Tanzania yatumia trilioni 1.1 kumaliza mgawo wa umeme

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imetumia Sh.1.1trilioni kumaliza tatizo la mgawo wa umeme. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Hayo amesema na Dk. Hassan Abbasi, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania leo Jumamosi tarehe 15 Agosti 2020, wakati anazungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, katika sekta ya nishati.

Dk. Abbasi amesema, kiasi hicho cha fedha kilitumika katika ujenzi wa miradi mikubwa miwili ya umeme wa gesi, upanuzi wa Kinyerezi I na Kinyerezi II, Dar es Salaam.

“Katika kipindi hiki cha miaka mitano, Serikali imeongeza uzalishaji umeme ambao ulikuwa changamoto kubwa ya miaka mitano iliyopita ya mgawo wa umeme,” amesema Dk. Abbas

“Sasa mnafahamu hata ile hadithi iliyokuwa inasimuliwa na magazeti yetu miaka mitano iliyopita ya mgawo wa umeme sasa ni historia, umeme ukikatika ni kutokana na sababu za kiufundi na sio kukosekana kwa umeme,” amesema.

Dk. Abbasi amesema, mradi wa upanuzi wa Kinyerezi I unaozalisha Megawati 185 uligharimu Sh. 315.4 bilioni wakati wa Kinyerezi II unaozalisha megawati 248.22, ambao unagharimu Sh. 794 bilioni.

“Kufikia Desemba mwaka huu, jumla ya mewagawati 583.22 za umeme wa gesi zitakuwa zimeingizwa kwenye Gridi ya Taifa,” amesema Dk. Abbasi.

Dk. Abbas ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema, utekelezaji wa miradi hiyo imeongeza uzalishaji wa umeme kutoka Megawati 1,308 mwaka 2015 hadi Megawati 1,602.32 hadi kufikia Julai 2020 na kupelekea nchi kuwa na akiba ya umeme ya Megawati 300.

“Utekelezaji wa miradi hiyo imesaidia sana nchi yetu kuwa na bakaa ya umeme, kwa sasa ina akiba ya umeme kutokana na umeme mwingi tuliozalisha lakini sio wote unatumika sababu matumizi hayajafika megawati 1600, Tanzania ina bakaa ya megawati 300,” amesema Dk Abbasi.

Licha ya mafanikio hayo, Dk. Abbas amesema, Serikali imefanikiwa kuongeza ufanisi wa utendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ambapo linajiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini pamoja na kupata faida.

“Kwa mara ya kwanza tangu Uhuru, mikoa ya Lindi, Mtwara, Njombe na Ruvuma imeingia katika Gridi ya Taifa na kusaidia kuachana na kutumia mitambo ya mafuta mazito iliyokuwa inaigharimu Tanesco Sh. 15.3 Bil. kwa mwaka katika mikoa hiyo,” amesema Dk. Abbasi.

Dk. Abbasi amesema “Sanjari na mitambo ya mikoani kuzimwa, Tanesco pia iliachana na kununua umeme kutoka mitambo binafsi ya mafuta mazito na kuliwezesha shirika kuokoa matumizi ya Sh. 118.175 Bil.”

Sambamba na hilo, Dk. Abbasi amesema, Serikali imefanikiwa kutekeleza mpango wa usambazaji umeme vijijini, na kwmaba hadi kufikia mwezi Julai 2020 jumla ya vijiji 9,412 vimeunganishwa na umeme kutoka vijiji 2,018 mwaka 2015.

“Hii ni ongezeko la vijiji 7,394. Jumla ya Sh. 2.29 trilioni zimetumika kutekeleza mradi huo, ambapo Sh.1.78 trolioni ni fedha za ndani na Sh.515.71 bilioni ni fedha za nje kutoka kwa washirika wa maendeleo,” amesema Dk. Abbasi.

SERIKALI ya Tanzania imetumia Sh.1.1trilioni kumaliza tatizo la mgawo wa umeme. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea). Hayo amesema na Dk. Hassan Abbasi, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania leo Jumamosi tarehe 15 Agosti 2020, wakati anazungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, katika sekta ya nishati. Dk. Abbasi amesema, kiasi hicho cha fedha kilitumika katika ujenzi wa miradi mikubwa miwili ya umeme wa gesi, upanuzi wa Kinyerezi I na Kinyerezi II, Dar es Salaam. “Katika kipindi hiki cha miaka mitano, Serikali imeongeza uzalishaji umeme ambao ulikuwa…

Review Overview

User Rating: Be the first one !

About Regina Mkonde

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!