January 27, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Takukuru yaiokoa Tanesco, yawaonya wakandarasi 16

Brigedia Jenerali, John Mbungo, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru

Spread the love

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania, imerejesha vifaa ghafi vya umeme vya zaidi ya Sh.1.2 bilioni kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Anaripoti Mwandishi Wetu, Iringa … (endelea).

Makabidhiano ya vifaa hivyo, yalifanyika jana Jumanne tarehe 29 Desemba 2020, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo alivikabidhi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA), Amos William Maganga.

Mbungo alisema, kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007, Takukuru kupitia kurugenzi ya ya uzuiaji rushwa wanalo jukumu la kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Alisema lengo ni kujiridhisha iwapo miradi hiyo ilitekelezwa kwa mujibu wa mikataba iliyoingiwa kati ya REA na wakandarasi waliopata zabuni za kutekeleza miradi hiyo na iwapo thamani ya fedha iliyotumika inaendelea na ubora wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Mbungo alisema, kutokana na sababu hiyo, Miezi mitano iliyopita – Julai 2020, Takukuru ilianzisha operesheni kwenye Miradi ya Usambazaji wa Umeme vijijini – Awamu ya pili (REA II) mradi ambao uko chini ya REA.

Alisema, mpaka jana operesheni hiyo ilikuwa imeshafanyika katika mikoa mitano ya Geita, Iringa, Pwani, Morogoro na Kagera.

“Kwa mujibu wa mikataba kila mkandarasi, ana wajibu wa kurejesha Tanesco vifaa ghafi vya umeme vinavyobaki baada ya mkataba kukamilika. Vifaa hivi ni vile ambavyo ni Mandatory Spare Parts and Materials remained for uncovered scopes,” alisema Mbungo

Bosi huyo wa Takukuru alisema, katika mikoa mitano iliyofanyiwa kazi – wakandarasi hawakukabidhi Tanesco vifaa ghafi vyenye thamani ya zaidi ya Sh.4.35 bilioni licha ya kukumbushwa mara kwa mara kufanya urejeshaji huo na kupewa notisi ya kufanya hivyo mwaka 2017.

Alisema, vifaa ghafi vilivyokabidhiwa jana kwa Tanesco ni kutokana na operesheni ya uchunguzi wa Miradi ya REA II iliyofanyika katika mkoa wa Iringa.

Vifaa ghafi hivyo ni pamoja na: Transfoma 34 zenye ukubwa tofauti, Mita za Luku 1,458 na vifaa vyake, nyaya zenye urefu wa km 70.8 pamoja na vifaa 30 vya umeme (Ready boards) vya aina tofauti tofauti.

“Vyote vikiwa na thamani ya Sh.1.2 bilioni,” alisema Mbungo

“Natumia hadhira hii kutoa rai kwa wakandarasi 16, ambao walipelekewa notisi na REA tangu mwaka 2017 lakini bado hawajawasilisha vifaa ghafi hivyo katika ofisi za Tanesco kama Notisi walizopokea zinavyowataka kufanya. Ninawaagiza kwamba wahakikishe wamerejesha vifaa ghafi hivyo ndani ya siku 14 kuanzia jana Jumanne,” alisema Mbungo.

error: Content is protected !!