hapo atakapothibitishwa hana hatia,” alisema Dk. Nshala

“Kumfanyisha kazi mahabusu ni kumtweza mtu na kumpa adhabu wakati bado hajatiwa hatiani na kunaweza kuchagiza kuwekwa ndani watu wengi kwa makosa ya kuwabambikia, ili kuwakomoa na kuwatweza.”

Dk. Nshala alisema, “hilo ni kosa kubwa ambalo historia haitotusamehe wote kwa kuliruhusu kuwa sehemu ya sheria zetu.”

Aliitaka Serikali ya Tanzania, kuboresha mfumo wa utoaji haki, ili kupunguza gharama za kuwahudumia mahabusu, badala ya kuwafanyisha kazi ili wajihudumie wenyewe.

“TLS tunaitaka Serikali kusitisha mara moja mpango wake badala yake ijikite katika kuboresha mfumo wa utoaji haki, kwa haraka ili kupunguza gharama za kuwahudumia mahabusu,” alisema Dk. Nshala.

TLS ilisema,  njia nzuri ya kuwa na watuhumiwa wa makosa ya jinai ambao wanajitafutia chakula chao cha kila siku ni kuhakikisha watuhumiwa wanapata dhamana.

“Dhamana iwe haki ya kila mtuhumiwa. Sheria zote ambazo zinazuia kutolewa kwa dhamana kwa watuhumiwa zifanyiwe marekebisho na ikiwa ni pamoja na makosa ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na makosa yote yaliyoainishwa na kifungu cha 148(5)(a)(i) –(vi)-(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai Namba 20 kama ilivyorejewa Mwaka 2002,” alisema Dk. Nshala

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!